Thursday, January 29, 2015

TUMIENI TOVUTI KWA UMAKINI – NATAI

Mkuu wa Kitengo  cha Mazingira Shakwaanande Natai  akifungua mafunzo ya utumiaji wa Tovuti ya mazingira
Watumishi wakifuatilia hotuba ya ufunguzi

 Watumishi wakiwa katika mafunzo ya matumizi ya tovuti
 Mwezeshaji wa mafunzo ya tovuti Bw. Masudi Kisamfu
  Watumishi wakifuatilia mafunzo ya matumizi ya tovuti
 
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira cha Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bi.  Shakwaanande  Natai amewataka wadau wa kilimo kutumia Tovuti  ya Mazingira kwa manufaa zaidi ili kuleta tija.
Aliyasema hayo wakati akifungua  mafunzo ya utumiaji wa mtandao wa mazingira uliobuniwa na kitengo hicho katika ukumbi wa Afya ya Mimea  ( PHS)  wizarani.
“Tumefurahishwa na kukamilishwa kwa shughuli hii ambayo tuliingojea kwa muda mrefu na leo ni siku muhimu imefika” aliongeza Natai katika hotuba yake ya ufunguzi.
Aliwasihi  wadau kuitumia tovuti kwa lengo lililokusudiwa na si vinginevyo ili kuboresha huduma za kilimo kupitia mazingira.
Mafunzo haya yaliwajumuisha watumishi wa Wizara ya kilimo Chakula na Ushirika kutoka  katika   Idara na  Vitengo mbali mbali na kuratibiwa na Mhandisi Mazingira wa kitengo hicho Bi Jane Marwa.
 


Monday, January 26, 2015

CHIZA AINISHA MAJUKUMU YA WIZARA

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mhe Eng. Christopher Chiza ameanisha majukumu ambayo wizara inayafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kupata ufumbuzi.

Mhe Chiza alitoa kauli hiyo wakati akimkaribisha waziri mpya wa wizara Mhe Stephen Wasira kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete mwishoni mwa wiki.

Aliyataja majukumu hayo kuwa ni mgogoro wa kiwanda cha chai cha Mponde mkoani Tanga, malipo ya wakulima kwa mazao waliokopesha  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya  Chakula ( NFRA).

Jukumu lingine ni sakata la sukari hapa nchini inayoingia kwa magendo, Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufuji na suala la tuhuma ya wizi katika zao la Tumbaku.

Mhe Chiza alisema majukumu hayo yanafanyiwa kazi na alimtaka Mhe Wasira kuendelea  kuyafanyia kazi ili kupata ufumbuzi.


WASIRA AWASILI OFISI ZA WIZARA

Waziri mpya wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Mhe. Stephen Masatu Wasira akisalimiana na wafanyakazi wa wizara mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Wizara ya Kilimo


Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bi. Sophia Kaduma akitoa taarifa ya wizara kwa Waziri mpya Mhe. Stephen WasiraWaziri mpya wa Kilimo Chakula na Ushiriki Mhe. Stephen Wasira amewasili wizarani na kupokelewa kwa shangwe na wafanyakazi wa wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Bi. Sophia Kaduma.

Mhe.Wasira alipokelewa majira ya saa 6:30 katika viwanja vya wizara na moja kwa moja alienda ofisini kwake na kupokelewa na Waziri wa  zamani wa wizara hii Mhe. Eng. Christopher Chiza, ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji na Uwezeshaji.

Baada ya kupokelewa,  Mhe Wasira, alipokea taarifa fupi ya utendaji wa wizara katika mambo muhimu yaliyogusa Taifa.

Pia Mhe Wasira alipokea taarifa ya wizara toka kwa Katibu Mkuu Bi. Kaduma  inayohusiana muundo, majukumu na shughuli muhimu za wizara kwa ujumla.


Hii ni mara ya nne kwa Mhe Wasira kuiongoza wizara hii ambayo inabeba jukumu kubwa na zito la kuhakikisha usalama wa chakula hapa nchini, miaka aliyoongoza wizara hiyo ni mwaka 1989 – 1990, 2006 – 2008 kama waziri na pia kama Naibu Waziri 1973 – 1975. 

