Monday, December 21, 2015

TFRA YAMFUNGIA MFANYABIASHARA WA MBOLEAMamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imemfungia Wakala Isaya Tito anayeuza mbolea katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kwa kukiuka taratibu za kutunza na kuhifadhi mbolea.

Uamuzi huo ulichukuliwa na Maafisa wa TFRA baada ya kujiridhisha kuwa mmiliki wa duka hilo Bwana Tito asifanye biashara ya kuuza mbolea mpaka hapo atakapokamilisha taratibu za uendeshaji. 

Maafisa wa TFRA walibaini kuwa Bwana Tito amekiuka taratibu za Sheria ya Mbolea Na. 9 ya Mwaka 2009 ambayo inawataka Mawakala wanaouza mbolea kuzingatia masharti ya uhifadhi, utunzaji wa mbolea na kuwa na vibali halali vya kuendesha biashara, ikiwemo, cheti na leseni inayotolewa na Mamlaka hiyo kabla ya kuanza biashara ya mbolea. 

Akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali  Mkaguzi kutoka TFRA Bwana Allan Marick alisema tumemfungia kwa muda Bwana Tito  mpaka hapo atakapokamilisha taratibu za uuzaji wa mbolea kama ilivyoainishwa katika sheria na alifahamisha kuwa zoezi hili ni endelevu na linalenga kuwabaini mawakala wanaokiuka taratibu za uuzaji wa mbolea.

“Tumesikitishwa na uendeshaji wa duka la Bwana Tito kwa kuwa  hajazingatia uwekaji wa chaga ili mbolea ikae sehemu kavu na safi,  na pia anauza mbolea kwa kutumia mzani kwa rejareja ikiwa wazi, hivyo anawauzia wakulima mbolea ambayo haina ubora unaotakiwa”, aliongeza Bwana Marick. 

Awali kabla ya kuanza kwa zoezi la ukaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bwana Ally Mpeya aliwaomba Maafisa wa TFRA kufikisha ombi la kuweka mpango wa kuwafundisha wakulima jinsi ya kutambua mbolea zisizo na ubora kwa kutumia njia rahisi.

Bwana Mpeya alitoa mfano wa njia rahisi ya kufundisha wakulima kwa kutumia shamba darasa ilivyoleta mafanikio makubwa, na hivyo njia hiyo inaweza kutumika kuwafundisha wakulima kutambua mbolea iliyo na viwango bila kuhitaji usimamizi wa wataalam.  

Pia alisisitiza kuwa wakulima ndiyo watumiaji wakubwa wa pembejeo hizo, hivyo ni vema wakapewa kipaumbele katika kupatiwa mafunzo ya utambuzi wa mbolea bora.

“Ni vema Serikali ikiwekeza katika suala la elimu ya kutambua ubora wa mbolea hasa katika Mkoa wa Ruvuma ambapo matumizi ya mbolea yapo katika kiwango cha juu na kuwa wakulima wamehamasika katika matumizi yake katika kila msimu wa kilimo”, alisisitiza Bwana Mpeya.

 TFRA inaendesha zoezi maalum la ukaguzi ili kuona kama Mawakala na Wafanyabiashara wa mbolea katika Wilaya tatu za Mkoa wa Ruvuma na Wilaya mbili za Mkoa wa Iringa, wanafuata masharti na maelekezo ya namna ya uendeshaji wa biashara kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha taasisi hiyo.Wakaguzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA) Bwana Allan Marik (Mwenye shati ya maua) na Bwana Raymond Ngoka (Mwenye fulana ya kijivu) wakiwa katika ukaguzi wa mbolea katika sehemu za kuhifadhia katika maduka ya Mawakala katika Wilaya ya Namtumbo, Mkoani Ruvuma hivi karibuni

Wednesday, December 16, 2015

Tafuteni Majawabu ya Kero za Wananchi, Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Awaagiza WatumishiWaziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba amewataka wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, kutumia muda wao kuhangaikia kutafuta majawabu ya matatizo ya wananchi.  Aliyasema hayo leo wakati anaongea na Wakuu wa Idara za kilimo, mifugo na Uvuvi mara baada ya kuwasili Wizarani hapo kufuatia alipoteuliwa kuiongoza Wizara hiyo. 

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (Kushoto) wakati anawasili Wizarani. Katikati ni Katibu Mkuu, Bibi Sophia Kaduma, na Kulia ni Katibu Mkuu Dk. Yohana Budeba
Katika hotuba yake aliyoitoa baada ya kukabiribishwa na Wafanyakazi wa Wizara hiyo, Mheshimiwa Waziri alionya kuwa hizi siyo zama za kufanya kazi kwa mazoea ambapo kila mtumishi anatakiwa kusugua kichwa kutafuta majawabu ya kero za wakulima, wafugaji na wavuvi ambao ni zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania. 

Alisema, ipo dhana iliyojengeka miongoni mwa watumishi wa Serikali kuwa muda mwingi wanahangaika kutafuta “majibu” badala ya “majawabu” ya matatizo yanayo wakabili wananchi. Akitoa mfano wa maelezo yake alisema, pembejeo za kilimo zinapochelewa kufika kwa wakulima jibu linaweza kutolewa kuwa makampuni na wakala wa pembejeo hawakupeleka mbolea kwa wakati. Hilo linaweza kuwa ni jibu lakini siyo jawabu au suluhisho la tatizo kwa wakulima ambao wameshindwa kutumia mbolea ili kuendena na msimu wa kilimo. 

