Sunday, May 20, 2018

HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO, MHESHIMIWA MHANDISI DKT. CHARLES JOHN TIZEBA (MB), AKIWASILISHA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KILIMO KWA MWAKA 2018/2019

HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO, MHESHIMIWA MHANDISI DKT. CHARLES JOHN TIZEBA (MB), AKIWASILISHA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KILIMO
 KWA MWAKA 2018/2019
   
DODOMA
15 MEI 2018

1.0            UTANGULIZI

2.      Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Kawaida na ya Maendeleo ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa Fedha wa 2018/2019. Hoja hii inawasilishwa kwa kuzingatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni mapema leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji.
3.      Mheshimiwa Spika,sisi ni waja wa Mwenyezi Mungu. Hivyo, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema alizoturehemu kutuwezesha kufikia siku ya leo, tukiwa wazima wa afya njema na majaliwa ya amani kwa nchi yetu kwamba tunaweza kujadili bajeti hii inayolenga kusukuma mbele kasi ya maendeleo ya Watanzania, hususan wakulima.
4.      Mheshimiwa Spika, ninayoheshima ya kipekee kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uchungu alionao kwa Watanzania na msukumo dhahiri anaoutoa katika kuendeleza Sekta ya Kilimo. Anafanya hivi kwa kuamini kwake kuwa sekta hii ina umuhimu wa kipekee katika mustakabali wa maisha ya watanzania wengi kiuchumi na ushiriki wao katika ujenzi wa uchumi tarajiwa wa viwanda. Nakiri ameweka imani kubwa kwa kuweka dhamana hii kwangu. Faraja yangu ni namna anavyonipa shime na miongozo bayana kuhusu mabadiliko na maendeleo anayoyakusudia katika sekta hii. Uthibitisho wangu ni namna alivyotumia muda na umahiri wake mkubwa katika kuongoza Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Council-TNBC) uliofanyika jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 19 Mwezi Machi, 2018.
Lengo kuu la mkutano huu ulikuwa kubaini namna tutakavyoweza kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara nchini.
Kupitia mkutano huo, aliweka bayana haja ya kuondoa utitiri wa kodi, tozo na ada kwa sekta za kilimo na shughuli nyingine zitokanazo kwa lengo la kumwezesha mkulima kupata manufaa stahiki kulingana na jasho lake na pia kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao kama vile  mahindi, mpunga, sukari, korosho, chai, kahawa, pamba, tumbaku na mbegu za mafuta.
5.      Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumuahidi Mhe. Rais, Bunge lako Tukufu, Wakulima na Watanzania wote kwamba sitawaangusha. Kwa kadri itakavyowezekana, nitatumia uwezo wangu wote, tena kwa unyenyekevu, uaminifu na uadilifu mkubwa,kuhakikisha kwamba rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo zitatumika kwa ufanisi na kuwafikia walengwa, hasa wakulima ili waongeze uzalishaji, tija na ubora wa mazao na kujipatiamanufaa stahiki kwa jasho lao.
6.      Mheshimiwa Spika,msingi wa ustawi wa kilimo ni upatikanaji wa soko la uhakika. Namshukuru sana Mhe. Rais kwa kulivalia njuga suala la kuvutia uwekezaji katika viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini, hasa za mazao ya kilimo. Matokeo ya juhudi hizi yameanza kuonekana. Hivi karibuni tumeshuhudia akizindua viwanda katika mikoa mbalimbali nchini kama vile Kagera, Mwanza, Shinyanga, Singida, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, vingi kati ya viwanda hivyo vinatumia malighafi za kilimo, kudhihirisha kuwa tumeanza kupata muunganiko wa shughuli za viwanda na kilimo nchini, jambo ambalo lilishindikana kwa muda mrefu.
7.      Mheshimiwa Spika,kipekee napenda kukutambua na kupongeza juhudi za Mhe. Samia Suluhu Hassan,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuhimiza utunzaji wa mazingira kwa ustawi endelevu wa uchumi na maisha ya watu.
