Thursday, June 29, 2017

NFRA- YASHUSHA MFUMUKO WA BEI YA NAFAKA
Serikali imesambaza mahindi katika baadhi ya Halmashauri kwa bei nafuu lengo likiwa ni kupunguza bei ya mahindi  ambayo wafanyabiashara walikuwa wanayauza kwa gharama kubwa kwa kilo na kusababisha wanachi kushindwa kununua
Usambazaji huo ulifanywa na wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula(NFRA) katika maeneo ambayo yalionekana kuuza bidhaa hiyo kwa bei kubwa na hasa sehemu ambazo kulikuwa na upungufu wa chakula
Akiongea na Kitengo cha Mawasilioano Serikalini Kaimu Meneja wa Kanda ya NFRA Dodoma bwana Felix Ndunguru amesema lengo la zoezi hili ni  Kukabiliana na upandaji wa bei za chakula katika baadhi ya halmashauri na kupunguza bei ya mahindi
 Bwana Ndunguru alisema kwamba zoezi lilianza tarehe 16/5 /2017 na litaendelea mpaka mwezi wa 17 /6/2017 ambapo katika Kanda ya Dodoma Halmashauri zilizolengwa ni Manyoni, Itigi, Chamwino, Nchemba Bahi na Kondoa ambapo zilionekana bei ya nafaka kuwa juu .
Aidha katika kanda ya Dodoma Bwana Ndunguru anasema zoezi limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani kabala serikali kupitia wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula ( NFRA) kusambaza mahindi kwa bei nafuu, kilo moja ya mahindi ilikuwa inauzwa katika shilingi 1300 mpaka 1500 ambapo baada ya usambazaji huo  bei ya mahindi imeshukwa  hadi kufikia shilingi 600 hadi 800 kwa kilo katika maeneo mengi ya mji huo
Hata hivyo Bwana Nduguru alisema zoezi la usambazaji wa chakula  kwa bei nafuu ni la kitaifa kwa sababu linahusisha kanda zote zilizoko chini ya wakala wa taifa wa uhifadhi wa chakula.
Aidha Kanda ya Shinyanga inayojumuisha Mkoa wa Tabora, Mwanza, Mara na Shinyanga na Simiyu walipata mgao wa tani 4000 ambazo zilikuwa zimegawanywa katyika Halmashauri ambazo zilionekana kuwa na uhaba wa chakula
Alipohojiwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bwana Jeremia Kilembe Kaimu Meneja wa Kanda  hiyo alisema kuwa  tani 3600 zimeshauzwa zikabaki tani 400 ambazo nazo zinategemewa kuuzwa hivi karibu
‘Wananchi wamepokea zoezi vizuri  na ndio maana tulikuwa tumepangiwa kuuza tani 4000 mpaka sasa tayari tani 3600 zimeuzwa zimebaki 400”
Hata hivyo bwana jeremia alisistiza kwamba katika maeneo ya Musoma uhitaji wa mahindi ni  mkubwa sana ukilinganishwa na sehemu nyenginezo.
Naye Ramadhani Athumani Nondo Kaimu meneja  Kanda ya kaskazini Arusha inayohusisha Mikoa ya Manyara,Kilimanjaro  na Babati anasema mahindi yalisambazwa katika wilaya nane(8) za Babati, mbulu,Simanjiro,Mwanga ,Same,Longido,Munduli na Loliondo.
Kwa mujibu wa  bwana Nondo zoezi lilifanikiwa kwakiasi kikubwa kwani mfumuko wa bei ulishapunguwa kutoka shilingi 1500 kwa kilo mwanzoni hadi kufikia shilingi 1000 baada ya kuingiza mahindi sokoni
“Bei elekezi 650 ila serikali ya wilaya nayo inapanga bei zake lakini hazizidi 800 kutegemeana na umbali kutoka kijiji hadi kijiji alisema”. Bwana NondoWednesday, June 21, 2017

WADAU WA SEKTA YA MBEGU WAHIMIZWA KUWEKEZA ZAIDI KUZALISHA MBEGU ZA MBOGAMBOGA HAPA NCHINI.Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi  Mhe. Charles John Tizeba, amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa kushirikisha Wadau wa Tasnia ya Mbegu kuandaa mkakati wa kusaidia uzalishaji wa kutosha wa mbegu  za mazao ya  mbogamboga.  Amesema hayo katika Warsha ya Wadau wa Mbegu iliyofanyika  katika Hoteli ya Mount Meru Arusha. 

