Thursday, March 31, 2016

TANZANIA, NORWAY NA AGRA WAZINDUA MRADI MPYA
Taasisi ya Mapinduzi ya Kijana barani Afrika (AGRA) imezindua mradi mpya wa kuwasaidia wakulima wadogo ambao wapo kwenye mpango wa uendelezaji wa kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Mradi huo mpya ambao ni programu ya kukuza mapinduzi ya kijani katika kilimo (IGGSAS) unasaidiwa na Norway kupitia Wizari yake ya Mambo ya Nje.
Aidha,  programu hiyo imelenga kuwafikia na kukuza kipato cha wakulima wadogo 30000 katika mkao wa Mbeya ifikapo 2020.
Mradi huo utahusisha kuboresha angalau mazao sita katika mnyororo wake wa thamani huku wakiongeza matumizi ya pembejeo na elimu ya uchumi katika kilimo miongoni mwa wakulima wadogo.
Mradi huo pia umelenga kuwezesha upatikanaji wa masoko kwa mazao yanayolimwa na kuboresha sera ya mazingira na kuchagiza kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Mnamo Julai 2015, Serikali ya Norway kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nchi za Nje iliipatia AGRA krona za Norway milioni 9 ambazo ni  sawa na dola za marekani milioni 1.2.
Fedha hizo zililenga kuwezesha awamu ya kwanza ya programu ya AGGSAS katika ukanda huo wa SAGCOT huku kampuni ya YARA International ikiwa mshirika mkubwa.
Katika kipindi cha mwaka mmoja cha uhai wa programu hiyo, awamu ya kwanza AGRA iliweka mifumo husika kama raslimali watu na raslimali zingine katika hali ya kutumika kwa kuzingatia makubaliano ya ruzuku hiyo iliyohitaji ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma.
 AGRA  imefanya utafiti na kuweka mfumo wa kupima athari za mazingira na ikolojia.
Kutokana na mafanikia hayo,leo wadau wanashuhudia kuzinduliwa kwa awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo utakaochukua miaka minne kuanzia julai 1,2016  hadi juni 30,2020.
Akizungumza katika uzinduzi huo  Rais wa AGRA Dk. Agnes Kalibata alisema ushirikiano wa AGRA na Norway, unatoa nafasi ya taasisi ya AGRA Kuongeza utendaji wake nchini Tanzania.
Akizungumza zaidi katika hafla hiyo ambayo pia imetumika kuzindua mpango wa miaka mitano wa kazi wa AGRA,  alisema Tanzania inauwezo mkubwa wa ghala la nafaka.
“Kwa miaka tisa tumekuwa tukifanya kazi bila kuchoka nchini Tanzania na kushirikiana na sekta binafsi na umma katika kuakikisha kwamba wakulima wadogo wanatumika katika uwezo wao wote na kuwaondoa katika kilimo cha kujikimu na kuwa na kilimo cha kujiongezea kipato kutoka katika kazi yao ngumu,”  alisisitiza Dk Kilibata.
Miaka tisa iliyopita Tanzania ilipata ruzuku 95 kutoka kwa wafadhili mbalimbali waliopitisha fedha zao AGRA zinazofika takribani dola za Marekani milioni 49.
 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway  Tone Skogen alisema serikali ya Norway imeridhika kusaidia mpango wa kuwawezesha wakulima wadogo kupitia ushirikiano  wa sekta binafsi na umma, kuwezesha kukuza kilimo kwa kuangalia watu maskini na kuwawezesha kuwa na kilimo kinachozingatia mazingira na tabianchi na upatikanaji wa masoko.
Uzinduzi huo ulifanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dr Florence Turuka kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Mwigulu Nchemba na kushuhudiwa na  wawakilishi wa mkoa wa Mbeya , mshirika mkakati wa AGRA, YARA, wadau wa maendeleo katika kilimo,kituo cha SAGCOT,  taasisi ya kimataifa ya uhifadhi mazingira IUCN na wadau wengine.

