Thursday, November 24, 2016

VIWANDA VIDOGO VIDOGO NI CHACHU KWA ZAO LA CHAI KWA WAKULIMA

Wakulima wadogo wa zao la chai wametakiwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kutumia fursa zilizopo ili kupata soko la uhakika.

wakiongea katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa kilimo 1, katibu mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dkt. Florens Turuka amesema uanzishwaji wa viwanda vidogo utaongeza thamani ya zao la chai na kuongezeka kwa soko.

“zao la chai ni muhimu katika kuinua uchumi wa nchi na kutupatia fedha za kigeni,Tanzania ni nchi ya 13 katika uzalishaji wa chai duniani, kwa Afrika ni nchi ya nne na kwa Afrika mashariki ni nchi ya 3 Kenya ikiwa ya kwanza hivyo uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo kwa wakulima ni muhimu katika uendelezaji wa zao hili” alisema Dkt. Florens Turuka

Aidha Bwana Joseph Massimba kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo SUA akiwasilisha andiko lake alisema chai ni zao la nne kwa kuingizia Taifa kipato baada ya korosho,pamba na tumbaku.

Aliendelea kusema kuwa zao hili hutoa ajira laki mbili katika kaya elfu 30 mpaka elfu 50 ambapo asilimia 37 ya mazao ya chai huzalishwa na wakulima wadogo na asilimia 63 huzalishwa na wakulima wakubwa


Monday, November 21, 2016

MHE. TIZEBA AZINDUA BODI YA MAMLAKA YA UDHIBITI WA MBOLEA TANZANIABodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imezinduliwa rasmi na
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles John Tizeba katika ukumbi wa Kilimo I hivi karibuni lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa  wakulima wanapata mbolea kwa urahisi na kwa bei nafuu.

Mhe Dkt. Tizeba amewataka kufanya kazi kwa umakini wa hali ya juu ili kuweza kufika lengo kuu la kuanzishwa kwa mamlaka hii.
Amewataka wajumbe wa Bodi kuwa wawe wawajibikaji na wabunifu katika utendaji wa kazi zao.
Aidha Jambo kubwa ambalo alilowataka wajumbe hao kuanza nalo kulifanyia kazi ni bei ya mbolea hapa nchini ambayo ni kubwa na hivyo kupelekea wakulima wengi kushindwa kumudu kununua.
“ Suala la kushusha bei ya mbolea liwe suala la kwanza kulifanyia kazi kwa mstabali wa maendeleo ya kilimo chetu kwa wakulima wetu” alifafanunua Dkt. Tizeba.
Kushusha bei ya mbolea kutasaidia sana na kuchangia kupunguza gharama za uzalishaji wa mazao mbali mbali kwa wadau wetu, alifahamisha Mhe. Dkt. Tizeba
Aliwataka kutazama upya sheria iliyoanzisha mamlaka hii kuona kama kuna uwezekano wa kukukabiliana na bei za mbolea ambazo zinatengenezwa kijanja kijanja mitaani ili kumuumiza mkulima mdogo.
“ Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Mbolea Tanzania ina upungufu kidogo hivyo nawaomba muitazame upya ili tuweze kufanya marekebisho madogo katika sheria hii” aliongeza Dkt. Tizeba
 
Pia Dkt. Tizeba aliwatahadharisha wajumbe kuwa wanafanyakazi miongoni mwa watu matajiri na wanyonge sana, hivyo wajihadhari kuingia katika mtego wa vivutio vya rushwa.
“Wajumbe acheni tabia ya kutaka “kuonwa” na matajiri kwani mnaweza kupoteza uadilifu katika utekelezaji kazi zenu na kujikuta mnajiingiza katika kashfa za kukosa uaminifu” alisisitiza Dkt. Tizeba
Kutokana na hali hiyo alienda mbali zaidi kwa kuwapa pole Wajumbe wa Bodi kwa kuwa watafanyakazi katika mazingira magumu kwani wako midomoni mwa watu wenye fedha.
Alisisitiza kuwa maendeleo ya kilimo hapa nchini yako mikononi mwao kwa kiasi kikubwa kwani wao ndio chanzo cha maendeleo ya kilimo kwa wakulima wetu waliowengi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Mshindo Msolla amemhakikishia Mhe. Dkt. Tizeba kuwa watafanyakazi kwa uwezo wao wote ili kufikia lengo lao.
“ Hatuwezi kukuangusha hata kidogo tutafanya kazi kwa bidii na uzalendo wa hali ya juu kwa manufaa ya Taifa letu “ aliahidi Dkt. Msolla.
Wajumbe wa Bodi hiyo ni pamoja na Dkt. Mshindo Msolla ambaye atakuwa ni Mwenyekiti na anatoka Taasisi inayojishughulisha na Biahshara ya Mbolea ( AFAP), Dkt. Ernest Marwa kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Dkt. Matilda Kulumuna kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mlingano cha mkoani Tanga na Dkt. Mwijarubi Nyaruba ambaye anatokea Tume ya Mionzi Tanzania ( Tanzania Atomic Energy Commission).
Wajumbe wengine ni Bw. Farank Mushi ambaye anatokea Umoja wa Wauzaji wa Mbolea Tanzania ( TANADA), Bw. Arnold Kisinga mjumbe kutoka NEMC na kutoka Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) ni Bw. Nickonia Mwambene, Hawa Kihwele kutoka MVIWATA na kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi ni Bw. Canuth Komba na Bw. Sospeter Mtemi.
Bodi Mpya ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea TanzaniaBodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania (TFRA) imezinduliwa leo na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa DK. Charles Tizeba. Akizungumza na Wajumbe wa Bodi hiyo, Mheshimiwa Dk. Tizeba ameitaka kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia ubunifu na uwajibikaji ili kuhakikisha kuwa mbolea yenye bei nafuu na yenye ubora inawafikia wakulima hapa nchini. Aliongeza kuwa gharama kubwa ya uzalishaji wa mazao ya kilimo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na bei ya pembejeo hususan mbolea kuwa juu sana. Hali hiyo inachangia mazao yanayozalishwa nchini kuwa na bei ya juu ikilinganishwa na mazao yanayoingizwa kutoka nje ya nchi. 

