Wednesday, October 15, 2014

Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa Godfrey Zambi (MB) afungua maadhimisho ya siku ya SACCOS duniaNaibu Waziri wa  Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa Godfrey Zambi (MB)  amefungua maadhimisho ya siku ya SACCOS dunia yaliyofanyika mkoani  Dar es Salaam kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.
Maadhimisho hayo ya siku ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo huadhimishwa dunian kote  kila alhamisi ya tatu ya mwezi Oktoba kila mwaka, sherehe hizo zitafanyika kwa  siku tatu ambapo kutakuwa na maonyesho ya kazi na huduma mbalimbali zitakazotolewa na SACCOS na  wadau wake. Lakini  pia sherehe hizo zitaambatana  na shughuli mbalimbali za kuwaenzi Waasisi wa SACCOS hizo.
Mheshimiwa Zambi  alitoa rai kwa wanachama hao, ili kufikia malengo yao waliojiwekea inabidi wafanye kazi katika vikundi ili kurahisisha kazi kwa Serikali kutekeleza kwa urahisi mahitaji yao pale inapobidi, lakini pia aliwashauri wanachama hao wawe na jukwaa la kuzungumza mambo yao ili kurahisisha mawasiliano na Serikali kwani kila mwanachama akiwa na  mtazamo wake na kufanya mambo yake peke yake, serikali itapata ugumu katika kufikia azma yake.
Naibu  Waziri aliweka msisitizo, kwa wanachama wa SACCOS kuendeleza kuziimarisha kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia kanuni kuu ya SACCOS  inayosema ‘Weka akiba mara kwa mara kopa kwa busara na lipa kwa wakati’ kanuni hii itawezekana tu kwa kuzingatia sheria, kanuni masharti na sera mbalimbali zinazosimamia vyama vyetu.
Aidha Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza jinsi SACCOS zilivosaidia kutatua matatizo ya wananchi waliowengi  kiuchumi na kijamii katika maeneo ya vijijini na mijini. Umuhimu wa SACCOS  katika sekta mbalimbali umekuwa na mvuto si tu kwa Wananchi bali pia kwa Wanasiasa Wafadhili na Taasisi pamoja na Asasi mbalimbali.
Naibu Waziri Mheshimiwa Godfrey Zambi aliwapongeza Wanachama hao kwa kuona umuhimu wa SACCOS na kuweza kujitoa kwa hali na mali kufanikisha maadhimisho hayo.

Saturday, October 11, 2014

Wizara Yatilia Saini na Benki za Wananchi Kuwakopesha Wakulima

Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika leo imetia saini makubaliano na Benki za Wananchi tisa yenye lengo la kuwakopesha wakulima fedha za kununulia pembejeo za kilimo nchi.
Benki hizo ni Benki ya Wananchi Njombe (Njombe) Benki ya Wananchi Mwanga (Kilimanjaro), Benki ya Wananchi Tandahimba (Mtwara), Benki ya Wananchi Mbinga(Ruvuma), na Benki ya Wananchi Mufindi (Iringa).

Nyengine ni Benki ya Wananchi Kilimanjaro (Kilimanjaro), Benki ya Ushirika Kagera (Kagera) na Benki ya Wananchi ya Uchumi (Kilimanjaro).

Hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo ilifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu, Bibi Sophia Kaduma.
Katibu Mkuu aliongeza kuwa, chini ya utaratibu huo, wakulima watakopeshwa fedha kupitia Benki hizo, na watapaswa kurejesha kiasi walichokopeshwa, pamoja na riba ya asilimia 18. Serikali itamsaidia mkulima kwa kumlipia asilimia 14 huku wakulima wakilipa asilimia nne tu ya riba kwa kila mkopo uliochukuliwa na vikundi hivyo.
Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bibi Sophia Kaduma akitia sahini mkataba wa makubaliano ya utaratibu mpya wa kuwawezesha wakulima kupata pembejeo kwa kuwakopesha mikopo kupitia Benki za Wananchi. Akishuhudia tukio hilo ni Naibu Katibu Mkuu, Eng. Raphael Daluti

Katibu Mkuu aliongeza, kuwa huu ni utaratibu mpya ambapo sasa Serikali imeboresha mfumo wa utoaji wa ruzuku kwa mfumo wa vocha na badala yake sasa wakulima waliojiunga katika vikundi, watakopeshwa fedha za kununulia pembejeo kutoka katika Benki hizo.

Bibi Kaduma aliongeza kuwa, makubaliano ya leo ni mwanzo wa safari ya kuwasaidia wakulima kupitia Benki za Wananchi na kwamba Wizara ipo mbioni kutiliana saini na Benki ya CRDB na NMB.

Alisema, Benki ya CRDB na NMB zitaongeza wigo wa kuwasaidia wakulima wengi kwa kuwa zina matawi mengi na mtandao mkubwa, ambao utasaidia kuwafikia wakulima wengi nchini.

“Juhudi hizi ni mwanzo tu wa kumsaidia mkulima lakini Wizara inamsaidia mkulima kuanzia hatua ya uzalishaji na baadae kumtafutia masoko, lakini wito wetu ni kuwa ni vyema kama wakulima watajiunga katika vikundi vya ushirika ili wawe na sauti moja” Alikariri Katibu Mkuu.

Wawakilishi wa Benki za Wananchi walioshiriki katika tukio la kutiliana sahini makubaliano ya kuwakopesha wakulima mikopo kupitia vikundi, wakifuatilia maelezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bibi Sophia Kaduma

Bibi Kaduma, alimalizia kwa kusema, uzalishaji wa mazao ya chakula kama mahindi na mpunga umefikia asilimia 125. Mathalani uzalishaji wa mahindi umefikia ziada ya tani milioni 1.5.  Ongezeko hilo limetokana na juhudi za Serikali za kumwezesha mkulima ili aongeze uzalishaji.