Katika ziara zakembalimbali nchini moja ya ajenda yake kuu ni kutuasa juu ya kuendesha shughuli zetu huku tukizingatia hifadhi ya mazingira na kujenga uwezo wa kuhimili mabadiliko ya mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi. Maelekezo hayo yamezingatiwa katika utekelezaji wa majukumu na mipango ya Wizara.
8.      Mheshimiwa Spika, niruhusu pia kutumia fursa hii kumshukuru Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa muda wake mwingi anaotumia kuhamasisha na kutoa maelekezo muhimu yenye lengo la kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya kilimo, hususan mazao mkakati kama vileChai, Kahawa, Korosho, Pamba na Tumbaku. Sanjari na hili,Mhe. Waziri Mkuu amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha muunganiko wenye tija wa shughuli za kilimo na masoko hasa ya ndani. Katika hili ameweka azma ya kweli ya kufufua na kuimarisha maendeleo ya vyama vya ushirika nchini. Vile vile, kwa lengo la kuchochea mageuzi ya kilimo nchini, Mhe. Waziri Mkuu aliongoza Kikao Kazi cha Baraza la Mawaziri kilichojadili na kuridhia Utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II), programu ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi hivi karibuni Jijini Mwanza.
9.      Mheshimiwa Spika, aidhanitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kumpongeza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kwa hotuba yake na pia Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango kwa taarifa zake mbalimbali zilizotoa ufafanuzi kuhusu hali halisi ya uchumi kwa mwaka 2017, mwenendo na mwelekeo wa sekta ya kilimo kwa mwaka ujao, misingi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/2019, ambazo zimeweka misingi ya hotuba yangu.
10.  Mheshimiwa Spika,nitakuwa mnyimi wa fadhila ikiwa nitajisahau na hivyo kushindwa kutambua na kukupongeza wewe mwenyewe, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge kwa umahiri mkubwa. Bunge letu hivi sasa limerejesha hadhi na heshima yake na wananchi wana matarajio makubwa na Muhimili huu katika kutetea mustakabali wa maendeleo yao.Uongozi wenu, ndio umetufikisha hapa.Aidha, nitumie nafasi hii pia kuwapongeza Wabunge wote kwa umahiri wao mkubwa katika mijadala inayoendelea katika Bunge hili la Bajeti.
11.  Mheshimiwa Spika,kipekee napenda kutambua ushirikiano, maoni na ushauri wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa, Mbunge wa MufindiKaskazini na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Christine G. Ishengoma (Mb). Naomba nistakabadhi shukranizetu za dhati kwa miongozo waliyotupatia wakati wote wa maandalizi ya bajeti ya Wizara kwa mwaka 2018/2019. Naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tutaendelea kuipatia Kamati ushirikiano kwani kwa njia hii, ndiyo tutaweza kutekeleza lengo letu la kubadilishakilimo nchini kufikia matarajio ya jamii na uchumi wa kati. 
12.  Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu,niruhusu nitoe shukrani kwa wananchi wa Jimbo langu la Buchosa kwa ushirikiano na uvumilivu wanaoendelea kunipatia pale ninapokuwambali nao, nikitakiwa kutekeleza dhamana yangu hii. Nawapongeza kwa ushirikiano na kuwapa shime kwa juhudi wanazofanya katika kujiletea maendeleoyao wenyewe na maendeleo ya jimbo letu.
13.  Mheshimiwa Spika, baada ya salaam na shukrani hizi niruhusu sasa nitoe ufafanuzi, kwa muhtasari, wa hali ya kilimo nchini.
HALI YA KILIMO NCHINI
14.  Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo nchini imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla hususan katika wakati huu tunapojizatiti kufikia uchumi wa viwanda. Sekta hiyo imeendelea kuimarika na hivyo kuchangia asilimia 30.1 katika Pato la Taifa kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 29.2 kwa mwaka 2016.

