Tuesday, April 12, 2016

MHE. NCHEMBA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA CZECH NA BALOZI WA NAMIBIAWaziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba  ameendelea na jitihada zake za kuinua Sekta za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kuondoa umasikini miongoni mwa Watanzania.
Ameendelea na jitihada hizo  kwa kukutana na Waziri  wa Kilimo wa Jamhuri ya Czech Bw. Marian Jurecka   na Balozi wa Namibia nchini Tanzania Bi. Theresia Samaria katika ukumbi wa Bodi ya Chai Jijini Dar es Salaam.
Awali katika mkutano wake na Bw. Jurecka, Mhe. Nchemba alimwomba  nchi yake kushirikiana na Tanzania katika kuinua sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hapa nchini.
Mhe. Chemba alishauri  kuwepo na utambuzi wa  fursa za ushirikiano  ili sekta hizi ziweze kuleta tija kwa Watanzania waliojikita katika kilimo, mifugo na uvuvi.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Wiliam Tate ole Nasha, ambaye alikuwemo katika ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo hayo  aliiomba Serikali ya Czech  kushirikiana na Tanzania katika teknolojia za kisasa za kilimo, mifugo na uvuvi ukiwemo usindikaji wa nyama, ujengaji na uboreshaji wa miundo mbinu ya umwagiliaji na utunzaji wa mazingira.
Maeneo mengine aliyosisitiza Mhe Nasha ni teknolojia ya juu katika matumizi ya Biogas ili kuweza kupunguza uharibifu wa mazingira.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dkt. Florence Turuka , anayeshughulikia Kilimo aliiomba Serikali ya  Czech kuona uwezekano wa kusaidia katika uanzishaji wa viwanda vya kilimo, uwezeshaji katika maghala na umwagiliaji.
Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi,  anayeshughulikia Uvuvi  Dr. Yohana Luhunga Budeba  pamoja na mambo mengine aliiomba Serikali ya Czech kusaidia katika teknolojia ya uzalishaji wa samaki na magonjwa ya samaki .
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi,  upande wa Mifugo Dr. Maria Henry Mashingo aliomba ushirikiano katika Utafiti na Mafunzo, kujiingiza katika  uendelezaji wa ranchi za mifugo ili kuinua sekta hii.
Aidha, Waziri  Bw. Jurecka aliomba kuyatambua  na kuyainisha maeneo ya kipaumbele ya kushirikiana kati ya nchi yake na Tanzania  ili yaweze kufanyiwa kazi kwa manufaa ya nchi hizi mbili.
Bw. Jurecka alisema nchi yake imeshirikiana  na nchi za kiafrika kama Ethiopia na Zambia katika nyanja mbalimbali.
Wakati huo huo,Mhe. Nchemba amekutana pia na kufanya mazungumzo na Balozi wa Namibia nchini Bi. Theresia Samaria, ambapo alielezea historia ya mahusiano ya kindugu kati ya Tanzania na Namibia.
Mhe. Nchemba alisema Tanzania ina mambo mengi  ya kujifunza kutoka Namibia na hasa katika Sekta ya Uvuvi, Mifugo na Kilimo.
Bi.Samaria aliahaidi kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na kufanya kazi na Tanzania pia alifahamisha kuwa upande wa mafunzo kuna wanafunzi toka Namibia wanasoma katika vyuo vya hapa nchini.
Mhe. Nchemba amekuwa akikutana mara kwa mara na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa ili kutafuta fursa za kuinua Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa manufaa ya Watanzania waliowengi.
Mhe. Chemba akiongoza mazungumzo alipokutana na Waziri Jurecka

