Thursday, September 14, 2017

SERIKALI YAANZA JITIHADA ZA KUWAKABILI VIWAVIJESHI HATARI AINA YA FALL ARMYWORM (FAW)Kiwavijeshi mpya aina ya Fall Armyworm (FAW)Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema akizungumza wakati akifungua warsha ya siku moja kujadili namna ya kukabiliana na mdudu aina ya Kiwavijeshi
Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm (FAW) wakishambulia mahindi shambani

Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi imeanza jitihada za kuwakabili Viwavijeshi wapya aina ya Fall Armyworm (FAW) wanaojulikana kitaalamu kama Spodoptera Frugiperda ambao wametajwa kuwa na uwezo mkubwa kuharibu mazao mbalimbali hususan mahindi ambayo ndio zao kuu la chakula nchini.


Imeelezwa kuwa Viwavijeshi hao wanapofika kwenye mazao hutoa kemikali ambayo huweza kudanganya mmea kuwa unashambuliwa na magonjwa kama ukungu au fangasi hivyo mmea unapohisi unashambuliwa na hayo magonjwa, hupunguza kinga dhidi ya wadudu hao hatari na kuwa rahisi kushambuliwa. 


Hayo yamebainishwa leo Septemba 14, 2017 na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bwana Beatus Malema wakati akifungua warsha ya siku moja mbele ya Wadau wa Kilimo ambao ni Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani USAID, ONE HACKER FUND, Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki  (TPRI), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), na Mradi wa WEMA.


Mkutano ulikuwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja kwa ajili ya kumkabili mdudu huyo aina ya Fall Armyworm (FAW) ambaye anashambulia mazao mbalimbali nchini hususani zao la mahindi.


Alisema Athari ya viwavijeshi haishii kuharibu majani ya mimea pekee, wadudu hao wanapokula majani na kutengeneza sumu aina ya ‘firenide’ inayodhuru mifugo inapokula majani yaliyoathiriwa.


Bwana Malema amesema tayari Serikali imechukua juhudi za awali kukabiliana na mdudu huyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya utambuzi wa mdudu huyo kwa kuwataka Wananchi kung’oa mazao na kuyachoma pindi wanapobaini uwepo wa mdudu huyo.


Pia tayari dawa tatu zimepitishwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi ya uchunguzi wa Viatilifu (TPRI) zinazoangamiza wadudu hao ambazo ni Duduba 450, Mupacrone 500 EC na Match Save kutoka Kampuni ya Syngenta hivyo Wananchi wametakiwa kuzitumia haraka pindi wanapoona dalili za kuwepo wa wadudu hao shambani.


Bwana Malema amesema kuwa katika kipindi cha miaka mingi Tanzania imekuwa ikikumbwa na viwavijeshi aina ya African Armywarms ambapo mara zote imekuwa ikiwadhibiti wadudu hao wanapojitokeza kwa kuwapa kiuatilifu kinachosababaisha matumbo ya wadudu hao kujaa na hatimaye kuwasababishia vifo.


Ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza Wizara ilipata taarifa ya uvamizi katika shamba la Mwekezaji mkubwa Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa mwezi Machi 2017 na walipofuatilia na kupeleka sampuli maabara mdudu huyo alibainika kwa jina la  Spodoptera frugiperda au Fall arymworm ambaye ni hatari na amekuwa akiripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani.


Kutokana na unyeti wa suala hilo Wizara ya Kilimo imewasiliana na  Shirika la Chakula Duniani (FAO), kwa ajili ya kuunganisha juhudi za pamoja ili kumdhibiti mdudu huyo kabla hajasambaa kwenye maeneo mengi nchini.Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika taarifa yake imesema viwavijeshi hao aina ya Fall armyworm wameonekama pia katika nchi za Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Namibia Afrika ya Kusini na Zambia huku chanzo chake ikiwa ni nchini Marekani.Kwa mujibu wa Redio ya Umoja wa Mataifa, FAO bado haijatangaza   kiwango kamili cha uharibifu katika nchi hizo, huku ikiongeza kuwa Shirika hilo na Wadau wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamejadili  udhibiti wa viwavijeshi.


Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Afya ya Mimea, Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Bibi Beatrice Palangyo akiwasilisha mada ya utambuzi wa wadudu hao katika warsha hiyo amesema kuwa katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wadudu hawa walianza kuingia nchini Nigeria na kwa sasa wameenea katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Afrika kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Malawi.


Alisema wadudu hao wanashambulia mazao ya jamii ya nafaka kama mahindi (Corn) wanauwezo wa kushambulia hata magugu pale wanapokosa mazao kama mahindi kwani hawali mazao mengine kama mboga na matunda, wanakula zaidi mahindi na magugu yanayofanana na mahindi.


