Tuesday, January 31, 2017

MTIGUMWE AWAONDOA HOFU WATUMISHI KUHAMIA DODOMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Mathew John Mtigumwe amewaondoa hofu watumishi wa wizara yake kuhusu zoezi la serikali kuhamia Dodoma kuwa litafuata misingi na stahili za watumishi kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa Umma.

Mhandisi Mtigumwe ametoa kauli hiyo wakati wa kikao maalumu cha kuhusiana na uamuzi wa serikali kuhamia Makao Makuu ya Nchi mkoani Dodoma.

Alifahamisha kuwa Awamu ya Kwanza ya uhamisho utawahusisha watumishi 88 kutoka Idara Kuu ya Kilimo, ambapo katika mchakato huo watumishi 41 watahamia Dodoma kuanzia tarehe 14 – 15/2/2017 na wengine 47 waliobaki watahamia muda wowote kufikia mwezi Juni.

Kuhusu maandalizi ya ofisi amesema yanaendelea vizuri huko Dodoma na mambo yote yanakwenda kadri ilivyopangwa.


Uamuzi wa Watumishi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kuhamia Dodoma ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka Serikali yote kuhamia Dodoma ili kutekeleza uamuzi uliofikiwa tangia miaka ya 70 na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutambua na kutangaza kuwa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi.


Mkutano huo ulifanyika Makao Makuu ya Wizara Temeke Jijini Dar es Salaam.
HALMASHAURI 55 ZINA UHABA WA CHAKULA NCHINI

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles John Tizeba amesema jumla ya Halmashauri 55 hapa nchini zinakabiliwa na uhaba wa chakula.
Kauli hiyo ameitoa wakati akiwasilisha kauli ya serikali kuhusu ya hali ya chakula na mvua kwenye Bunge la 11, mkutano wa 6 kwenye kikao cha kwanza mjini Dodoma. 

Amezitaja badhi ya Halmashauri zinazokabiliwa na upungufu wa chakula kuwa zinapatikana katika mikoa ya kanda ya Ziwa, Kati na Kaskazini.

Pia katika kikao hicho ameitaja mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ya Songwe, Mbeya, Rukwa, Katavi, Iringa, Njombe na Ruvuma kuwa hali ya mvua inaridhisha na hali ya chakula ni nzuri kwani kuna chakula cha ziada katika mikoa hiyo.

Dkt. Tizeba amesema kuwa serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu sana hali ya chakula nchini.
Kumekuwa na ongezeko la bei katika zao la mahindi hapa nchini na hii imetokana na sababu mbali mbali, Dkt. Tizeba aliliambia Bunge.

Dkt. Tizeba alizitaja baadhi ya sababu zilizopandisha bei ya mahindi kuwa ni pamoja na hali isiyoridhisha ya mwenendo wa mvua ambayo imewafanya wafanyabiashara kutumia mwanya huo kupandisha bei ya mahindi sokoni.

Sababu nyingine ni kama vile uhitaji na bei nzuri ya mahindi katika nchi jirani zinazotuzunguka na hivyo kusababisha bei ya mahindi kupanda.

Mhe. Dkt. Tizeba alibainisha athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mwendo mbaya wa mvua kuwa ni matarajio ya uzalishaji wa mazao usfikiwe kutokana na matarajio yaliyokusudiwa.

Pia uzalishaji wa mbegu za mazao huenda ukaathirika na hivyo kupungua kutokana na hali ya mvua.
Ameliambia Bunge kuwa athari nyingine zinazotarajiwa kutokea kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa utapiamlo na migogoro ya wakulima na wafugaji kutokea kutokana na kukosekana kwa malisho na maji.

Wizara itakuwa na jukumu la kusambaza mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi na pia kuhamasisha wakulima kulima mazao ya aina ya mizizi yenye uwezo wa kustahilimi ukame.

Mhe. Dkt. Tizeba aliendelea kutaja mikakati mingine ya wizara yake kuwa ni Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ( NFRA) kuendelea kutunza chakula ili kuweza kutumika pale kitakapohitajika.
Sekta Binafsi zitashirikishwa katika usambazaji wa chakula kwenye maeneo yaliyo na uhaba na pia usindikaji wa mazao ili kuongeza thamani yake.