Hivyo, Bodi hiyo inatakiwa kufanya kazi kwa weledi, huku ikizingatia sheria ya mbolea na kuaangalia vipengele vya sheria iliyopo vinavyoweza kubadilishwa ili kuendana na malengo ya kuhakikisha kilimo kinakuwa kuendana na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa DK.Tizeba aiwaagiza wafanyakazi na Wakaguzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea (TFRA) kote nchini wafanye kazi zao kwa umakini mkubwa kwa kuhakikisha sheria ya mbolea inatekelezwa. Alitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua stahiki kwa wafanyabiashara wanaokiuka sheria ya mbolea. Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea inajumuisha Mwenyekiti na wajumbe tisa wafuatao:-


  1.  Dk. Mshindo M. Msolla                 Mwenyekiti
  2.  DK. Ernest Marwa                          Mjumbe
  3.  DK. Matilda Kalumuna                  Mjumbe
  4.  DK. Mwijarubi M. Nyaruba          Mjumbe
  5.  Bw. Frank Moshi                           Mjumbe
  6. Bw. Arnold Kisiraga                      Mjumbe 
  7.  Bw. Nickonia Mwambene            Mjumbe
  8. Bw. Canuth Komba                      Mjumbe
  9. Bi.  Hawa Kihwele                       Mjumbe
  10. Bw. Sospeter  Mtemi                    Mjumbe

Uteuzi wa Bodi hiyo ni wa miaka mitatu na imeanza kazi leo kwa kufanya kikao chake cha kwanza.

Mhe. Dk. Charles Tizeba akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya TFRA


Wajumbe wa Bodi ya TFRA wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Dk. Tizeba baada ya kuizindua.


Tuesday, November 8, 2016

Kampuni ya Mbolea yaanza kusambaza Mbolea ya Ruzuku kwenda kwa Wakulima

Wakati msimu mpya wa kilimo ukiwa unatarajiwa kuanza, Kampuni ya Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Company – TFC) imeanza zoezi la kusambaza mbolea ya ruzuku kwenda katika mikoa inayotarajia kuanza msimu wa kilimo wa 2016/2017.

Akiongea na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania, Bwana Salum Mkumba amewataka wakulima kujiandaa kupokea mbolea ya ruzuku ambayo imeanza kusafirisha tangu jana tarehe 7/11/2016 kutoka kwenye maghala ya Kampuni hiyo yaliyopo Jijini Dar es Salaam kwenda Mikoa 20 ya Tanzania Bara.

Bwana Mkumba amesema kuwa kwa zoezi la kusambaza mbolea hiyo ya ruzuku, litahusisha kiasi cha tani 32,300 (Tani elfu thelasini na mbili na mia tatu) ambazo zinaigharimu Serikali fedha kiasi cha shilingi bilioni 12 ambapo mkulima atapaswa kununua mfuko wa mbolea ya kupandia au kukuzia wa kilo 50 kwa shilingi 30,000.

Bwana Mkumba aliongeza kuwa mbolea hiyo imeanza kupelekwa katika Mkoa wa Katavi na Mikoa minginge ya Nyanda za Juu Kusini, Mikoa hiyo matumizi ya mbolea yapo juu na kwamba zaoezi hilo litaendelea kwenda Mikoa mingine kwa kutumia usafiri wa Reli na Barabara mpaka kukamilisha zaidi ya tani 32,000 zilizokusudiwa.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Pembejeo, Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Shanil Nyoni amesema, lengo la Serikali ni kuiwezesha Mikoa 20 kupata mbolea hiyo na ndivyo itakavyokuwa na kwamba Mkoa wa Katavi na Rukwa inaanza kupata mbolea hiyo kwa sababu, msimu wa kilimo unaanza hivyo itawafikia kwa wakati.