Zaidi ya Mikoa 15 nchini ikiwemo Zanzibar imeripoti kuwepo kwa kadhia ya mdudu huyo hivyo asilimia 15 ya mazao jamii ya nafaka kama mahindi yameathiriwa, jambo ambalo kama lisingepatiwa ufumbuzi wa haraka, lingesababisha upotevu mkubwa wa mazao mashambani na kutishia upatikanaji wa chakula nchini.Wednesday, September 6, 2017

WAZIRI TIZEBA AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MKUU WA (FAO) JOSÉ GRAZIANO DA SILVA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), Bwana José Graziano da Silva, Jana, Septemba 5, 2017 amefanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kikazi nchini Tanzania. 

Katika ziara hiyo Bwana Graziano da Silva atafanya mazungumzo na Viongozi waandamizi wa Serikali, Wadau na anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein sambamba na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, Bwana Hamad Rashid Mohamed.

Ziara hii ya Mkurugenzi Mkuu inajili wakati FAO ikiadhimisha miaka 40 toka kuanza shughuli zake hapa Tanzania Hafla ambayo itahudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Samia Suluhu Hassan. 

Katika mazungumzo na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi Mkuu wa FAO anabadilishana mawazo na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwenye masuala makuu yanayohusiana na uhakika wa chakula na maendeleo ya kilimo, ikijumuisha juhudi za FAO kitaifa na kikanda.

Pia yamejadiliwa mambo mengine yanayohusiana na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na FAO, pia masuala ya umuhimu kati ya pande hizo mbili.

Mbali ya Maafisa wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu atakutana na Wadau wengine wa FAO hapa nchini wakiwa ni pamoja na Asasi za Kiraia, Taasisi za Elimu, na Taasisi za Utafiti. 

Baadae Mkurugenzi Mkuu ataenda Zanzibar ambapo, miongoni mwa mambo mengine, anategemewa kuweka jiwe la msingi katika jengo la Mradi wa Kuzalisha vifaranga vya samaki unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa, KOICA. 

Pia Bwana Graziano da Silva atapata fursa ya kutembelea Mradi wa kilimo cha mwani na pia kuona maonesho ya bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa na wanawake wanaojihusisha na kilimo cha mwani. 

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alisema kuwa ujio wa Bw. Graziano da Silva nchini unaakisi ushirikiano bora uliopo kati ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO) ambapo hivi karibuni ILO walisaidia katika kuandaa mpango wa kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa fedha ya kutengeneza programu ya kutoa maarifa kwa wananchi ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika kilimo.

Dkt. Tizeba alisema kuwa tayari jarida limeshatengenezwa la namna ambavyo wananchi hususani wakulima katika kilimo chao wataweza kukabiliana na hali ya ukame au mafuriko kutokana na mvua zilizozidi kiwango.

Sambamba na hayo Mhe. Tizeba alisema pia FAO wametoa simu 50 na Kompyuta 15 kwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya Wataalamu wake kuwa na urahisi wa kukusanya taarifa na kuzifikisha kwa jamii.

Tanzania ilijiunga na FAO mwaka 1962, na mwaka 1977 . FAO ilifungua ofisi zake hapa Tanzania, katika miaka 40 ya uwepo wake, FAO imeisadia Serikali ya Tanzania katika kupanga na kutekeleza sera, mikakati na mipango ya kilimo hapa nchini. 

Kazi ya FAO imejikita katika kuboresha usalama wa chakula na lishe pamoja na maisha ya wakulima wadogo na hivyo kuwa chachu ya kukua kwa uchumi kupitia Sekta ya Kilimo. 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva (Kulia), akimpongeza Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba mara baada ya kuelezea taarifa mbalimbali zihusuzo Wizara.Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt. Charles Tizeba akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva, kuzungumzia ujio wake nchini na ushirikiano baina ya FAO na Serikali ya Tanzania.Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva, akizungumzia na wataalamu mbalimbali katika Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi juu ya ujio wake nchini na ushirikiano baina ya FAO na Serikali ya Tanzania. Kulia kwake ni Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe, Dkt. Charles Tizeba.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva (Kushoto) akiteta jambo na mwenyeji wake Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba mara baada ya kutembelea ofisini kwake. leo Jumanne Septemba 5, 2017.Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba akipokea simu 50 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silvakwa ajili ya wataalamu wa kilimo kuzitumia kukusanya taarifa mbalimbali na kuziwasilisha kwa jamii.Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba akionyesha moja ya simu kati ya 15 alizokabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva kwa ajili ya wataalamu wa kilimo kuzitumia kukusanya taarifa mbalimbali na kuziwasilisha kwa jamii.Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva akipokea zawadi ya vinyago kutoka kwa Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba mara baada ya mazungumzo ya kikazi kumalizika.


Picha ya pamoja kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva (Aliyeketi kwenye kiti kulia), Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt Charles Tizeba, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Dkt. Marry Mashingo na Wataalamu wengine kutoka FAO na Wizara ya Kilimo.