Wednesday, December 21, 2016

MHE. TIZEBA ASIMAMISHA SHUGHULI ZA MFUKO WA KOROSHO

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles John Tizeba amesimamisha mara moja shughuli zote zinazofanywa na Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho.

Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mfuko kushindwa kutekeleza majukumu ya kuanzishwa kwake na pia kwenda kinyume na maagizo ya Serikali hasa ukizingatia kuwa wanatumia kodi ya Watanzania.

Wadau wa zao la korosho wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu sana juu ya huu mfuko lakini hayakuweza kufanyiwa kazi ipasavyo.

Baadhi ya tuhuma zilizoelekezwa kwenye mfuko na Mhe. Dkt. Tizeba ni pamoja na kushindwa kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake badala yake mfuko umebaki na kazi ya kupokea pesa na kujikita katika manunuzi ya pembejeo.

Mfuko umeshindwa kusimamia kwa kiwango kikubwa maelekezo mbalimbali ya Bodi ya Korosho na Wadau kama yalivyokuwayakitolewa katika nyakati mbalimbali.

Mfuko umejiingiza katika matendo ya kuhujumu wakulima wakorosho na hasa wakati wa ununuzi wa pembejeo.

Tuhuma nyingine kwa mujibu wa Dkt. Tizeba ni pamoja na Mfuko umeendeshwa vibaya kwa uzembe au kwa makusudi na hasa wakati wa ununuzi wa viatilifu kama salfa kwa bei kubwa.

“ Mfuko unaeendeshwa kama mali ya watu binafsi na haufuati taratibu wakati unatumia kodi ya serikali “ aliongeza Dkt. Tizeba.

“ Kuanzia sasa shughuli zote za Mfuko zitafanywa na Bodi ya Korosho mpaka hapo utaratibu mwingine utakapoandaliwa” alifahamisha Dkt. Tizeba .

Mhe. Dkt. Tizeba amezitaja baadhi ya tuhuma zidi ya mfuko huu kuwa ni pamoja na matumizi makubwa ya fedha katika mambo ambayo si msingi na yako nje ya majukumu ya mfuko.

Matumizi haya makubwa yamechangia wakulima kununua pembejeo ya zao la korosho kwa gharama kubwa na hivyo kupelekea baadhi yao kushindwa kuzalisha.

Aidha, mfuko umeshindwa kutekeleza agizo la Serikali ya kutoweka fedha kwenye miamala ya muda maalumu ( fixed Account)katika benki za biashara.

Pia Rais ameagiza kwa taasisi zote za serikali kuhamisha akaunti Benki kuu kutoka benki za biashara lakini Mfuko umegoma kutekeleza agizo halali la kiongozi wa nchi.

Vitendo hivi vinahujumu sana maendeleo ya zao la korosho na vinaweza kurudisha nyuma jitihada za serikali kuinua na kuendeleza tasnia ya korosho.

Pia mfuko hauruhusiwi kufanya muamala wowote wa kibenki mpaka hapo baadaye pale utaratibu mpya utakapofanywa.

Mhe. Dkt. Tizeba pia amwemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Mathew Mtigumwe kumwomba Mkaguzi Mkuu wa Serikali ( CAG) kufanya ukaguzi katika mfuko huu kuona kama matumizi sahihi ya fedha za mfuko yalifuatwa au kukiukwa.

Mhe. Dkt. Tizeba ameagiza shughuli zote za mfuko zitafanywa na Bodi ya Korosho wakati sheria iliyoanzisha mfuko inatazamwa.

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi  Mhe Dkt  Charles John Tizeba akizungumza na Waandishi wa Habari, kushoto ni Katibu Mkuu Mhandisi Mathew Mtigumwe

Wednesday, December 14, 2016

KASUGA: TANZANIA INACHAKULA CHA KUTOSHA

Tanzania ilizalisha ziada ya chakula cha kutosha kiasi cha tani 1,101,341 kwa mazao ya nafaka  na tani 1,912,174 kwa mazao yasiyo nafaka katika msimu wa 2015/2016 ambayo yanatumika katika msiku wa 2016/2017. 

Hayo yalithitishwa na Msemaji wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dr. Richard Kasuga wakati akizungumza na Waandishi wa Sahara Media Group katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo.