Rais wa AGRA Dr. Agnes Kalibata akizungumza katika uzinduzi huo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dr. Florence Turuku akizundua mradi mpya wa kuwasaidia wakulima wadogo
baadhi ya wajumbe walioudhuria uzinduzi huoDr. Florence akitoa hotuba kwa wadau

MHE. NASHA ASISITIZA UBIA KATI YA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI ILI KUINUA KILIMO


Serikali imeahidi kushirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza kilimo hapa nchini ili kuinua maisha ya wakulima ili kuondoa umasikini na kuongeza pato la Taifa.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. William Ole Nasha katika hotuba yake wakati akizindua mpango wa TAP II ( Tanzania Agricultural Parternaship) katika ukumbi wa Tanzanite uliopo hoteli ya Blue Pearl Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Nasha katika hotuba yake aliweza kuainisha baadhi ya changamoto zinazokabili kilimo hapa nchini ikiwemo uwekezaji mdogo katika katika sekta ya kilimo, ambao unatokana pamoja na mambo mengine na sera na taratibu za kuwekeza katika sekta hii.
Ili kuweza kuvutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi, Mhe. Nasha alisema serikali itaondoa urasimu usio wa lazima sana na pia taratibu za viwango vya ushuru na kodi katika sekta ya kilimo itapitiwa upya.
Changamoto nyingine ni ufinyu wa bajeti ambapo Tanzania bado haijafikia makubaliano ya nchi za afrika ya mwaka 2003, zilipokutana Jijini Maputo huko Msumbiji kuwa bajeti ya sekta ya kilimo ifikie asilimia 10 kwa nchi za Afrika ifikapo mwaka 2013, kwani katika bajeti ya mwaka 2015/2016 hapa nchini sekta kilimo ilitengewa asilimia 4.5.
Serikali imedhamiria kuongeza bajeti ya kilimo kwa kuweka mikakati mbalimbali ili kuboresha kilimo chetu, alifahamisha Mhe. Nasha.
Suala lingine ni ardhi ya kilimo na ufugaji , ambapo kumetokea migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, katika hili serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti kukomesha hali hii ya migogoro isiyokwisha.
“Katika jitihda za kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji serikali itatumbua ardhi ya wakulima na wafugaji kwa kupima na kuiwekea alama za mipaka”, alisisitiza Mhe. Nasha.
Jitihada nyingine za kupambana na changamoto za kilimo, Serikali ya Awmu ya Tano itaelekeza rasilimali nyingi zaidi katika kilimo cha umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu na kutumia teknolojia zenye ufanisi kwani wakulima wengi wanategemea mvua katika shughuli zao za kila siku za kilimo.
Mhe. Nasha alifahamisha kuwa Tanzania ina hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini mpaka sasa eneo linalomwagiliwa ni hekta 461,326 tu, eneo ambalo ni dogo sana.
Zana za bora za kilimo ni muhimu sana katika kuinua kilimo ili kufanikisha wepesi wa utendaji wa kazi kwa wakulima, inakadiriwa kuwa asilimia 62 ya kilimo chetu ni cha jembe lamkono ili kubaliana na hali hii serikali inahamasisha sekta binafsi kuagiza zana hizi kwa wingi ili kuondokana na tatizo hili, alibainisha Mhe. Nasha.
Msingi wa mazao bora ni pembejeo na kwa kutambua hili serikali inatoa kipaumbele kwenye upatikanaji na matumizi sahihi ya mbegu kwa wakulima.
Pia katika kupambana na uhaba wa pembejeo kwa wakulima tayari Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kupitia kwa Wakala wa Uzalishaji wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuna hekta zipatazo 8713 zinazozalisha mbegu za aina mbalimbali, sehemu ya hotuba ya Mhe. Nasha ilibainisha.
Pia sekta ya Uvuvi imepewa kipaumbele na serikali ili iweze kuboreshwazaidi kwa kuzingatia mifumo ya ikolojia na mazingira ya wavuvi.
Naye Balozi wa Norway nchini Tanzania Bi. Hanne Maria Kaarstad alielezea umuhimu hali ya kilimo hapa nchini na mchango wake kwa Taifa la Tanzania.
Kilimo kinatoa mchango mkubwa kwa maisha ya watanzania hivyo Serikali ya Norway itaendelea kusaidia mpango huu wa TAP II ili kilimo kiweze kutoa mchango wake muhimu kwa Watanzania wanaotegemea kilimo.
Norway ni mdau mkubwa katika kusaidia mpango huu wa TAP II wenye lengo la kuboresha kilimo chetu kupitia wadau mbalimbali ili kuondoa umasikini.
Uzinduzi huu uliratibiwa na Baraza la Kilimo Tanzania

