Friday, March 13, 2015

ZAMBI ATEMBELEA OFISI ZA WIZARA                                 
Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mhe. Godfrey  Zambi ,ametembelea  Tume, Idara na Vitengo vilivyopo makao makuu ya wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika.
   Mhe  Zambi katika ziara hiyo  aliambatana na  Kaimu Mkurugenzi wa  Utawala na  Rasilimali watu  Bi. Mary Temba, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Bi. Hilda  Kinanga  na Maafisa habari toka Kitengo cha Mawasiliano  cha  Wizara.
Mhe Zambi alitembelea  ofisi kwa lengo la kufahamiana, kujua  utendaji wa kazi na kujua changamoto  zinazokabili Tume, Idara na Vitengo vilivyopo makao makuu ya wizara.
Aidha,  watumishi hao walibainisha  changamoto mbali mbali ikiwemo  uhaba wa fedha na kutofika kwa wakati na   pia suala la upungufu wa ofisi jambo ambalo linapelekea kupunguza ufanisi katika utendaji wa kazi za kila siku.
Changamoto nyingine kwa mujibu wa watumishi hao ni kuna upungufu  na uchakavu wa vitendea kazi, ambavyo vinachangia sana kutokufanya kazi kwa wakati.
Upande wa madereva wao kilio chao kilikuwa ni tatizo la sare na ofisi, wamemuomba  kushonewa sare waweze kutambulika kwa urahisi kama ilivyo kwenye  wizara nyingine lakini pia wameomba wajengewe  ofisi  na sio kukaa chini ya mti na kipindi cha mvua wanapata usumbufu wa hali ya juu.
Hii ni ziara ya kwanza ya Mhe. Zambi kuifanya ndani ya Wizara tangu ateuliwe kuwa Naibu wa Wizara  hapo mwaka jana.


Mheshimiwa Naibu Waziri Godfrey Zambi akiongea na watumishi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Mheshimiwa Naibu Waziri Godfrey Zambi akiongea na watumishi wa Kitengo cha  ICT


 Mheshimiwa Naibu Waziri Godfrey Zambi akiongea na watumishi wa Idara ya Sera na Mipango


 Mheshimiwa Naibu Waziri Godfrey Zambi akiongea na watumishi wa Idara ya Uhasibu
 Mheshimiwa Naibu Waziri Godfrey Zambi akiongea na  Madereva

Sababu za Kupanda kwa Gharama za Mbolea Zatajwa

Mkurugenzi wa Uendelezaji Mazao Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Twahir Nzallawahe akifungua mkutano wa Afya ya Mimea katika Hoteli ya LandMark Jijini Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa kuna sababu mbali mbali zinazochangia kuongezeka kwa gharama za mbolea kwa wakulima wetu wa Tanzania.
Hayo yamebainishwa katika mkutano wa Sera ya Afya ya Mimea uliofanyika Jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya LandMark .
Sababu hizo zilibainishwa na Dr Francis Mwaijande toka Chuo Kikuu cha Mzumbe wakati akiwasilisha Mada ya Mbolea na gharama zake, alizitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na upatikanaji wake, ni jinsi gani mfanyabiashara amepata mbolea ambapo bei inaweza kuongezeka au kupungua.
Usafirishaji nayo ni sababu tosha inayoweza kuwa dira ya upangaji wa bei za mbolea kwa mdau mkubwa ambaye ni mkulima, umbali na njia aliyotumia mfanyabiashara kusafirisha mbolea hadi kumfikia mtumiaji, inaweza kuongeza bei ya mbolea.
Shughuli za bandari nazo zimekuwa zikiongeza gharama za mbolea kwani kumekuwa na ukiritimba wa hali juu katika utoaji wa mbolea, kitu ambacho huongeza gharama kwa mwingizaji wa mbolea ambapo mwisho wa siku gharama zote zinamwelemea mkulima ambaye ni mtumiaji wa mwisho, aliongeza Dr Mwaijande
Mawakala wa Mbolea nalo ni chanzo pia cha kuongeza gharama za ununuaji wa mbolea kwa kukosa uaminifu kwani huongeza bei zao kufidia wanachoita gharama walizotumia.
Naye Profesa Evelyne Lazaro toka Chuo Kikuu cha Sokoine katika mchango wake aliomba njia mbadala zitafutwe katika kukabiliana na changamoto hizi ili kumpunguzia mkulima mzigo huu mzito wa bei za juu za mbolea.
Mkutano huo wa siku moja mada mbali mbali ziliwasilishwa katika mkutano huo zikiwa na lengo la kuendeleza kilimo na uliwashirikisha wadau mbali mbali kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Sekta Binafsi, Wakulima, Wafanyabiashara, watalaamu toka Chuo Kikuu cha Sokoine, Chuo Kikuu cha Mzumbe na nje ya nchi.