1.1              Hali Ya Upatikanaji Wa Chakula

15.  Mheshimiwa Spika,tathmini ya awali ya Uzalishaji wa Mazao ya Chakula nchini kwa msimu wa 2016/17 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2017/18 iliyofanyika mwezi Juni 2017 imebaini kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa 2016/17 ulifikia tani 15,900,864. Uzalishaji wa mazao ya nafaka ambayo ndiyo kipimo kikuu cha hali ya upatikanaji wa chakula, ulifikia tani 9,388,772, ambapo mahindi yalikuwa tani 6,680,758 na mchele tani 1,593,609. Uzalishaji wa mazao mengine yasiyo ya nafaka ulifikia tani 6,512,092.
16.  Mheshimiwa Spika,upatikanaji wa chakula nchini ukilinganishwa na mahitaji umeendelea kuwa imara. Mahitaji ya chakula kwa mwaka 2017/18 ni tani 13,300,034 kati ya hizo, mahitaji ya nafaka ni tani 8,457,558 na yasiyo ya nafaka ni tani 4,842,476. Kwa ujumla kuna ziada ya tani 2,600,831.Kati ya hizo kwa nafaka,kuna ziada ya tani 931,214 na kwa mazao mengine yasiyo ya nafaka,ziada nitani 1,669,617. Hali hii inafanya Taifa liwe na kiwango cha utoshelevu wa chakula cha asilimia 120 ikilinganishwa na kiwango cha utoshelevu cha asilimia 123 kwa mwaka 2016/2017.Hivyo, kufuatia hali hii, Serikali imeruhusu mazao ya chakula, ikiwa ni pamoja na mahindi kuuzwa nje ya nchi. Hali hii pia imesaidia kushuka kwamfumuko wa bei kufikia asilimia 6.2 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwezi Desemba 2016.Ili kuboresha masoko kwa mazao ya chakula, hususan mahindi, Serikaliitaanzisha utaratibu wa kutoa vibali mipakani kwa mfumo wa kielektroniki, ambapo waombaji wataweza kupata huduma yavibali vya kusafirisha nje bila kulazimika kwenda Makao Makuu ya Wizara ya Kilimo kuvifuata.
17.  Mheshimiwa Spika,licha Taifa kujitosheleza kwa chakula, bado kuna Halmashauri ambazo zina maeneo yenye upungufu wakujirudia rudia kila mwaka. Hali hii inapelekea kuwa na matatizo ya usalama wa chakula na lishe katika maeneo husika. Ili kukabiliana na changamoto hii, Serikali kwa kushirikiana na wadau itafanya tathmini katika kipindi cha mwezi Mei hadi Juni, 2018kubaini mwelekeo wa hali ya uzalishaji kwa msimu wa 2017/18 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/19.

1.2              Maendeleo ya Ushirika

18.  Mheshimiwa Spika,hali ya ushirika nchini imeendelea kuimarika  ambapokufikia Desemba 2017 vyama vipya 394 vilisajiliwa na kufanya idadi ya vyama kufikia 10,990 kutoka 10,596 vilivyokuwepo Machi 2017. Vyama hivi vinakadiriwa kutoa ajira mpya takribani 1,182. Katika kipindi hicho, wanachama wapya 385,295 walijiunga kufanya idadi ya wanachama kuongezeka kutoka 2,234,016 hadi 2,619,311. Aidha,amana za SACCOS zimeongeza kufikia shilingi bilioni 53 mwaka 2017/18 ikilinganishwa na shilingi bilioni 47 mwaka 2016/2017.Ufafanuzi wa mwenendo wa ushirika nchini umetolewa kutoka aya ya 18 hadi 24 za kitabu cha hotuba.

1.3              Mwelekeo na Malengo ya Sekta ya Kilimo

19.  Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa Sekta ya kilimo kufikia mwaka 2025 ni kuleta mageuzi (transformation), kutoka mtazamo wa kilimo cha kujikimu kuelekea katika mfumo wa kibiashara.
Lengo la mageuzi haya ni kuhakikisha kuwa shughuli za kilimo zinakuwa na manufaa kwa nchi na wakulima,pia kuendana na dhamira ya kuwa uchumi wa viwanda wa hadhi ya kipato cha kati.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha malengo yetu ya kubadili kilimo yanafanikiwa, mazao makuu 5 ya kilimo (Pamba, Kahawa, Tumbaku, Chai, na Korosho) yatauzwa na kununuliwa kupitia vyama vya ushirika vya wakulima (AMCOS).
Naomba ieleweke  kwamba vyama vya ushirika siyo vitakavyonunua mazao haya bali wanunuzi/wafanyabiashara ndio watakaonunua mazao ya wakulima kupitia vyama vya ushirika.
Ni marufuku vyama vikuu vya ushirika  au vyama vya msingi vya ushirika kupeleka dhana kwa wananchi kwamba vyenyewe ndivyo vinavyonunua mazao ya wanachama wake.  Kazi ya vyama ni kuleta pamoja mazao ya wakulima ili wafanyabiashara wanunue au moja kwa moja au kwa njia ya mnada.
Kahawa: Vyama vya ushirika vitakusanya na kupeleka  kahawa mnadani. Pamba: Vyama  vitasimamia kukusanya na kuhakiki ubora wa pamba ili wanunuzi waje kununua  kutoka  katika maghala ambayo ushirika utakuwa umeyaanda.Maelezo ya kina juu ya mwelekeo na malengo ya sekta yakilimo yanapatikana katika aya za 25 hadi 28 za kitabu cha hotuba yangu.