Alimalizia kwa kusema, Serikali imeongeza msukumo, kwa kumtafutia mkulima masoko, na kwamba Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza ameonyesha njia kwa kutembelea nchi ya Sudan Kusini, Kenya kwa lengo la kutafuta masoko.

Friday, October 10, 2014

Naibu Waziri Zambi aishauri NFRA kuwapa kipaumbele Wakulima

Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa, Godfrey Zambi  akiongea na wakulima  wa mkoa wa Arusha, waliopeleka mahindi katika kituo cha ununuzi wa mahindi cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) huko, Kateshi Mkoani Arusha.


Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Mheshimiwa, Godfrey Zambi ameushauri uongozi  wa Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Arusha kutoa kipaumbele kwa kununua mahindi ya wakulima wadogo.
Mhe. Zambi alitoa wito huo wakati alipotembelea Kituo hicho cha ununuzi wa mahindi, Kituo kinachomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, huko Kateshi wakati alipokuwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani humo, wakati huohuo aliwashauri wakulima wadogo kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kusaidiwa.
Naibu Waziri, Mhe. Zambi aliongeza kuwa ni vyema wakulima wajiunge katika vikundi vya ushirika ili Serikali na Taasisi za Fedha ziweze kuwasaidi kwa kununua mazao yao na pia kuwakopesha pembejeo za kilimo.
Naibu Waziri yupo kwenye ziara ya kikazi ya wiki moja, yenye lengo la kukagua shughuli mbali mbali za maendeleo, zinatekelezwa na Taasisi na Vituo vilivyo chini ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika katika Mkoa wa Arusha na Morogoro.

Thursday, October 9, 2014

Wizara Yapata Hati Safi Kwa Mara Nyingine

Bwana Burhan Shabani, Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi.
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imeibuka kuwa miongoni mwa tasisi za serikali zilizofanya vizuri katika shughuli za ununuzi hapa nchini kwa kushika nafasi ya sita kati ya taasisi 76 zilizofanyiwa ukaguzi kwa mwaka 2013/2014.

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ilichukua nafasi hiyo kwa  kufuata kikamilifu taratibu na Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011.

Taaarifa hiyo ilionyesha kuwa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ilitanguliwa  na nyingine za  TASAF, Ofisi ya Rais Utumishi, SUMATRA, TCRA na DAWASA.

Aidha, matokeo ya ukaguzi huo yanaonyesha ukaguzi ulifanywa  kulingana na makundi ambapo Wizara, Idara na Wakala ilifanyika kwa asilimia 71, Mamlaka na Mashirika ya Umma ilikuwa asilimia 68 na upande wa Serikali za Mitaa ukaguzi ulifanyika kwa asilimia 62.

Jumla ya mikataba iliyokaguliwa ilikuwa ni 4,532 yenye thamani ya shilingi bilioni 429.51 taarifa hiyo iliongeza.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi wa Wizara, Bwana Burhan Shaban alisema matokeo haya ni habari njema kwa Wizara kwa kuwa huu ni mwaka wa tatu mfululizo Wizara imekuwa ikifanya vizuri.  Alisema mwaka 2011/2012 ilipata alama 86, mwaka 2012/2013 ilipata alama 78 na mwaka 2013/2014 imepata alama 80 na kuwa Wizara pekee iliyo katika nafasi sita za juu.

Bwana Shaban aliongeza kuwa matokeo hayo mazuri yametokana na ushirikiano kati ya Idara ya Ununuzi ya Wizara na mihimili yake ambayo yote kwa pamoja imekuwa ikifanya kazi kwa kutegemeana. Alitaja mhimili hiyo kuwa ni Idara na Vitengo vinavyohitaji huduma na ununuzi, Kamati ya Uchambuzi, Afisa Masuhuli na Idara ya Ununuzi yenyewe.

Alitoa wito wa mihmili hiyo kuendelea kushirikiana na kuisoma Sheria mpya Na. 7 ya manunuzi ya mwaka 2011 ili kuendelea kuboresha utendaji wao wa kila siku na kuepuka kukwama kwa manunuzi yanayoihusu Wizara.  Aliongeza kuwa mhimili mmoja kama utashindwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati basi hali hiyo itathiri mchakato mzima 

Wednesday, October 8, 2014

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika ahuzuria mkutano wa FAO nchini Italia

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mhandisi Christopher K Chiza (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wengine wa mkutano wa FAO uliofanyika mjini Rome hivi karibuni . Mkutano huo ulizungumzia soko la mazao ya kilimo na bei.
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa Mhandisi Christopher K Chiza (Mb)  akitoa hotuba yake katika mkutano wa FAO uliojumuisha Mawaziri wa Kilimo wa nchi Wanachama.
Mheshimiwa Chistopher K Chiza (Mb) akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose’ Graziano da Silva katika ofisi ya Mkurugenzi huyo mjini Rome. Mkurugenzi  mkuu alitaka kujua kwa undani juu ya mafanikio ya kilimo nchini Tanzania,mara baada ya kusikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri ndani ya Ukumbi wa FAO mjini Roma
Mkurugenzi mkuu wa FAO Jose’ Graziano da Silva akisisitiza jambo mara baada ya kumkabidhi kitabu cha FAO Mheshimiwa Mhandisi  Christopher K Chiza Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika  Mheshimiwa Christopher  K Chiza akihojiwa na Waandishi wa habari mara baada ya kutoa hotuba yake katika mkutano wa FAO hivi karibuni