Akitoa ufafanunuzi alisema upande wa uzalishaji wa zao la mahindi kulikuwa na ziada ya tani 946,284 na mchele tani 1,252,146. 

Ufafanuzi umetolewa baada ya kuongezeka ghafla kwa bei ya unga wa mahindi katika mikoa mbalimbali hapa nchini.  

Aidha, Dr. kasuga amekanusha vikali kuwa suala la kupanda bei ya unga wa mahindi lisichukuliwe kuwa nchi ina uhaba wa chakula bali ni hali ya kawaida ambayo hujitokeza katika miezi ya Desemba, Januari na Februari kila mwaka kabla ya kuanza kuvunwa kwa mazao ya msimu unaofuata wa kilimo. 

Serikali inakabiliana na hali hii ambapo Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko inaendelea na kazi ya kusaga na kusambaza  unga wa mahindi ili kushusha bei.

Serikali imeanza usambazaji wa Chakula kwa baadhi ya maeneo ya Handeni, Tanga mijini na Chalinze  na maeneo mengine ili  bei iweze kushuka, alifahamisha Dr. Kasuga.

Amewahimiza Wafanyabiashara waichukulie hali hii kama fursa ya kutoa mahindi yaliyopo katika maghala yao kwani  muda si mrefu hali ya mahindi katika soko itarudia hali ya kawaida kutokana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuongeza kiwango cha unga wa mahindi unaoingia sokoni. 

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usalama wa Chakula Bi. Marystela Mtalo amewataka wananchi kutotegemea aina moja ya chakula kwa kuwa mazao kama mchele upo wa kutosha na bei yake haijapanda.

Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ina jumla ya tani 90,716 za chakula cha tahadhari ya njaa na ununuzi unaendelea.  Hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi na hali ya kupungua kwa mahindi sokoni kwa kuwa hali itatengemaa katika muda mfupi kutonana na juhudi zinazofanyika na Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula.


Moja kati ya ghala la chakula Temeke Dar es Salaam

Msemaji mkuu  wa  Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Dr. Richard  Kasuga (kushoto) na Bi. Marystela Mtalo wakizungumza na Waandishi wa Habari.

Tuesday, December 13, 2016

ENG. MTIGUMWE AOMBA USHIRIKIANO KWA WAFANYAKAZI

Katibu Mkuu Mpya wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia Kilimo Eng. Mathew Mtigumwe ameripoti wizarani na kuomba ushrikiano kwa watumishi wa wizara hiyo.

Akiongea katika kikao cha kwanza muda mfupi baada ya kuwasili wizarani hapo kuchukua nafasi yake kufuatia uteuzi uliofanywa hivi karibuni na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ameomba kupewa ushirikiano ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

“ Naomba sana ushirikiano wenu ili tuweze kufikia lengo la kuwatumikia wananchi hasa wakulima wetu” alisisitiza Eng. Mtigumwe.

Ameonyesha imani kubwa kwa manajementi aliyoikuta kwani imejaa watu wenye uwezo wa hali juu kitaaluma na kiutendaji katika sekta hii ya kilimo.


Pia amebainisha kuwa Sekta ya Kilimo ina changamoto nyingi lakini kwa kufanyakazi kwa ushirikiano na umakini tunaweza kupunguza changamoto hizo.


Eng. Mtigumwe aliweza kutoa shukrani kwa mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa wafanyakazi kwani wamejitokeza kwa wingi kumkaribisha wizarani.


Kabla ya uteuzi huu Eng. Mtigumwe alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, ambapo nafasi yake imechukuliwa na Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kutoka mkoa wa Njombe.


Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt. Florens Turuka ambaye kabla ya mabadiliko haya alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi amewashukuru sana wafanyakazi kwa kumpa ushirikiano wa hali ya juu katika kipindi chote wakati akihudumu katika wizara hiyo.


“ Nawaomba sana ushirikiano mlionipa mimi muendelee kumpa huyu katibu mkuu wetu mpya” aliongeza Dkt. Turuka.


Wizara ya KIlimo Mifugo na Uvuvi inao Makatibu Wakuu watatu, anayeshughulikia KIlimo, Katibu Mkuu wa sekta ya Mifugo na Katibu Mkuu sekta ya Uvuvi.
Dkt Florens Turuka (kushoto) akimkaribisha Katibu Mkuu mpya Eng.Mathew Mtigumwe (kulia)