Balozi Bi. Samaria akizungumza na ujumbe wa Tanzania

Friday, April 8, 2016

Fursa za Kilimo Mifugo na Uvuvi zawagusa Wachina               
Serikali ya china imeonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya kilimo mifugo na uvivi  ili kuifanya sekta hiyo kuchangia kikamilifu katika uchumi  na kuinua vipato vya watanzania
Mipango hiyo ilijadiliwa hivi karibuni baada ya timu iliyoongozwa na   Waziri wa Kilimo mifugo na uvuvi Mh.Mwigulu Lameki Nchemba na Naibu wake Mhe.William Tate ole Nasha  kukutana na  ujumbe wa watu 16 ulioongozwa na Balozi wa china hapa nchini  Mhe. Li Jianhua na Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamaa cha china Bwana H.Shangarai katika ukumbi wa Kilimo I wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.
Aidha Waziri alimueleza  Balozi kuwa Tanzania kuna fursa ya uwekezaji hususani katika uzalishaji wa mbolea,mbegu na teknolojia za umwagiliaji maji ambazo nchi ya china inaweza kuwekeza.
china iko mbele sana katika teknolojia za uvunaji wa maji,kilimo na ufugaji wa kisasa hivyo ni vizuri muwekeze tanzania ili wakulima wetu waweze kujifunza kutoka kwenu, alisema Mhe. Waziri
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe.William Tate ole Nasha alimweleza balozi kuwa Tanzania ina  idadi kubwa ya mifugo hivyo kuna fursa ya kipekee kwa nchi ya china kuanzisha viwanda vya usindikaji na uendelezezaji wa mifugo hapa nchini.
aidha balozi wa china hapa nchini  Mhe. Li Jianhua alisema nchi yake ipo tayari kuwekeza Tanzania kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wetu wa kibiashara na kidiplomasia hivyo kuwataka kuandaa taratibu za makubaliano ili utaratibu huo uweze kuanza mapema 
 Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuivi (kulia)Mh.Mwigulu Lameki Nchemba akisisitiza jambo wakati alipotembelewa na balozi wa China Mhe. Li Jianhua

Tuesday, April 5, 2016

SINARE ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI WA ACTMkutano Mkuu wa Baraza la kilimo Tanzania (ACT) umemchagua Dkt. Sinare Yusuf Sinare kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa  Baraza hilo.
Mkutano Mkuu uliweza kuwachagua wajumbe wa Bodi wapatao 12 ili kuendeshe shughuli za ACT kwa muda wa miaka mitatu ijayo.
Mbali ya Dkt. Sinare pia Profesa Andrew Temu alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na Dkt. Salum Shamte alichaguliwa kwa nafasi ya  Mweka Hazina.
wajumbe kamili waliochaguliwa katika Bodi ya Wakurugenzi ni   Dkt. Sinare Yusuf Sinare ambaye ni  Mwenyekiti,  Profesa Andrew Temu   Makamu Mwenyekiti na Mweka Hazina  Dkt. Salum Diwani.
Waliochaguliwa katika nafasi ya ujumbe  ni Bw. Salum Shamte, Mhe. Jitu Soni (Mb) na  Bi. Jacqueline Mkindi.
Wajumbe wengine ni  Dkt. Sophia Mlote, Bi. Patricia Charles, Bw. Abdul Mwilima, Bw. Abel Lyimo, Bw. Enock Ndondole na Bi. Janet Bitegeko ambaye ni  Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi.

Mkutano huo wa uchaguzi ulifanyika Machi 31, 2016  Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanachama wa ACT hapa nchini.

Shughuli zote za ACT zinasimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi kwa niaba ya wanachama wote  wa ACT.
Wakati huo huo, kikao cha Bodi cha 27 kilichofanyika tarehe 19 Machi 2016 kwenye ofisi ya ACT na wajumbe walijadili masuala kadhaa muhimu.

 Hoja kuu ilikuwa ni jinsi gani  chombo hiki kitaweza kujitegemea kifedha na Bodi ilipata nafasi ya kujadili bajeti ya mwaka 2016, hoja nyingine zilizojiri ni miradi ya kuingiza mapato,  maandalizi ya Warsha ya Wadau wa Sekta ya Kilimo na Mkutano Mkuu wa Mwaka.

Bodi ilionyesha wasiwasi juu ya  uwezo wa ACT wa kuwa na vyanzo vya mapato yanayotosha kuendesha shughuli zake bila kutegemea sana wafadhili.

 Miongoni mwa njia za kujikwamua zilizopendekezwa  ni kuanzisha miradi ya kibiashara ambayo Bodi iliidhinisha na Sekretariati iliagizwa kuharakisha mchakato wa kuanzisha miradi hiyo haraka iwezekanavyo.

PICHA ZA VIONGOZI WA BARAZA LA KILIMO TANZANIA (ACT)