Wednesday, January 21, 2015

Huduma za Mgahawa zarejea Wizarani
Mgahawa huo utatoa huduma zake kuanzia asubuhi mpaka jioni kwa siku zote za kazi ambapo pia vyakula na vinywaji mbalimbali vimeandaliwa kulingana na mahitaji ya wateja waliopo.
 Hayo yalisemwa Meneja wa mgahawa huo  Bwana Daudi Masatu Machumi alipohojiwa na Kitengo cha Mawasiliano.
  “Napenda kuwatoa wasiwasi wateja wetu kwani uongozi huu ni mpya na tupo kwa ajili ya kumridhisha mteja, kwani wateja hao ndio sababu ya sisi kuwepo hivyo hatuna budi kufanya wapendavyo wao” Alisema Machumi
Aidha Machumi  alisema bei  za vyakula zitakuwa za chini ili kila mteja aweze kumudu gharama hizo.
Baadhi ya wateja wa mgahawa huo ambao hawakutaka kutajwa majina yao walidai kwamba ni kweli  huduma hiyo imeboreshwa na vyakula ni vya bei ya kawaida sana.
Aidha Meneja huyo amewakaribisha wafanyakazi wote wa Wizara na majirani waweze kufika kwenye Mgahawa hiyo na kijipatia huduma nzuri yenye  uhakika .
Huduma za mgahawa zimerejeshwa hapa wizarani baada ya matengenezo ya muda mrefu kukamilika.

Tuesday, January 20, 2015

Mradi wa Sukari Bagamoyo Waanza


Wataalamu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika wamekutana na timu kutoka  IFAD  katika ukumbi wa kilimo I kufanya upembuzi wa miundombinu  ya mradi wa sukari uliopo Bagamoyo mkoani Pwani.
Akiongea katika kikao hicho Naibu Katibu MKuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Dr Yamungu Kayandabila amesema jitihada zinafanywa na wizara ili mradi huo uweze kuanza kwa wakati.
Aidha upembuzi huo umefanyika kwa kuzingatia zaidi maeneo ya upatikanaji wa maji,athari za mazingira na  matumizi bora ya aridhi. Hata hivyo kikao kiliahirishwa mpaka muda mwingine  ambapo mambo mengine yataendelea kujadiliwa kwa kina zaidi.

Monday, January 5, 2015

Serikali Yajipanga Kulipa Deni la Makampuni ya Pembejeo

Kikao cha Wizara na makampuni ya Pembejeo 
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika iko kwenye maandalizi ya kulipa madeni kwa makampuni ya yaliyosambaza pembejeo hapa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa  na MKurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Bw. Twahir Nzallawahe katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara.

“Wizara italipa madeni yote yaliyobakia kwa makampuni ya pembejeo yanayofanya kazi na wizara ili kuboresha huduma kwa wakulima wetu” alisisitiza Bw. Nzallawahe

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika kikao hicho, serikali kwa msimu wa kilimo wa 2013/2014 ilikuwa inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 40 lakini hadi sasa deni hilo limebakia kiasi cha shilingi bilioni 10 tu.

Wizara iliitisha mkutano na makampuni ya pembejeo ili kubadilishana mawazo na uzoefu juu ya utendaji wa kazi zao za kila siku.

Jumla ya makumpuni sita yalihudhuria mkutano huo, ambayo ni Tanzania Fertilizers Company (TFC), Mea  Fertilizers (T) LTD,  China Pesticide (T) LTD, YARA (Tz), STACO Agrochemicals LTD na Africa Fertilizers LTD.

Mwisho wa kikao,  Bw. Twahir Nzallawahe aliwashukuru wajumbe wote kwa kufika kwao na pia kwa kutoa mchango wa mawazo yao mazuri yanayolenga kuboresha huduma kwa wakulima wetu ili kuinua kilimo hapa nchini.

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika na Balozi wa Ujerumani Wajadili Mpango wa Kuimarisha kilimo

Mhe. Egoni Kochanke na Mhe. Christopher Chiza 
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mhe. Christopher Chiza  ameiomba Serikali ya Ujerumani kuangalia namna Serikali hizi zitakavyoweza kushirikiana katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, miundombinu ya uhifadhi wa mazao pamoja na uimarishwaji na uendelezwaji wa mazao ya bustani hapa nchini.
Ili kufanikisha maswala haya Mhe. Chiza amesema kuwa katika kuimarisha sekta ya kilimo ushirikishwaji wa sekta binafsi baina ya Tanzania na Ujerumani  ni muhimu sana
Aidha, eneo lingine la ushirikiano ni katika  sekta ya mbegu ambayo inahitaji kuimarishwa  ili kuongeza matumizi ya  mbegu bora hapa nchini.

Naye Balozi wa Ujerumani Mhe. Egoni Kochanke   ametaka jitihada zifanyike ili sekta binafsi za nchi hizi mbili zikutane na kujadili fursa ambazo zimo katika maeneo yao.