Monday, November 30, 2015

Naibu Katibu Mkuu Afungua Mkutano wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kuhitimisha Awamu ya Kwanza ya Mradi wa EAAPP.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Eng. Raphael Daluti leo amefungua mkutano wa 10 wa Kanda ya Afika Mashariki wa kuhitimisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa EAAPP.
Katika hotuba yake, Eng. Daluti alisema kuna mambo mengi ya kujivunia kutokana na matokeo ya utekelezaji wa mradi katika kipindi cha miaka mitano huku akitaja maeneo ambayo yamekuwa na ongezeko la uzalishaji wa mazao ya mpunga, mihogo, ngano na uzalishaji wa maziwa na mazao yake.
Eng. Daluti aliongeza kuwa eneo lililoonyesha mafanikio wakati wa utekelezaji wa mradi huo, ni ongezeko la wataalam katika eneo la utafiti. Mradi umefanikisha ufadhiri katika tafiti kadhaa na kuongeza kuwa zaidi ya Watafiti 110 kwenye ngazi mbalimbali walishiriki huku zaidi ya Watafiti 6 kwenya ngazi ya shahada ya  uzamivu (PhD) na Watafiti 16 kwenye shahada ya Uzamili (Masters) walifadhiriwa na kusoma kwenye vyuo mbalimbali.
 Mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa mshikamano wa kikanda katika maendeleo ya sekta ya kilimo kwani kumekuwa na juhudu za pamoja za kukabiliana na changamoto zinazomkabili mkulima wa Afrika. Alipongeza juhudi hizi kuwa ni namna nzuri ya kujiandaa kukabiliana na ongezeko la idadi ya watu, ambapo, inafikiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 duinia itakuwa na watu zaidi ya bilioni 9.1 ambao watahitaji chakula ambacho kwa sehemu kubwa, kinazalishwa Afrika. 
“Wote, tunafahamu namna ambavyo malengo ya mradi wa EAAPP yalivyotekelezwa kwa vitendo na matokeo, yameonekana kwenye, kuongeza tija na uzalishaji lakini pia kuongezeka kwa ushirikiano katika kuboresha teknolojia na mafunzo ya wataalam. Hayo yamechangiwa na jinsi ambavyo nchi zetu, zilivyoshirikiana katika upeanaji wa taarifa za kimkakati katika mazao manne ya kipaumbele ambayo, ni mpunga, ngano, mihongo na uzalishaji wa maziwa.” Alisema Eng. Daluti.
Mradi wa EAAPP ulikuwa ukitekelezwa na taasisi za kilimo na mifugo katika nchi nne ambazo ni Ethiopia, Kenya, Tanzania na Uganda kwa mazao ya ngano, maziwa, mpunga na muhogo mtawaliwa.
Mradi huo ulikuwa na malengo za kuzalisha teknolojia kupitia utafiti wa mazao ngano, maziwa, mpunga na muhogo, pia kuzisambaza kwa walengwa ambao ni wakulima na wafugaji. Tangu mradi wa EAAP ulipoanzishwa miaka minne iliyopita zaidi ya teknolojia 400 zimepatikana na kusambazwa kwa wakulima na wafugaji.
Akizungumza katika mkutano huo, mtalaam kutoka Kenya Dr. David Wekesa Nyongesa alisema mradi huo umewawezesha kuzalisha mbegu za mifugo ambazo zimeanza kuwa na mahitaji makubwa ndani na nje ya Kenya.
Mradi wa EAAPP ulianza kutekelezwa mwaka 2010.  Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Eng. Raphael Daluti wakati wa  mkutano wa 10 wa Kanda ya Afika Mashariki wa kuhitimisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa EAAPP. uliofanyika katika ukumbi wa wanja wa taifa DSM.


Wednesday, November 25, 2015
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UGONJWA WA
MNYAUKO FUSARI WA PAMBA NA MBEGU ZISIZOOTA

Serikali imewataka wachambuaji na wasambazaji  wa mbegu za pamba kuacha kuwasambazia wakulima mbegu zilizozalishwa katika maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa wa mnyauko fusari (Fusarium Wilt Disease).  Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi, Bodi ya Pamba Tanzania, Bwana James Shimbe.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bwana Shimbe amesema, ugonjwa wa mnyauko fusari unaweza kudhibitiwa ikiwa wakulima wa pamba watatumia mbegu bora kutoka kwa wasambazaji wanaotambulika na Bodi ya Pamba Tanzania.