Mhe. Waziri amesema, nchi kwa sasa inaupungufu mkubwa wa mbegu za mbogamboga ingawa uzalishaji wa mazao hayo umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa katika Uchumi na pato la Taifa.
Amesema, Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kupitia Sheria ya Mbegu Na.18 ya Mwaka 2003 imefanya maboresho makubwa ya kuwezesha mbegu za Kilimo kupatikana kwa wingi hapa nchini. Kupitia marekebisho ya Sheria na Kanuni, kwa sasa, muda wa majaribio ya mbegu mpya umepunguzwa kutoka miaka mitatu na sasa majaribio hayo ni msimu mmoja tu hususan kwa mbegu zinazotoka nchi zenye makubaliano ya udhibiti wa Ubora wa mbegu na Tanzania ikiwemo nchi za SADC.

Aidha , Mhe. Waziri ameiagiza Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu nchini (TOSCI) kusimamia kwa karibu Sheria ya Mbegu ili kusaidia kuwalinda wakulima dhidi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu ambao wanauza mbegu zisizo na ubora  (Mbegu feki).
Awali, aliwaeleza Wadau wa Mbegu nchini kuwa nchi ina  upungufu wa mbegu bora kutokana na uwekezaji mdogo kwenye tasnia ya Mbegu.

Aliwajulisha Wadau kuwa ili kuwezesha sekta binafsi kuzalisha mbegu zilizogunduliwa na vituo vya Utafiti vya Serikali, Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi imetoa Waraka maalumu unaoweka utaratibu wa jinsi ya sekta binafsi itakavyoweza kupata kibali cha kutumia mbegu hizo za umma.
Amewaahidi Wadau kuimarisha Maabara ya Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI) ili iweze kutekeleza vyema mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu masuala ya ubora  wa mbegu. Alisema, Wizara itatoa kiasi cha Dola za Kimarekani  13,000 kwa ajili ya kuwezesha Maabara ya TOSCI kupata ithibati (accreditation) ya Shirika la Kimataifa la Mbegu (ISTA). Ithibati hiyo itasaidia mbegu zinazozalishwa nchini ziweze kuuzwa bila kikwazo nje ya Tanzania.
Amewataka Wadau wa Mbegu kutumia fursa ya ardhi yenye rutuba kuanzisha na kuendeleza mashamba ya mbegu. Pia, aliwaasa washirikiane na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ili kupata maeneo ya kuzalisha mbegu kwa makubaliano maalumu.

Ameongelea fursa kubwa iliyopo kwenye kilimo kwa kuondolewa kwa tozo kwenye maeneo mbalimbali kwenye sekta ya kilimo. Alisema, takriban tozo 80 zimeondolewa kwa Wizara ya Kilimo tu ukiondoa zile zilizokuwa zikisimamiwa na Wizara nyingine.

Aliwapongeza wafanyabishara wa mbegu kwa kuwa kiungo muhimu kwenye maendeleo ya tasnia ya mbegu. Aliahidi Wizara yake kuyafanyia Kazi yale ambayo yataazimiwa na Wadau wa mbegu.

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mhandisi Dk. Charles Tizeba

Friday, June 9, 2017

Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima –Nane Nane Mwaka 2017

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi anatangazia umma kuwa Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima – Nane Nane mwaka 2017, ngazi ya Ki-Taifa zitaadhimishwa katika Uwanja wa Maonesho ya Kilimo wa Ngongo, Manispaa ya Lindi. Maandalizi na maonesho hayo yanaratibiwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na uongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara. 

Uratibu wa maonesho ya mwaka huu ngazi ya Ki-Taifa unafanywa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa kuwa Taasisi ya Kilimo Tanzania (TASO) iliyokuwa inaratibu maandalizi na maonesho ya Wakulima (Nane Nane) miaka ya nyuma imefutiwa usajili wake mwezi Mei 2017. Washiriki wa maonesho ya kilimo na sherehe za Ki-Taifa wawasiliane moja kwa moja na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi au Sekretarieti za Mikoa ya Lindi na Mtwara. 

Aidha, maadhimisho ya Ki-Kanda yatafanyika katika  viwanja vya maonesho ya John Mwakangale –Mbeya; Mwalimu J.K. Nyerere –Morogoro; Themi – Arusha; Nzuguni -  Dodoma; Nyahongolo – Mwanza; na Fatuma Mwassa - Tabora. Maandalizi na maonesho ya  Ki-Kanda yanaratibiwa na uongozi wa  mikoa husika. Washiriki wa maadhimisho ya Ki-Kanda wanatakiwa kuwasiliana na Sekretarieti za Mikoa husika ili kupata maelekezo na taratibu zingine za ushiriki. 

Hivyo kuanzia sasa utaratibu wa maandalizi na maonesho ya sherehe za wakulima (Nane Nane) ni kama ulivyotolewa katika tangazo hili. Maelezo zaidi kuhusu maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima yataendelea kutolewa kupitia njia zifuatazo:-
www.tzagriculture.blogspot.com;
www.twitter.com/tzagriculture
WOTE MNAKARIBISHWA