Wakuu wa Mikoa na Wilaya wametakiwa kuhamasisha wakulima katika maeneo yao kutumia mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi.
Jitihada nyingine ni kuwashauri wananchi kutunza na kutumia vizuri chakula katika ngazi ya kaya.
Dkt. Tizeba amewaasa wananchi kuacha utamaduni wa kuchagua aina fulani tu ya chakula kwa baadhi ya makabila yetu.
Jitihada nyingine ni Serikali kupeleka na kuuza chakula kwa bei nafuu kwa wananchi katika maeneo yanayokabiliwa na uhaba wa chakula.
Athari zinazotegemea kutokea kama Taifa kutokana na mwenendo wa mvua ni kupungua kwa mapato ya halmashauri mbalimbali kutokana na kodi na tozo mbalimbali za mazao.
Nchi yetu pia itakosa fedha za kigeni kutokana na mazao yanayouzwa nje ya nchi kuathirika, aliongeza Dkt. Tizeba.
Mhe. Dkt. Tizeba amelihakikishia Bunge kuwa hali ya chakula nchini inaridhisha na kuwa kuna baadhi ya maeneo yana chakula cha ziada.

CHANGAMOTO YA UPATIKANAJI WA MBOLEA KUTATULIWA

Changamoto za upatikanaji wa mbolea kwa bei stahiki zimeanza kutatuliwa baada  ya wataalam na wadau wa mbolea kukutana na kuandaa rasim ya kanuni  za usimamizi wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (The Fertilizer (Bulk Procurement) Regulation 2017)
Akiongea baada ya kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa kilimo I hivi karibuni  mwanasheria wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (Tanzania Fertilizers Regulatory Authority -TFRA) Bi Belinda Kyesi amesema kuwa lengo la kanuni hizo ni kuondoa changamoto za upatikanaji wa mbolea kwa bei stahiki,kuongeza uelewa kwa watumiaji wa mbolea  na kupamabana na changamoto za uhaba wa wataalamu wa utambuzi wa sayansi ya udongo kwa matumizi ya  aina za mbolea.

Aidha kutokana na changamoto ya bei za mbolea  Belinda amesema kuwa uwepo wa kanuni hizo zitawasaidia  wadau kupunguza gharama za uagizaji, kuwa na bei elekezi pamoja na kupunguza gharama za bima hivyo mbolea kupatikana kwa bei stahiki.

Hata hivyo  Kaim Mtendaji Mkuu  wa Mamlaka ya Mbolea Bwana  Lazaro Kitandu  amesema kwamba kanuni hizo zitasaidia upatikanaji wa mbolea ya kutosha  na yenye ubora ambayo itasababisha wakulima kuongeza uzalishaji  na kuinua kipato vyao
Aidha Bwana Kitandu alisisitiza kwamba uwepo wa kanuni hizo zitaongeza ufanisi katika kusimamia majukumu ya TFRA katika kudhibiti ubora wa mbolea kote nchini.Monday, January 23, 2017

WIZARA YAKABIDHIWA GARI

Taasisi ya Ushirikiano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) imeikabidhi Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi gari lenye thamani ya shilingi milioni 88 za kitanzania itakayotumika katika Idara ya Mipango na Sera.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizaya ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Bi. Nkuvililwa Simkanga ndiye aliyepokea gari hilo katika hafla iliyofanyika katika viunga vya wizara hiyo.
Gari hilo litatumika katika Mradi wa Micro Reform for African Agribusiness Project (MIRA) ambao ni mradi wa kufanya mageuzi ya kisera na kisheria yanayokwamisha utekelezaji wa sekta binafsi katika kilimo unaosimamiwa na Idara ya Mipango na Sera.
MIRA ni mradi utakaogharamiwa na AGRA na utekelezaji wake utaratibiwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.
“ AGRA ni wadau wetu wakubwa na wamekuwa pamoja na Wizara bega kwa bega katika kuinua kilimo chetu kwa nguvu zote” aliongeza Bi. Simkanga.
Bi. Simkanga aliishukuru sana AGRA kwa kuendelea kushirikiana na Wizara katika kundeleza kilimo hapa nchini.
Mradi huu unategemea kutekelezwa kwa muda wa miaka 5 kwa kiasi cha Dola za Marekani zipatazo milioni 50 na umeanza kutekelezwa tangia Juni 2015 na utafikia kikomo Juni 2019.
Mbali ya gari vifaa vingine vilivyokabidhiwa hapo awali kuwa ni Komputa Mpakato (Laptop) na flash na hii ni kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango Bw. Gungu Mibavu.
Naye mwakilishi wa AGRA Bw. Vianey Rweyendela amepongeza ushirikiano uliopo kati ya AGRA na Wizara katika harakati za kuinua kilimo na akasisitiza kuwa kupitia ushirikiano huu vitafanyika vitu ambavyo havijafanywa katika kuhakikisha kuwa kilimo kinasonga mbele.
“ Tumedhamilia kuhakikisha kuwa partnership yetu tunafanya vitu ambavyo havijafanywa katika Sekta ya Kilimo hapa nchini” alisisitiza Bw. Rweyendela.
Wawakilishi wengine katika hafla hiyo alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango toka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Gungu Mibavu na Liston Njoroge toka AGRA.