Akizungumzia tatizo la kuenea kwa ugonjwa huo Bwana Shimbe amesema kwa kiasi fulani limetokana na baadhi ya wachambuaji wasio waaminifu kuendelea kusambaza mbegu za pamba za kupanda ambazo zinaweza kuwa zimetoka katika maeneo yaliyobainika kuwa na  ugonjwa wa mnyauko fusari.

“Tulishatoa maelekezo kwa kuwataka wasambazaji wa mbegu za pamba za kupanda kutosambaza mbegu zilizozalishwa katika maeneo yenye ugonjwa.”

Hivyo tunaendelea kusisitiza kuwa wakulima wawe makini wanapo nunua mbegu kutoka kwa wasambazaji wasiotambulika na watoe taarifa haraka kwa Bodi wanapoona mbegu hizo hazioti ili hatua za haraka zichukuliwe za kupeleka mbegu zingine mbadala ili kuendana na msimu wa kilimo.

Aidha, Bwana Shimbe amewataka wachambuaji wa pamba ambao ndio wasambazaji wa mbegu kuacha mara moja kuwasambazia wakulima mbegu ambazo zimetoka kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa na badala yake mbegu za pamba hizo zisindikwe kuzalisha mafuta ya kula kama walivyokuwa wameelekezwa na Bodi hapo awali.

“ Bodi ilishatoa maelekezo kwa wachambuaji wote wa pamba kote nchini,  kutenga mbegu za pamba za kupanda  msimu huu wa kilimo kutoka maeneo yaliyo salama kwa kuziwekea lebo ili  kuzitofautisha na zile zinazotoka kwenye maeneo yaliyobainika  kuwa na ugonjwa, ambapo  zile zinazotoka katika maeneo yenye ugonjwa zisitumike kama mbegu za kupanda, bali zisindikwe kupata mafuta ya kula kama sehemu ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa, na zile mbegu ambazo zimetoka kwenye maeneo yasiyo na ugonjwa zisambazwe kwa wakulima kwa ajili ya kupanda kwenye mashamba yao baada ya kufanyiwa majaribio ya uotaji (seed germination test) na taasisi inayohusika na udhibiti wa ubora wa mbegu (TOSCI)”

 Aidha, mbegu zinazofaa kutumika kwa sasa ni UKM08 iliyofanyiwa utafiti na Kituo chetu cha Utafiti cha Ukiriguru, ambayo ubora wake umethibitishwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) na inauwezo wa kuhimili magonjwa pamoja na uzalishaji wenye tija zaidi. Mbegu hiyo itakuwa inaiondoa kwenye uzalishaji ile ya zamani  ya UK 91 ambayo imepungua ubora wake. Katika msimu huu wa kilimo wa 2015/16 Mbegu ya UKM08 itaendelea kuzalishwa kwa wingi (seed multiplication) katika maeneo salama yasiyo na ugojwa wa mnyauko fusari katika mkoa wote wa Singida na wilaya ya Nzega na Igunga, mkoa wa Tabora.

Bwana Shimbe ametoa wito kwa wakulima na wadau wote wa pamba nchini kufuata kanuni za kilimo bora cha pamba ikiwa ni pamoja na kutumia mbegu bora za pamba.  Aidha, baadhi ya mawakala wa ununuzi wa pamba mbegu na wakulima wenye tabia ya kuchanganya pamba mbegu na maji, mchanga, chumvi na kemikali zingine kama vile “mafuta ya kenge” kwa madai ya kuongeza uzito kwenye pamba yao waachane na tabia hiyo potofu, kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuoza kwa kiini cha mbegu na kuharibu ubora wake na hivyo kusababisha mbegu kutokuota.  

Imetolewa:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika
Kilimo Complex
1 Mtaa wa Kilimo 15471
DAR ES SALAAM Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Bwana James N. Shimbe