Bwana Shanil ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuwasaidia wakulima wasio na uwezo wa kumudu kununua mbolea na kwa utaratibu unaanza kwa kuwatambua wakulima kuanzia katika  ngazi ya Kijiji wenye sifa ya ukaazi wa eneo hilo, mwenye eneo la kulimia mahindi kuanzia ekari moja, na awe mkulima aliyetayari kupokea utaalam wa matumizi ya pembejeo hizo, ikiwemo mbolea na mbegu bora na awe tayari kuchangia gharama kidogo na kuongeza kuwa kwa kuanzia mpango huu umelenga kuwafikia wakulima laki tatu.


Aidha Bwana Nyoni amewataka wakulima kuondoa hofu ya kuwa mbolea hizo zinadumaza mazao na badala yake zinaongeza tija na uzalishaji kwa kuwa zimefanyiwa utafiti kabla ya kuwafikia wakulima kulingana na udongo na aina ya mazao.  

Mkurungezi Msaidizi wa Pembejeo za Kilimo Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvvi Bwana Shanil Nyoni akizungumza na Waandishi wa Habari 
Meneja Mkuu wa Kampuni  ya Mbolea Tanzania Bwana Salum Mkumba akisema jambo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari
Baadhi ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Mbolea  Tanzania (TFC) wakipakia mifuko ya mbolea ya ruzuku tayari kwa kusafirishwa

Monday, November 7, 2016

Bwana Patrick Ngwediagi wa Tanzania achaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mbegu CAJ ya Shirika la Hakimiliki la Kimataifa la Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea(UPOV)


Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Mbegu za Mimea kutoka Tanzania hivi karibuni amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mbegu CAJ ya Shirika la Kimataifa la Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea Hakilimiki la Kimataifa (The International Union for the Protection of New varieties of Plants - UPOV))

Wanachama wa Shirika la Kimataifa la Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (UPOV) mwishoni mwa mwezi Oktoba walikutana Jijini Geneva, Uswisi ambapo pamoja na ajenda zingine, walilifanya uchaguzi wa viongozi wa Shirika hili akiwemo Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Utawala (Legal and Administrative Committee - CAJ). Hii ndiyo Kamati ya juu inayolishauri Baraza la UPOV kuhusu masuala yote ya kitaalamu na kisheria. Kwa kawaida pamoja na kazi ya kumsaidia Mwenyekiti wake, Makamu Mwenyekiti huandaliwa kuwa Mwenyekiti mara tu kipindi cha Mwenyekiti wa CAJ kinapoisha.

Katika uchaguzi huo, Mwakilishi wa Tanzania kwenye Baraza la UPOV, Bwana Patrick Ngwediagi, alichaguliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa CAJ.

Bwana Ngwediagi ni Msajili wa Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (Tanzania Bara) na anao utaalamu na zoefu mkubwa katika masuala ya hakimiliki za mbegu, mfumo wa hakimiliki wa shirika la UPOV na tasnia ya mbegu kwa ujumla na pia ni mkufunzi wa wakufunzi (trainer of trainers) katika masuala ya hakimiliki za wagunduzi wa mbegu mpya kwa mujibu wa Mkataba wa UPOV wa mwaka 1991.

Aidha, Bwana Ngwediagi alisimamia na kuratibu kwa weledi mkubwa mchakato mrefu wa kuiwezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwanachama wa UPOV. Mchakato huo ulihusisha kupitishwa kwa Azimio la Bunge kuhusu kuridhia Mkataba wa UPOV wa mwaka 1991 na kutungwa kwa sheria ya Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea kwa upande wa Tanzania Bara (2012) na Zanzibar (2014). Kuanzia tarehe 22 Novemba, 2015, Tanzania ni mwanachama wa 74 wa UPOV na kabla ya hapo ilikuwa Mwanachama Mwangalizi (Observer).

Bwana Ngwediagi pia ni mbobezi wa masuala ya mbegu katika ngazi ya Kikanda na Kimataifa. Kwa sasa yeye ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mbegu ya Afrika iitwayo, AfricaSeeds. Taasisi hiyo inaundwa na nchi wanachama (Inter-governmental organization) wa Umoja wa Afrika (AU). Africa Seeds ndiyo taasisi iliyopewa jukumu la kutekeleza na kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Africa Seed and Biotechnology Programme (ASBP) wa Umoja wa Afrika (AU).

Kuchaguliwa kwa Bwana Ngwediagi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CAJ, pamoja na kuongeza heshima ya Tanzania kimataifa, nafasi hiyo pia itaitangaza Tanzania na hivyo kuongeza uwekezaji katika ugunduzi wa mbegu mpya, uzalishaji wa mbegu na kilimo kwa ujumla.