Tuesday, January 17, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HALI YA CHAKULAJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KILIMO MIFUGO NA UVUVI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HALI YA CHAKULA
1.0      UTANGULIZI
Hadi kufikia katikati ya  mwezi Januari, 2017 hali ya chakula na upatikanaji wa chakula hapa nchini inaonyesha kuwa bado ni ya kuridhisha na hasa upatikanaji wa vyakula kama mchele na maharage ikilinganishwa na zao la mahindi. Pamoja na hali hii bei za baadhi ya vyakula zimeanza kupanda kufuatia mazao kidogo kuingia sokoni kwa wakati huu kunakochangiwa na mwenendo usioridhisha wa unyeshaji wa mvua za vuli na kuchelewa kuanza kunyesha kwa mvua za msimu katika maeneo mengi ya nchi.
2.0     HALI YA MAZAO MASHAMBANI
Hali ya mazao mashambani kutoka mikoa mbalimbali katika kipindi cha mwezi Desemba, 2016, inaonyesha kutoridhisha katika baadhi ya maeneo kutokana na uhaba wa mvua na mtawanyiko usioridhisha. Hata hivyo maeneo mengi ya nchi yamekuwa yakiendelea na uandaaji wa mashamba, kupanda, kupalilia na usambazaji wa pembejeo za kilimo. Kutokana na uhaba wa mvua na kuwa na mtawanyiko usioridhisha, hali ya unyevunyevu katika udongo si ya kuridhisha kwa ustawishaji wa mazao ya kilimo yanayohitaji maji mengi.
Taarifa ya hali ya upatikanaji wa mvua kutoka mikoa inayopata mvua za vuli, zinaonyesha kuwa kwa ujumla mvua zimechelewa kuanza na zimenyesha katika kiwango cha wastani na chini ya wastani zikiwa na mtawanyiko usioridhisha.  Mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Pwani, Tanga, Morogoro pamoja na sehemu ya mkoa wa Shinyanga na Simiyu na zilipoanza kunyesha zilikuwa chini ya wastani. Mazao yaliyopandwa katika baadhi ya maeneo hayo yameathirika kutokana na ukame uliojitokeza ukiwamo mkoa wa Kagera wilaya za Kyerwa, Missenyi na Karagwe. Mikoa iliyobakia mvua zimeanza kunyesha ingawa mtawanyiko wake sio wa kuridhisha.

3.0     HALI YA UPATIKANAJI CHAKULA KATIKA MIKOA
Kulingana na taarifa kutoka mikoani hali ya upatikanaji wa chakula katika masoko yaliopo katika halmashauri zote za mikoa unaridhisha isipokuwa bei ya mahindi imepanda ikilinganishwa na mwaka 2016 kipindi kama hiki. Hii inatokana na kutoingia sokoni kwa mazao mapya ya msimu wa mvua za vuli. Maeneo yaliyotolewa taarifa kuwa na uhaba mengi ni yale yaliyoonekana wakati wa tathmini ya awali ya uzalishaji msimu wa 2015/2016. Maeneo yaliyoongezeka ni kutoka katika mikoa ya Geita, Tabora na Kagera. Pamoja na kuwa mvua za vuli hazijanyesha vizuri na hivyo kutokuwepo kwa mazao mapya sokoni, mikoa bado imeonyesha kuwa na ziada ya chakula. Takwimu katika Kiambatisho hiki, kwa mazao yasiyonafaka hazijabadilishwa katika mlinganisho wa nafaka (Grain equivalent). Aidha, Mikoa  yenye kivuli taarifa zake ni za mwezi Novemba 2016 na baadhi ya mikoa takwimu zake zimetolewa katika mfumo wa wanga na zimeonyeshwa katika kipengele cha nafaka.

4.0     HALI YA UNUNUZI NA HIFADHI YA CHAKULA
Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa mwaka wa fedha 2016/2017 umepanga kununua jumla ya tani 100,000 za chakula. Hadi kufikia tarehe 8 Januari, 2017, Wakala umenunua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo ililojiwekea. Kati ya kiasi hicho, tani 38,162.280 zimenunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani 23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima. Aidha, hadi kufikia tarehe 12 Januari, 2017 Wakala una akiba ya tani 88,152.443 za mahindi.