Katika hotuba yake, aliwataka watumishi katika kila eneo kupitia kero zinazowakabili wananchi na kuweka mikakati ya kuzishughulikia kero hizo katika muda mfupi.
“Nataka katika kipindi cha siku saba muainishe kero na mikakati yake ya kuzitatua ili tupate matokeo kwa haraka” alisema Mheshimiwa Nchemba. 

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (katikati), akisisitiza jambo wakati akizungumza na Wakuu wa Idara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani)
 Katika moja ya mambo yanayotakiwa kushughulikiwa kwa haraka ni pamoja na kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo inazidi kukua kila siku kwa kuzingatia kuwa ardhi haiongezeki, hali ya hewa inabadilika, wakati watu na mifugo inaongezeka.  Hivyo, lazima hili tatizo lipatiwe suluhisho kwa haraka na kama kuna kitu  kinakwamisha lazima kielezwe ili kiondolewe,  alisema Mheshimiwa Nchemba.  

Mheshimiwa Nchemba alihitimisha, kwa kuwataka watumishi kujituma na kufanyakazi kwa ushirikiano wa hali ya juu ili kupata mafanikio yanayohitajika. 

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Olenasha alisema, falsafa ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano, ni kufanya jambo kwa haraka, kwa wakati na kupata matokeo sahihi na tija kwa kuzingatia maslahi mapana kwa umma. 

Alisema, mathalani unapolima shamba, kazi inakuwa imefanyika, lakini kinachotegemewa ni kupata mavuno ambayo mwisho wa siku yatatumika kuwapatia chakula Watanzania.  Aliwataka wafanyakazi wa Wizara hiyo kuzingatia falsafa hiyo wanapotekeleza majukumu yao ili mwisho wa siku wananchi waone mabadiliko katika maisha yao.

Mara baada ya kuwasili Wizarani hapo, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri walipokea maelezo ya shughuli za kilimo yaliyotolewa na Katibu Mkuu Bibi Sophia Kaduma, ambapo maelezo ya shughuli za Mifugo na Uvuvi yalitolewa na Katibu Mkuu Dk. Yohana Budeba.  

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (wa tisa kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi

Monday, December 14, 2015

Naibu Waziri Kilimo Mifugo na Uvuvi Ameanza Kazi Rasmi

Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Ole Nasha leo amewasili ofisini Makao Makuu ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi tayari kuanza kazi rasmi, baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Nasha alilakiwa na Katibu Mkuu Bibi Sophia Kaduma, Naibu Katibu Wakuu Eng. Raphael Daluti na Bwana Zidikheri Mundeme.  Mheshimiwa Nasha, alisaini kitabu cha wageni katika Ofisi za Kilimo I na baadae alielekea katika ofisi yake iliyoko katika Majengo ya Mifugo na Uvuvi.

Akiwa katika Majengo ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Naibu Waziri Nasha alilakiwa na Katibu Mkuu Dkt. Yohana Budeba ambaye alimkaribisha rasmi na kumtambulisha kwa baadhi ya Watumishi.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, ameanza kazi kwa kutembelea Wilaya ya Mvomero, katika Mkoa wa Morogoro ambako imeripotiwa kutokea mauaji katika mapigano ya wakulima na wafugaji. 
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, alimteua Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Kilimo Mifugo na uvuvi na Mhe. William Tate Ole Nasha kuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo, na waliapishwa rasmi siku ya Jumamosi tarehe 12 Desemba 2015.

Akitoa ufafanuzi kuhusu ofisi za Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu Bibi Sophia Kaduma amesema kuwa Mheshiwa Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba atakuwa katika ofisi iliyoko katika  jengo la Kilimo I, wakati Naibu Waziri Mheshimiwa William Nasha atakuwa katika Jengo la Mvuvi House.

Aidha, Katibu Mkuu Bibi Sophia Kaduma aliongeza kuwa mapokezi rasmi ya Waziri na Naibu Waziri ambayo yataambatana na kuwakabidhi taarifa mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi yatafanyika mara baada ya Waziri kurudi kutoka safari ya Kikazi Mkoani Morogoro.

Thursday, December 10, 2015

Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza Baraza jipya la Mawaziri ambalo lina jumla ya Mawaziri 19 na Naibu Waziri 15.

Katika Baraza hilo, iliyokuwa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imeunganishwa na iliyokuwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na kuwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.

Katika Baraza hilo jipya la Serikali ya Awamu ya Tano lililotangazwa, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amekuwa Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, wakati Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, ni Mhe. William Tate Ole Nasha (Mb).


Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Wiliam Ole Nasha (Mb).
Watumishi wa Wizara wamepongeza na kuwakaribisha sana Viongozi hao Wakuu. Wakiongea kwa nyakati tofauti, Bwana Rashid Likiligo wa Kitengo cha Mifumo ya Kopyuta, amesema, “Uteuzi aliofanya Mhe. Rais Magufuli ni mzuri na umelenga kuleta ufanisi katika Wizara hasa kwa kuzingatia uchapakazi wa viongozi hao”.


Naye Caltas Kabyemela wa Idara ya Utafiti na Maendeleo alisema, “Nimependa uteuzi huo, hao wote waliochaguliwa ni wachapakazi na naamini Wizara yetu mpya itafanikiwa na kuwa na maendeleo yatakayoonekana kwa wananchi ambao ni zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania”.