UZINDUZI WA TAP KATIKA PICHA JIJINI DAR ES SALAAM

Tuesday, March 22, 2016

SERIKALI YA DENMARK KUSAIDIA KUJENGA KIWANDA CHA MBOLEASerikali ya Denmark imedhamiria kupitia wawekezaji  kujenga kiwanda cha mbolea hapa nchini ili kuondoa tatizo la upumgufu wa mbolea kwa wakulima.
Hayo yalisemwa na Balozi wa Denmark nchini Tanzania Einar Jensen alipomtembelea  na kufanya mazunumzo  na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba ofisini kwake.
“ Tumedhamilia kujenga kiwanda cha mbolea ili kuondoa tatizo la mbolea kwa wakulima wa hapa nchini Tanzania ” alisisitiza Jensen katika mazungumzo hayo.
Aliongeza kuwa kiwanda hicho kitaweza kuzalisha tani milioni 1.3  kwa kiwango cha chini na uzalishaji unaweza kuongezeka zaidi ya hapo.
Ujenzi wa kiwanda hiki utawezesha wakulima wa Tanzania kupata mbolea kwa wakati na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali, alifahamisha Balozi Jensen.
Naye Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Nchemba alimfahamisha Balozi Jensen kuwa Tanzania ina upungufu mkubwa wa mbolea unaoathiri kilimo.
“ Wakulima wamekuwa wakipata mbolea isiyotosheleza mahitaji ya Taifa na pia imekuwa ikiwafikia kwa kuchelewa sana” alibainisha Mhe. Nchemba
Tanzania ina mahitaji ya mbolea ya UREA, ambayo ni ya kukuzia kwa kiwango cha tani elfu 6 ili kukidhi mahitaji ya wakulima wetu, Mhe. Nchemba alimweleza Balozi Jensen.
Pia ameitaka Serikali ya Denmark kusaidia kuharakisha ujenzi wa kiwanda hiki ili kuendana na  ilani  ya  uchaguzi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mhe. Nchemba alimhakikishia Balozi Jensen kuwa atafanya jitihada binafsi kuhakikisha kuwa kiwanda hiki kinajengwa haraka iwezekanavyo ili kuinua kilimo hapa nchni.
Kiwanda hicho kinatarajia kujengwa wilayani Kilwa katika mkoa wa Lindi na kwamba tayari eneo limepatikana kinachofanyika kwa sasa ni kukamilisha taratibu za kisheria.
Hii ni mara ya pili ndani ya mwezi mmoja kwa Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi  Mhe. Nchemba na Balozi Jensen kukutana katika harakati zao za kuona sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi vinasaidia kuondoa umasikini kwa Watanzania waliowengi.

Mh.Nchemba akiongoza mazungumzo kati ya Balozi wa Denmark Bw. Jensen ofisini kwake
Picha ya pamoja kati ya wajumbe wa Tanzania na Denmark mara baada ya kumaliza mazungumzoMh. Nchemba akifafanua jambo


Monday, March 21, 2016

Wadau Wakutana Kujadili Mabadiliko ya Sera ya Kodi kwenye Kilimo

wadau wakutana  kujadili mabadiliko ya sera ya kodi kwenye eneo la kilimo katika baadhi ya mazao kama kahawa,chai,uvuvi, kuku na vyakula vya mifugo pamoja.
Akiwasilisha taarifa yake katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Kilimo I Wizara ya Kilimo Mfugo na Uvuvi, Bwana Iddi Alifan Shekabughi amesema wamepitia mapendekezo ya wadau na kubaini uwepo wa haja ya kuiangalia  na kurekebisha sera ya kodi kwenye eneo la  katika mazao hayo.
"ni kawaida kwa kila mwaka  wadau kuleta mapendekezo yao kuhusu kodi inayohusu mazao ya Kilimo, au bidhaa nyingine kutoka nje ya nchi ambazo zimesamehewa kodi na kufanya marekebisho kwa jinsi itakavyo onekana".  alisema  Shekabughi
Aidha wadau hao wameitaka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kufanya mkuatano wa pamoja na Wizara ya Fedha  ili kutatua changamoto hizo za kodi katika mazao ya kilimo  na ufugaji.
"Wizara hii ikutane na Wizara ya Fedha  waangalie namna ya kuondoa kodi za mazao  kwakuwa zimekuwa zikimuumiza mkulima kwa kiasi kikubwa"
Kutokana na kodi kubwa inayotozwa katika zao la kahawa kumechangia kuanguka kwa soko  la zao hili hapa nchini na kuimarika kwa soko hilo katika nchi ya uganda ambapo kodi yao ni asilimia moja  wakati hapa nchini hutoza asilimia tano.


 wadau wakiwa kwenye mkutano wa kujadili mabadiliko ya sera ya kodi kwenye eneo la kilimo

Thursday, March 17, 2016

  Mdau ambaye akipata maelezo kutoka Mwonyeshaji wa Kampuni ya Mohamed Enterprises (METL) 

  Sehemu ya Washiriki wa mafunzo hayo ya Wakulima wakimsikiliza, Mhandisi Rajab Mtunze aliyefungua mafunzo hayo