Wafanyabiashara Washiriki katika Kilimo – Komba


Wajumbe wa mkutano wakifuatilia mada
Mratibu wa Sera ya Afya ya Udongo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo toka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bw. Canuth Komba ameitika sekta binafsi hapa nchini kushiriki kikamilifu katika kuinua kilimo.
Komba alitoa wito huu wakati wa mkutano wa Sera ya Afya ya Udongo uliofanyika katika Hoteli ya LandMark Jijini Dar es Salaam, alisisitiza kuwa muda umefika kwa sekta binafsi kujikita kikamilifu katika kuboresha kilimo kwa manufaa ya wakulima wetu.
“ Serikali peke yake haiwezi kuinua kilimo chetu bila ushiriki wa sekta binafsi kikamilifu na hasa kwa wafanyabiashara wetu ambao ni nguzo muhimu katika uhakika wa soko la mazao ya wakulima.” alisisitiza Bw. Komba.
Wafanyabiashara ni watu muhimu sana katika kulisukuma gurudumu la kuinua sekta ya kilimo, aliongeza Komba.
Pia alifahamisha kuwa utafiti umefanyika kwa lengo la kuwashauri watunga sera wetu kuwa na sera ya matumizi bora na sahihi ya mbolea kwa wakulima.
Elimu kwa wadau wa kilimo juu ya matumizi sahihi ya mbolea ni muhimu sana katika kufikia lengo kubwa la kuongeza uzalishaji wa kilimo chetu.
Mkutano huo wa siku moja pia uliwashirikisha wadau mbali mbali kutoka Wizara Kilimo Chakula na Ushirika, Sekta Binafsi, Wakulima, Wafanyabiashara, Watalaamu toka chuo kikuu cha Sokoine, chuo kikuu cha Mzumbe na nje ya nchi.
Mada mbali mbali ziliwasilishwa katika mkutano huo zikiwa na lengo la kuendeleza kilimo kwa maslahi ya wakulima na taifa kwa ujumla katika harakati za kuondoa umasikini miongoni mwa Watanzania na kukuza pato la taifa.
Wajumbe wakifuatilia mada mbali mbali kwenye mkutano wa Sera ya Afya ya Udongo katika Hoteli ya LandMark Jijini Dar es Salaam