5.0     TATHMINI YA KINA YA HALI YA CHAKULA NA LISHE
Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, FAO, TFNC pamoja na  Wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya hali ya chakula na Lishe nchini katika kipindi hiki. Tathmini inatarajiwa kukamilika tarehe 28 Januari, 2017 na itazihusisha Halmashauri 55 zenye maeneo yenye uhaba wa chakula ili kubaini kaya zilizoathirika na uhaba wa chakula na mahitaji yao. Tathmini hiyo inayosimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, itaiwezesha Serikali kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe, hasa katika maeneo ambayo yalionekana kuwa na upungufu katika tathmini ya awali na yale yaliyojitokeza mara baada ya kufanya tathmini .6.0     MWENENDO WA BEI ZA MAZAO YA CHAKULA
Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa bei za mazao ya chakula hususan Mahindi na Mchele ili kujiridhisha uwepo wake na upatikanaji wake sokoni. Mwenendo wa bei za mazao haya sokoni kwa kipindi cha mwezi Desemba, 2016 kutoka kwenye masoko 13 kati ya 25 ya miji mikuu hapa nchini umekuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali.
Bei za Mahindi, Mchele na Maharage
Bei ya wastani ya mahindi katika msimu wa chakula na soko kwa mwaka 2016/2017 imekuwa na mwelekeo wa kupanda kuanzia mwanzo wa mwezi Julai, 2016. Bei hii iko juu ikilinganishwa na bei katika kipindi kama hicho mwaka 2015/16. Katika kipindi cha mwezi Desemba 2016, bei ya mahindi kwa gunia la kilo 100 imepanda na kufikia wastani wa shilingi 84,577.00 ikilinganishwa na Desemba 2015 ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 65,104.00.

Kwa upande wa mchele bei ina mwelekeo wa kushuka ambapo bei ya wastani kwa mwezi Desemba 2016 kwa gunia la kilo 100 ilikuwa shilingi 151,957.00 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka 2015 ambapo gunia liliuzwa kwa shilingi 176,237.00. Bei ya maharage inaonyesha kushuka kidogo kutoka wastani wa shilingi 172,852.00 mwezi Desemba 2015 na kufikia wastani wa shilingi 171,251.00 mwezi Desemba 2016.

Kupanda na kushuka kwa bei kwa kipindi kama hiki ni jambo la kawaida kwani mwanzo wa msimu hakuna mazao yanayoingia sokoni na hivyo hupelekea bei kupanda na mwanzo wa mavuno bei hushuka kutokana na mazao mengi kuingia sokoni. Aidha hali ya mwenendo usioridhisha wa unyeshaji wa mvua za vuli na za msimu kwa kipindi cha 2016/17 kwa ajili ya upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2017/18 katika maeneo mengi ya nchi, imechangia wafanyabiashara wa nafaka nchini na hasa zao la mahindi kuingiza zao hili kidogo kidogo sokoni, hivyo kuongeza kasi ya uhitaji kutoka kwa wananchi na kusababisha bei kuzidi kupanda. 

Hali halisi ya mwenendo wa bei katika masoko, unaonyesha kuwa bei ya juu kabisa ya mahindi imeonekana katika soko la Lindi ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 150,000.00 wakati bei ya juu ya mchele pia imeonekana katika soko la Lindi ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 245,000.00 na bei ya juu kabisa kwa maharage imeonekana katika soko la Lindi ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 243,333.00. Bei ya chini kwa mahindi ilionekana katika soko la Mbeya ambapo gunia liliuzwa shilingi 62,600.00. Mchele bei ya chini ilionekana katika soko la Geita ambapo gunia liliuzwa kwa wastani wa shilingi 99,000.00 na maharage bei ya chini yaliuzwa kwa shilingi 136,400.00 katika soko la Mbeya.

7.0     HITIMISHO
Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa uzalishaji na upatikanaji wa chakula hapa nchini. Pale itakapobainika kuwa kuna uhitaji wa chakula, Serikali itachukua hatua stahiki. Wafanyabiashara wanahamasishwa kununua mazao ya chakula katika maeneo yaliyo na ziada na kuweza kuyauza katika maeneo yenye uhaba. Serikali itaendelea kuhimiza kusindika mazao ya chakula kwa kuyaongezea thamani na kuyauza katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kutokana na hali ya mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli na msimu kutokuridhisha katika maeneo mengi ya nchi Serikali inapenda kutoa ushauri kwa wakulima kutumia mbegu zinazokomaa mapema na kupanda mazao yanayostahimili ukame. Wakulima wanashauriwa kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya. Sekta binafsi inahamasishwa kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.

Eng. Dr. Charles J. Tizeba (MB)
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi
16 Januari 2017