Tuesday, April 21, 2015

WIZARA YAENDESHA MAFUNZO YA ZANA MBEYA

Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika inaendesha mafunzo ya matumizi bora ya Zana za kuvuna na kupura mpunga yanayofanyika Jijini Mbeya katika ukumbi wa kituo cha mikutano cha Mkapa.
Mafunzo haya ya wiki moja yatajikita zaidi kuwapa mafunzo washiriki juu ya matumizi sahihi ya zana hizo,lengo likiwa ni kuwapatia utalaamu washiriki wote juu ya uendeshaji na usimamizi wa mashine hizo.
Akifungua mafunzo haya Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Zana za Kilimo anayeshughulikia Usindikaji na Nishati Mbadala toka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Mhandisi Rajabu Mtunze amewataka washiriki wote kushiriki kikamilifu katika mafunzo ili wakaongoze vizuri walizopewa katika maeneo waliyotoka kwa manufaa ya wakulima.
“Tumeletwa hapa kuchukua mafunzo ili tukawe viongozi wazuri wa mashine kwenye maeneo yetu kwa nia ya kuwasaidia walengwa wetu ambao ni wakulima wetu” alisema Mhandisi Mtunze.
Aidha, Mhandisi Mtunze aliwashukuru pia washiriki wote waliokubali kufika katika mafunzo haya pamoja majukumu makubwa mengine yanayowakabili katika shughuli zao.
“Nafarijika sana kuwa nanyi hapa kwa kukubali kwenu kuwa nasi katika mafunzo muhimu kwa taifa letu ili kuweza kuinua kilimo chetu” alisisitiza Mhandisi Mtunze.
Mafunzo yanalenga washiriki wote wanaotoka kwenye skimu zilizopatiwa zana bora za kuvuna na kupura mpunga, jumla mashine za kuvuna na kupura mpunga (combine Harvester ) zipatazo 64, mashine za kupura pekee (Paddy Threshers) jumla yake ni 36 na mashine za kukata mpunga (Reaper) zikiwa ni 16.
Wizara kupitia Idara ya Zana za Kilimo kwa kushirikiana na Tume ya Umwagiliaji ilifanya jitihada za ziada kuhakikisha kuwa zana hizo zinapatikana, alifahamisha Mhandisi Mtunze.
Jumla ya mada 17 zitawasilishwa katika mafunzo haya, ikiwa ni pamoja na Umuhimu wa Kalenda za kilimo za maeneo ya mazao husika, matunzo na uendeshaji wa miundo mbinu ya umwagiliaji matumizi na matunzo ya zana na usimamizi wa mashine.
Mada nyingine ni utunzaji wa kumbukumbu, huduma baada ya mauzo , uvunaji na upuraji wa mpunga.
Pamoja na mada hizo mafunzo haya pia yatatoa nafasi kwa washiriki kubadilishana uzoefu katika shughuli za kilimo na hasa kuhusu matumizi ya zana.
Miongoni mwa washiriki hao ni Maafisa wa fani mbali mbali toka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Ofisi za Makatibu Tawala wa mikoa ya Washiriki, Maafisa Zana toka wilaya za washiriki na washirika toka kampuni zilizouza mashine zikiwemo SAVOY (T) LTD na Farm Equip (T) LTD .
Washiriki wengine ni pamoja na Maafisa Ugani na Maafisa Umwagiliaji wa Skimu mbali mbali zilizoshiriki .
Mafunzo yanawajumuisha jumla ya washiriki wapatao 101 toka mikoa ya Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Morogoro, Arusha, Ruvuma, Manyara, Pwani na Tanga.
Mafunzo haya yameratibiwa na Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika na kufadhiliwa na Mradi wa Sera na Maendeleo ya Rasilimali Watu ya Japan (PHRD) na kusimamiwa na Benki ya Dunia.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Zana Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Mhandisi Rajabu Katunze akifungua mafunzo ya zana za kilimo Jijini Mbeya

Thursday, April 9, 2015

UTEUZI WA MWENYEKITI NA WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI YA BODI YA KOROSHO TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa mamlaka aliyopewa chini  ya kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Korosho ya mwaka 2009  (Sura ya 203 ya Sheria za Tanzania), amemteua Mhe. Anna  Margareth Abdallah (MB) kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Korosho.

Aidha, Mhe. Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika amewateua wafuatao kuwa wajumbe wa Bodi hiyo ya Wakurugenzi kwa mujibu wa kifungu  cha 4(1) cha Sheria ya Korosho ya mwaka 2009  (Sura ya 203 ya Sheria za Tanzania):-

1. Joseph Florian Haule - Mwakilishi wa wabanguaji korosho nchini.

2. Bw. Thomas Chatanda - Mwakilishi wa wakulima wa korosho

3. Mhe. Mudhihir M. Mudhihir- mtaalamu mwenye uzoefu kwenye sekta ya korosho

4. Bw. Rashid M. Serungwi- Mwakilishi wa wakulima wa korosho

5. Dkt Louis  Kagusa - Mtafiti wa Korosho, anayewakilishwa watafiti wa korosho

6. Bw. Mwinyikondo Lila - Mtaalamu mwenye uzoefu kwenye sekta ya korosho

7. Bw. Edgar Maokola Majogo - Mwakilishi wa wabanguaji wa korosho

8. Bibi Belinda P. Kyesi - Mwakilishi wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika.


Uteuzi huu  ni wa miaka mitatu na unaanza rasmi  tarehe 23 Februari, 2015.

Wednesday, April 8, 2015

Watendaji Wakuu RUBADA Wasimamishwa Kazi kwa Tuhuma za Ubadhirifu


Mheshimiwa Wasira (kulia) akiongea na Waandishi wa habari (hawapo pichani). Katibu Mkuu Bibi Sophia Kaduma (katikati), na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Dkt. Yamungu Kayandabila. 
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa Stephen M. Wasira (Mb), ametangaza kuwasimamisha kazi watendaji watatu wa Mamlaka ya Kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (Yaani Rufiji River Basin Development Authority – RUBADA) kutokana na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka.
Akitoa agizo hilo mbele ya Waandishi wa Habari leo, Watendaji hao ni Bwana Aloyce L. Masanja – Kaimu Mkurugenzi Mkuu; Bibi Tabu Ndatulu – Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji; na   Bwana Filozi John Mayayi – Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.
Taarifa ya Mheshimiwa Wasira imeanisha kuwa kati ya shilingi 2.748 billion zilizokuwa zimekusanywa kwa ajili uwekezaji, ni shlingi 714.606 milioni tu ndizo zimetumika kihalali wakati kiasi kilichobaki kimetumika bila kuzingatia sheria na kanununi za fedha za umma.
Aidha, Bodi ya RUBADA imetakiwa kuteua Maafisa watakaokaimu nafasi za viongozi hao wakati mchakato wa kuwapata viongozi wa kudumu ukiendelea.

Vilevile, mamlaka zingine ikiwa ni pamoja na vyombo vya dola kama vile TAKUKURU na Polisi wanaendelea na taratibu za kuwachukulia hatua viongozi hao kwa mujibu wa sheria za nchi.