Mhe Stephen Wasira na Balozi wa Marekani


Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Akutana na Balozi wa Marekani
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mhe. Stephen Masatu Wasira amefanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe Mark Childress.
Mhe Wasira katika mazungumzo yake na Balozi Childdress alibainisha changamoto zinazokabili kilimo nchini kuwa ni pamoja na zana duni zinazotumiwa na wakulima wadogo katika kilimo kuwa ni jembe la mkono.
Alisema kwa kutumia jembe la mkono itakuwa ni ngumu kuondoa umaskini kwa wakulima wadogo katika maeneo ya vijijini.
Aliongeza kuwa jembe la mkono hutumiwa wakulima wengi wa vijijini katika uzalishaji wa mazao katika Taifa letu.
’’ Wakulima wadogo ndio tegemeo kubwa katika uzalishaji wa mazao ya kilimo hapa nchini na karibu asilimia 90 ya chakula hapa nchini inazalishwa na wakulima wadogo” alifahamisha Mhe Wasira katika mazungumzo yake.
Soko nalo ni tatizo lingine linalokabili mazao ya wakulima wetu wadogo waishio vijijini, alitoa mfano wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika mikoa ya Mbeya na Iringa ambako kuna mazao mengi na hasa mahindi ambayo yamekosa soko.
Pia ameiomba serikali ya Marekani kusaidia kuwekeza zaidi katika viwanda vya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wetu ili waweze kufaidika na juhudi zao na mwishowe waondokane na umasikini
Uwekezaji katika viwanda vya kilimo utasaidia kuepukana na tabia ya kusafirisha malighafi na hivyo kutaongeza thamani ya mazao ya wakulima wetu, aliongeza Mhe Wasira.
Aidha, kitu kingine kilichosisitizwa na Mhe Wasira ni mkakati wa serikali kuwashirikisha vijana katika kilimo ili kuondokana na tabia ya sasa kwa vijana kukimbilia mjini na hasa Jijini Dar es Salaam kutafuta kile wanachokiita na kuamini kuwa maisha bora hupatikana mjini.
“ Kilimo cha Bustani ni muhimu kwani kinaweza kuwasaidia vijana kupata kipato cha haraka kwa kuwa mazao ya aina ya bustani huchukua muda mfupi kupata mafao yake, “ aliongeza Mhe Wasira.
Mhe. Wasira pia alisema serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inaboresha kilimo cha umwagiliaji na akaiomba serikali ya Marekani kusaidia katika hili kwani itaongeza uzalishaji kwa wakulima wadogo kwa kuwa watazalisha mara mbili kwa msimu mmoja wa kilimo.
Wakulima wanasafirisha mazao ghafi nje ya nchi kama korosho bila kuongezwa thamani yake na hivi kuwakosesha kupata faida kubwa katika mazao yao.
Naye Mhe Childress aliahidi kuwa serikali ya Marekani itafanyakazi na serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa inasaidia kilimo hapa nchini.

Sunday, March 1, 2015

Mbegu Mpya za Kilimo Zaidhinishwa

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Dkt.Yamungu Kayandabila (wa kwanza kushoto)  akiongea na vyombo vya habari wakati wa kuidhinisha aina mpya 65 za mbegu za kilimo katika mkutano uliofanyika hivi  karibuni katika  ukumbi wa New Safari  hotel ya mjini Arusha.


Naibu Natibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Chukula na Ushirika Dkt.Yamungu Kayandabila (wa kwanza kushoto) akisisitiza  jambo


Kamati ya Taifa ya Mbegu (National Seed Committee) imeidhinisha matumizi ya aina 65 za mbegu mpya za mazao mbali mbali ya kilimo. Mazao hayo ni mahindi, mtama, ngano, muhogo, miwa, pamba, mbaazi, kunde, ufuta, korosho na tumbaku.  Hatua hiyo ya Kamati inalenga kuongeza tija na kipato kwa mkulima. 
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa New safari Hoteli iliyopo Arusha Mjini, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Dkt Yamungu Kayandabila amesema kuwa kuidhinishwa kwa aina hizo za mbegu kunafuatia mapendekezo yaliyofanywa na Kamati ya Taifa ya Kupitisha Aina Mpya za Mbegu za Mazao (The National Variety Release Committee)
 Aidha aina hizo mpya za mbegu zimepitishwa baada ya kufanyiwa utafiti na kugundulika kuwa zina sifa mbalimbali kama vile kutoa mavuno mengi, kustahimili ukame, ukinzani dhidi ya magonjwa, kukomaa mapema na kupendwa na wakulima.
Miongoni mwa aina hizo mpya za mbegu, kuna aina kumi na sita (16) za mahindi, mtama (2), ngano (3), muhogo (4), miwa (5), pamba (1), mbaazi (4), kunde (2), ufuta (1), korosho (24) na tumbaku (3). Mbegu hizo zimefanyiwa utafiti wa kina na vituo vya utafiti vya Umma na Sekta binafsi hapa nchini kama.