 Meneja Mkuu wa Zana na Pembejeo, Kampuni ya Mohamed Enterprises, Indrabhuwan Singh akitoa maelezo kwa mkulima aliyekuja kwenye maonyesho hayo

  Meneja Mkuu wa Zana na Pembejeo, Kampuni ya Mohamed Enterprises, Indrabhuwan Singh akitoa maelezo kwa mkulima aliyekuja kwenye maonyesho hayo Fundi na mtoa mafunzo ya uendeshaji wa trekta, Ludovick Lyimo kutoka Kampuni ya Mohamed Enterprises ambao ndiyo wasambazaji wa matrekta ya TAFE

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Kampuni ya Mohamed Enterprises, (METL) yaendesha mafuzo kwa wakulima

Idara ya Zana za Kilimo iliyopo Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Kampuni ya Mohamed Enterprises, (METL) leo kwa pamoja wameendesha mafunzo ya matumizi ya zana za kilimo kwa kuonyesha moja kwa moja kwenye shamba la mfano lililopo karibu na Ofisi za Idara, majengo ya Kilimo III.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo la kuendesha mafunzo kwa vitendo ili kuonyesha namna zana za kilimo zinavyofanya kazi, Mhandisi Isaria Mwende alisema, lengo la Serikali ni kuonyesha kwa vitendo namna inavyomjali mkulima wa Tanzania lakini pia hii ni fursa ya kutambua ubora wa zana hizo.

Mhandisi Mwende aliongeza kuwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi haifanyi biashara ya zana za kilimo kama matrekta na majembe lakini inachofanya ni kuhakikisha kuwa zana hizo zinapoingizwa hapa nchini, zinakuwa za kiwango kinachokubalika, na kuwahakikishia watumiaji wake, kuwa wanapata huduma za matengenezo na vipuri.

“Napenda watu wafahamu kuwa, zoezi kama hili ni mihimu kwani hata sisi kama Taaisisi ya Umma, tunaitumia fursa hii, kujiridhisha kuhusu ubora wa zana hizo na pia tunawahudumia wananchi kwa kuwapa mafunzo ya matumizi ya zana hizi lakini pia kufahamu kuhusu mahitaji yao na kuwapa ushauri wa kiufundi na namna ya kuchangamkia fursa kwenye kilimo kwa kupitia zana bora.

Naye, Meneja Mkuu wa Zana na Pembejeo, Kampuni ya Mohamed Enterprises, Indrabhuwan Singh alisema mapinduzi ya kweli katika sekta ya kilimo yatafikiwa tu ikiwa wakulima wa Tanzania wataamua kuachana na jembe le mkono na kuanza kutumia zana bora kama matrekta na majembe katika kuongeza tija na uzalishaji.

Indrabhuwan Singh alisema Kampuni yao kimsingi inauza matrekta ya Kampuni ya TAFE ya nchini India ambayo imekuwa ikisifika duniani kote kwa kutengeneza matrekta imara na vipuri madhubuti na imekuwa ikizalisha na kuuza zaidi ya matrekta elfu 75 duniani kote.

Aliongeza kuwa mpaka sasa, Kampuni ya METL imeuza zaidi ya matrekta 500 nchini kote na kusisitiza kuwa inajiandaa kuingiza matrekta 1,000 katika msimu wa kwanza wa kilimo wa 2016/2017.

Naye Meneja Mwendeshaji wa Kampuni ya METL, Yahya Msagati alisema kilimo chenye tija na faida, kinaenda sambamba na matumizi ya zana bora kama matrekta na majembe yake, pamoja na elimu ya uendeshaji wa biashara na usimamizi mzuri.

“Napenda watu wafahamu kuwa si suala la kununua trekta na jembe lake tu bali ni pamoja na utunzani wa kumbukumbu na mambo mengine.”  Alisisitiza Msagati.

Msagati aliongeza kuwa ni vyema kama Wakulima wengi wanaonunua matrekta kwa lengo la kufanya kilimo kama ajira zao, kutumia zaidi ya asilimia 60 ya matumizi ya matrekta katika mashamba yao kuliko kuyatumia muda mwingi katika mashamba ya watu wengine ambapo, udogo wa mashamba ambayo wanawalimia wakulima wenzao, umbali kutoka shamba moja kwenda lingine na muda katika uendeshaji wa kilimo ni mambo ya muhimu kuzingatiwa na kinyume chake faida inaweza isionekane.

“Wito wangu kwa wakulima wanaokuja kununua matrekta ya TAFE, majembe na zana zingine, wawe na mashamba yao au ya kukodi, yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 50 na kuendelea kwa kufanya hivyo tija na faida katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, itaonekana.”Alimalizia Msagati.