Tuesday, March 7, 2017

Wakuu wa Vyuo vya Kilimo Wakutana Kujadili Kuongeza Mapato

Wakuu wa Vyuo vya Kilimo  hapa  nchini  wametakiwa kutumia vyanzo vya ndani ikiwemo mafunzo
na utafiti ili kuweza kujikwamua na changamoto ya rasilimali fedha inayokabili vyuo hivyo.                    
Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu  Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi katika Ukumbi wa         Kilimo  I Bi Nkuvililwa Simkanga amesema kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha vyuo
vijitahidi kuongeza mapato ya ndani yakiwemo utafiti na mafunzo ili kukabiliana na hali hiyo.

Aidha  Katibu Mkuu amewapongeza  wakuu wa vyuo hivyo kwa namna ambavyo wameweza kuendesha mafunzo Vyuoni pasipokuwa na fedha za kutosha na kuwataka kuendelea na mbinu hizo mpaka fedha zitakapopatikana.

Hata hivyo Siimkanga aliongeza kwamba fedha ya chakula cha wanafunzi ilitengwa na kulindwa 
(ring fenced) ambapo mawasiliano ndani ya serikali yanaendelea kufanyika ili upatikanaji wa fedha hizo ukamilike.

Monday, March 6, 2017

Serikali Kushirikiana na FAO Kupambana na Sumukuvu, Uhifadhi Bora wa Mazao baada ya Uvunaji

Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi  na Shirika la Chakula Duniani (FAO) wamewekeana sahihi juu miongozo ya mashirikiano  baina yao lengo likiwa ni kupambana na  tatizo la sumukuvu katika baadhi ya maeneo hapa nchini pamoja na uboreshaji wa uhifadhi wa chakula baada ya kuvunwa.

Akiongea na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Kilimo I hapa Dar es Salaam hivi karibuni mwakilishi wa FAO bwana Fred Kafeero amesema makubaliano hayo yatahusisha miradi mitatu ambayo ni  kupambana na sumukuvu,kusaidia vikundi vya wakina mama mkoani Kagera waliokumbwa na maafa ya tetemeko la ardhi na kusaidia namna bora ya uhifadhi baada ya mavuno.

Aidha Bwana Kafeero aliongeza kwamba miradi hiyo inachukua kipindi cha miaka  minne na ina thamani  ya dola za kimarekani 17,641,000  kwaujumla.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Eng.Mathew Mtigumwe amesema amelishukuru shirika la chakula duniani kwa kukubali kushirikiana na serikali katika kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo kwa sasa.

Eng. Mtigumwe amesisitiza kuwa serikali kwa kushirikiana na FAO watatumia sehemu ya mradi huo kuelimisha wananchi  hasa wa kanda ya kati ili kuepukana na matatizo yanayoweza kusababishwa na aina hiyo ya sumu.