Tuesday, November 24, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MADAI YA WAKULIMA WADOGO WA MIWA WA KILOMBERO KUKOSA SOKO
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MADAI YA WAKULIMA WADOGO WA MIWA WA KILOMBERO KUKOSA SOKO
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bibi Sophia Kaduma ameiagiza Bodi ya Sukari Tanzania, kushughulikia mara moja madai ya wakulima wadogo wa  miwa (outgrowers) katika Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kilichopo Mkoani Morogoro  yaliotokana na miwa yao kutonunuliwa na kiwanda.
Katika agizo hilo, Katibu Mkuu Bibi Sophia Kaduma ameiagiza Bodi ya Sukari Tanzania kukuta  na Uongozi wa Kiwanda  cha Sukari cha Kilombero na  ule wa wakulima wadogo wa miwa  ili kupata ufumbuzi wa kudumu kuhusu soko la miwa wanayozalisha.
Aidha, Katibu Mkuu ametoa muda wa siku saba kwa Bodi ya Sukari Tanzania iwe imetekeleza na kutoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo.
Agizo hilo limekuja kufuatia Serikali kupata taarifa kuwa Uongozi wa Kiwanda hicho umeshindwa kununua miwa ya wakulima hao licha ya makubaliano yao ya awali ya kuzalisha miwa na kukiuzia kiwanda kwa ajili ya kuzalisha sukari.  Wakulima wamedai kuwa miwa hiyo, inakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 16.
Bodi ya Sukari Tanzania imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Sukari Na. 26 ya mwaka 2001 kama ilivyorekebishwa mwaka 2009 na Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mazao Na. 20 ya mwaka 2009 (Crop Laws (Miscellenous Amendments) Act).
Bodi ya Sukari Tanzania inajukumu pamoja na mambo mengine, kusimamia na kuratibu  kilimo cha miwa  na biashara ya sukari nchini,  kusajili wakulima, wazalishaji wa sukari na wafanyabiashara wa sukari.
Aidha, Bodi ya Sukari ina dhamana ya kuhakikisha uwepo wa ushindani wa haki kwenye soko la miwa na biashara ya sukari nchini.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika
Kilimo Complex,
1 Mtaa wa Kilimo 15471
DAR ES SALAAM.


Monday, November 23, 2015

Upatikanaji wa Vibali vya Kusafirisha Mazao Nje ya Nchi

Mkuu wa  Kitengo  Cha Sheria , Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bwana George Mandepo Serikali leo imetoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa vibali vya kusafirisha mazao kwenda nje ya nchi ambapo imesisitiza kuwa vibali hivyo vinapatikana bila gharama  na hakuna urasimu wowote.
Akitoa ufafanuzi huo, Mwanasheria wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bwana George Mandepo alisema kuwa vibali vya kusafirisha mazao ya kilimo nje ya nchi, hutolewa bila gharama na kuongeza kuwa biashara hiyo inaweza kufanywa na mtu yeyote, kinachotakiwa ni mhusika kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Bwana Mandepo aliongeza kuwa, uuzaji wa mazao nje ya nchi, unasimamiwa na Sheria ya Usalama wa Chakula iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, inayojulikana kama Sheria ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Serial and Other Produce Act, 2009) inayompa mamlaka Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika kutoa kibali cha kuuza mazao nje ya nchi kwa mtu mwenye vigezo.
Sheria hiyo pia, inampa mamlaka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, kukasimu madaraka ya kutoa vibali kwa Makatibu Tawala wa Mikoa wakati wa dharura kama ilivyokuwa katika msimu wa kilimo wa 2013/2014 ambapo Taifa lilikuwa na ziada ya kutosha.
Bwana Mandepo aliongeza kuwa, katika Sheria hiyo inamtaka mfanyabiashara kuainisha aina ya mazao na  kiwango ambacho anataka kusafirisha, lengo ni kuhakikisha kuwa, Serikali inakuwa na takwimu kamili za mazao yanayosafirishwa nje ya nchi.
Baadhi ya masharti nafuu ambayo mfanyabiashara anatakiwa, kuyafuata ni pamoja na kuwasilisha taarifa zake binafsi kama Jina lake kamili au Jina la Kampuni, anuani ya makazi, au eneo analotoka na uthibitisho wa mazao anayotaka kusafirisha nje ya nchi.
Aidha, Bwana Mandepo aliongeza kuwa Mfanyabiashara wa mazao kwenda nje ya nchi atapaswa kuwa na Cheti cha ubora wa mazao husika anayosafirisha, kinachojulikana kama ‘phytosanitary certificate’ kwa mujibu wa  Sheria inayosimamia ubora wa mazao (The Plant Protection Act 1997). Sheria hiyo inataka mazao yanayosafirishwa nje au kuingizwa nchini, yawe na ubora unaokubalika Kimataifa.
Bwana Mandepo alimalizia kwa kutoa wito kuwa nafasi ipo wazi kwa kila Mtanzania kuchangamkia fursa ya kusafirisha mazao nje ya nchi kwa kuwasilisha  maombi ya kibali kwa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa ajili ya kupata kibali hicho na kwamba Mfanyabiashara anayewasilisha maombi yake, anapaswa kuambatanisha leseni yake ya biashara, cheti cha mlipakodi na awe na idhini ya maandishi kutoka Wilaya au Mkoa ambako mazao husika yanatoka.