Monday, October 31, 2016

KAMPUNI YA INDIA KUJENGA KIWANDA CHA MATREKTA TANZANIA

Kampuni ya utengenezaji wa Matrekta kutoka nchini India ya International Tractors Limited imeamua kuwekeza nchini kwa kujenga kiwanda cha kuunganisha matrekta na zana nyingine za kilimo.
Kaimu Mkurugenzi wa Zana za Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Rajabu Mtunze alitoa taarifa hiyo baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa kampuni hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu.
Kampuni hiyo kupitia kiwanda hicho itakuwa na uwezo wa kuunganisha matrekta makubwa kati ya 1500 – 2000 na trekta ndogo za mkono maarufu kama Power Tiller zipatazo 500 – 600 kwa mwaka, kulingana na mahitaji ya wakulima wetu nchini, alifahamisha Mhandisi Mtunze.
Aina ya mashine zitakazounganishwa katika kiwanda hicho ni aina ya Horse power 50, 75 na 90 ili kuweza kuweza kuhimili changamoto ya zana zinazohitajika kwa wakulima wa Tanzania.
“ Nimewashauri kiwanda hiki kijengwe mkoani Dodoma makao makuu ya nchi ili kiweze kutoa huduma kirahisi kwa nchi nzima “ aliongeza Mhandisi Mtunze.
Dhamira hii ya kujenga kiwanda hiki ni sehemu ya utekelezaji sera ya Serikali ya Awamu ya Tano inayooongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
Mazungumzo yalijumuisha viongozi wawili wa juu wa kampuni hii kutoka India akiwemo Rais wa Kampuni hiyo Rajiv Kumar na Meneja Mwandamizi Chhater Pal Yadav.
Kampuni hii ni maarufu hapa duniani na ina viwanda katika nchi 86, kati ya hizo Barani Afrika kuna nchi 26 .
Kahimu Mkurugenzi wa Idara ya Zana za Kilimo Mhandisi. Rajabu Mtunze  na Maafisa wa Idara hiyo wakiwa pamoja na viongozi wa kampuni ya kiwanda cha utengenezaji matrekta kutoka  India

DKT. TURUKA AZINDUA MKAKATI WA VIJANA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dkt. Florens Turuka amezindua Mkakati wa Taifa wa Vijana katika Kilimo hapa nchini, uliofanyika katika Hoteli ya Blue Pearl Jijini Dar es Salaam .
Kupitia mkakati huo Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa vijana wanahusishwa kikamilifu katika kupiga vita umasikini kupitia Sekta ya Kilimo, alifahamisha Dkt. Turuka.
Vijana ni sehemu kubwa ya jamii katika nchi yetu na hivyo kushirikishwa kwao kutasaidia sana kuleta maendeleo kwa kuwa kilimo kina nafasi kubwa.
Amesisitiza kuwa vijana wajione kuwa mpango huu uko kwa ajili yao ili kuweza kuwakwamua katika lindi la umasikini.
Aidha, amezitaka taasisi binafsi kushiriki kikamilifu katika mpango huu kwa vile wadau wengine nao ni muhimu katika kuwaendeleza vijana ambao ni tegemeo la Taifa letu katika kuleta maendeleo.
“Serikali itaweka mazingira mazuri katika kuwawezesha vijana wetu kupitia mafunzo mbalimbali ili kufanikisha ndoto za mkakati wetu maalum kwa vijana” aliongeza Dkt. Turuka.
Vijana wajione kuwa ni sehemu kubwa katika mkakati huu ili kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na changamoto zinazowakabili katika kilimo kama vile masoko, tabianchi na nyingine.
Vijana waliopata bahati ya kuhudhuria uzinduzi walitoa maoni yao kuhusiana na mwaliko huo, Julius Kidoti toka Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam alisema amefurahishwa na kualikwa katika uzinduzi huu kwa kuwa ametambua baadhi ya fursa katika kikundi chao kinachojighuliisha na kilimo na ufugaji wa samaki.
Naye Philemon Kiemi toka mkoani Singida ambaye kikundi chake kinajishughulisha na ufugaji wa nyuki amepongeza mkakati huo kuwa utatusaidia sisi vijana.
Uzinduzi huu ulihudhuriwa na vijana toka mikoa ya Mbeya, Njombe, Dar es Salaam, Singida, Dodoma na Iringa.

Wadau wengine walioshiriki ni vyombo vya Fedha vya NMB, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB).
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na mashirika mbalimali ya ndani na nje ikiwa ni pamoja na shirika la Kazi Duniani (ILO), Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), SAGCOT, Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO).
Taasisi nyingine zilizoalikwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu, ANSAF, Taasisi ya Utafiti katika Ukanda wa Joto (IITA), TAMISEMI na mwenyeji wa uzinduzi Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.
Mkakati huu maalumu kwa vjina ( Natonal Strategy for Youth Involvement in Agrigulture ) unategemewa kutekelezwa kuanzia mwaka 2016 hadi 2021.
Katibu Mkuu Dkt Frolens Turuka akizungumza na wadau wa mkutano
Picha ya pamoja na vijana walioshiriki katika uzinduzi huwo

Monday, October 17, 2016

WAZIRI WA KILIMO AFANYA UTEUZI MPYA BODI YA KOROSHO

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mh Dkt.Charles John Tizeba amefanya mabadiliko kwenye Menejimenti ya Bodi ya Korosho.
Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Tizeba  alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano   wa wizara ya kilimo.
 Amteuwa Bw. Hassan Mohamed Jarufu kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho nafasi iliyokuwa chini ya Bw. Mfaume Mohamed.
 Mabadiliko mengine ni nafasi ya  Kaimu Mkurugezi wa Masoko, ambapo amemteua  Bw. Ray Mtangi kuchukua nafasi ya  Bw. Juma Yusuf.
Pia amefanya mabadiliko katika  Bodi ya Wakurugenzi kwa kuwateuwa Wawakilishi wa Wakulima Bibi. Faith Mitambo na Bw. Mshamu Solemn Mahundila, kutoka kundi la Wabanguaji Wadogo Mhe. Edgar Maokola Majongo.
Wajumbe wengine walioteuliwa ni Mwakilishi wa Utafiti Prof. Peter Albert Massawe,  Bi. Belinda Kessy mjumbe kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi na Wawakilishi wenye uzoefu Prof. Marcellina Chijoriga na Prof. Wakuzu Magigim, alifahamisha Dkt. Tizeba.
Uteuzi huu ni kwa mujibu wa Kifungu Na. 4(i) cha sheria ya Korosho ya mwaka 2009,  kwa mamlaka aliyonayo Wazira mwenye dhamana ya Kilimo.
Ameongeza kuwa serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kufanya maboresho ya utendaji katika maeneo mbalimbali ili kuongeza ufanisi na tija   kwenye taasisi zake.

Wakati huo huo, Mh. Tizeba amemrejesha Bw. Marco Mtunga katika nafasi yake ya Mkurugenzi Mkuu wa Pamba hatua iliyochukuliwa baada ya kutokuwepo kwa uthibitisho wa hutuma zilizokuwa zikimkabili   Bw. Mtunga kuhusika na matumizi mabaya ya shilingi bilioni 2.4 zilizotakiwa kulipwa Wakulima kufuatia mdororo wa uchumi wa mwaka 2008.

Mh. Dkt. Charles John Tizeba akizungumza na waandishi wa habari