2.0      TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI KWA MWAKA 2017/18 NA MPANGO KWA MWAKA 2018/19


20.  Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo ina mafungu mawili, Fungu 43 – Wizara ya Kilimo na Fungu24 – Tume ya Maendeleo ya Ushirika,taarifa ya utekelezaji wa shughuli katika mafungu husika ni kama ifuatavyo:

2.1      Mapato na Matumizi ya Fedha katika Kipindi cha mwaka 2017/18, Fungu 43

2.1.1               Makusanyo ya Maduhuli

21.  Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo kwa Fungu 43 katika mwaka 2017/2018 ilikadiria kukusanya mapato ya Shilingi 2,015,010,000kutokana na vyanzo mbalimbali.
Kufikia tarehe 31 Machi, 2018 Wizara ilikusanya jumla ya Shilingi 1,708,724,841.68, sawa na asilimia 84.80 ya makadirio, na  Wizara bado inaendelea kukusanya maduhuli hadi tarehe 30 Juni 2018.

2.1.2               Fedha Zilizoidhinishwa

22.  Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo, Fungu 43, ilitengewa jumla ya Shilingi 214,815,759,000. Kati ya hizo, Shilingi 64,562,759,000 zilikuwani kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi 150,253,000,000 kwa shughuli za maendeleo.

2.1.3               Matumizi ya Bajeti ya Kawaida

23.  Mheshimiwa Spika,kufikia tarehe  31 Machi, 2018 jumla ya Shilingi  36,069,819,172 kati ya Shilingi64,562,759,000 zilizopitishwa kwa Fungu 43 kwa mwaka 2017/ 18 kwa matumizi ya kawaida zilikuwa zimetolewa na kupokelewa, sawa na asilimia 55.87 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge. Kati ya fedha zilizopokelewa Shilingi  33,054,942,776.63,sawa na asilimia 91.64zilikuwa zimetumika.

2.1.4               Matumizi ya Maendeleo

24.  Mheshimiwa Spika,Wizara ya Kilimo, Fungu 43, kwa mwaka wa 2017/18, ilitengewa jumla ya Shilingi 150,253,000,000 kwa utekelezaji wa shughuli zamaendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi  59,600,000,000 zilikuwafedha za ndani na Shilingi 90,653,000,000 za nje. Shilingi 27,231,305,232.69, sawa na asilimia 18 ya fedha zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge. Aidha, kufikia tarehe hiyo fedha zote zilizokuwa zimetolewa, zilikuwa zimetumika, sawa na asilimia 100 ya fedha za maendeleo zilizopokelewa.

2.2      Hali Halisi ya Utekelezaji wa Majukumu kwa Mwaka 2017/18 na Mpango kwa Mwaka 2018/19

25.  Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimokwa Fungu 43 katika mpango na bajeti ya mwaka 2017/18 ina Maeneo nane (8) ya Kipaumbele. Maeneo haya yanatekelezwa kupitia mipango-kazi ya Idara, Vitengo, Asasi na Taasisi za Wizara kama inavyoelezwa  kuanzia aya ya 34 hadi 194 za kitabu cha hotuba. Kwa muhtasari,utekelezaji wa maeneo haya ni kama ifuatavyo:

2.2.1   Kusimamia Matumizi Endelevu ya Ardhi ya Kilimo na Maji

26.  Mheshimiwa Spika,Wizara ikishirikiana na Wizara za Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Viwanda Biashara na Uwekezaji, Ofisi ya Rais - TAMISEMI na  Sekta binafsi kwamwaka 2017/18 imewezesha kupatikana ardhi ya uwekezaji mkubwa katika mashamba ya miwa na uzalishaji wa sukari katika eneo laMkulazi lenye hekta 60,000, Bagamoyo lenye hekta 10,000, na Mbigiri lenye ekari 12,000. Aidha, imeweza kuvutia wawekezaji, ambapo kwa shamba la Mkulazi ni kampuni ya Mkulazi Holding Company LTD, Bagamoyo niKampuni ya Bakhresa Group of Companies, na kwa  Mbigiri ni kampuni ya Mkulazi Holding Company LTD ikishirikiana na Jeshi la Magereza. Ili kuwanufaisha wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba la Mkulazi, Wizara kupitia ushirikiano wa kitaasisi imewezesha kutolewa hati za Hakimiliki 400 za Kimila  kwa wananchi wa Kijiji cha Chanyumbu.
27.  Mheshimiwa Spika,katika eneo hili, Wizara kwa mwaka 2018/19 imepanga kutekeleza mpango wa kujenga mabwawa ya kuvuna, kuhifadhi na kilimo cha umwagiliaji katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Aidha, Wizara itajenga bwawa la Kalege na miundombinu ya umwagiliaji kwa eneo la takriban hekta 11,700 na litahudumia Halmashauri za Bukoba Vijijini na Misenyi. Bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo 2,780,000 ambapo litasaidia upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo, ufugaji wa samaki (aquaculture) na kuchangia kupunguza uharibifu wa vyanzo vya maji (degraded sub-catchments) katika bonde la Mto Ngono Mkoani Kagera. Vilevile, bwawa hilo litatumika kwa ajili ya kuhifadhi maji kwa matumizi wakati wa kiangazi, kuboresha ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi, kuzuia athari za mafuriko katika eneo la takriban hekta 3,555, na uzalishaji wa megawati 2.46 za umeme.

2.2.2   UpatikanajiwaPembejeo za Kilimo

Mbolea
28.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/18,Wizara ilijielekeza katika kuimarisha upatikanaji wa mbolea. Kufikia mwezi Aprili, 2018 tani 435,178zilikuwa zimeingizwa na wafanyabiashara walioruhusiwa na kusambazwa katika mikoa mbalimbali nchini ikilinganishwa na tani 332,000 kipindi cha mwezi Aprili, 2017. Kiasi hicho kilichoingizwa nisawa na asilimia 89.73ya wastani wa mahitaji ya tani 485,000 kwa mwaka.
 Kati ya kiasi hicho cha mbolea, tani 233,979.16 ziliagizwa kwa kutumia mfumo wa Ununuzi wa Pamoja, zikiwa ni tani 88,945za mbolea ya kupandia (DAP) na tani 145,034.16 ya kukuzia (UREA).
Mheshimiwa Spika,kwa kuzingatia mafanikio yaliyopatikana, Wizarakatika mwaka 2018/19 itaendelea kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Pamoja wa Mbolea (Bulk Procurment system-BPS),ambapo wafanyabiashara watakaopata zabuni za kuleta mbolea nchini wataingiza tani 300,000 za mbolea. Kati ya hizo, tayari tani 100,000 zimeagizwa na tani 32,000 zimepokelewa, hali inayotoa uhakika wa upatikanaji wa mbolea kwa wakati msimu wote ujao. Ili kuimarisha usambazaji, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka za Mikoa itahamasisha ushiriki wa sekta binafsi kujenga maghala makubwa kwa ajili ya kuhifadhi mbolea (strategic storage facilities) hasa katika maeneo yenye mahitaji makubwa. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia bei ili kuwalinda wakulima na kuongeza matumizi ya mbolea.
Upatikanaji wa Mbegu Bora na Viuatilifu
29.  Mheshimiwa Spika,msukumo pia umewekwa katika kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora na Viuatilifu nchini. Katika mwaka 2017/18 upatikanaji wa mbegu bora umefikia tani 51,700.51 ikilinganishwa na tani 28,278.2 za mwaka 2016/2017, ambapo tani 26,112.69 zilizalishwa nchini, tani 16,277.7 ziliagizwa kutoka nje na wafanyabiashara, na tani 9,310.12 zikiwa ni bakaa ya msimu wa 2016/17.Kati ya mbegu zilizozalishwa nchini, tani 18,500 ni za Pamba.
30.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2018/2019, Wizara itachangia upatikanaji wa tani 40,000 za mbegu bora mbalimbali; miche bora ya chai milioni 10 na miche bora ya kahawa milioni 12; kusambaza tani 8,600 na lita 9,800 za viuatilifu; na ekapaki 7,000,000 za viuatilifu vya zao la pamba.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na “Bill and Melinda Gates Foundation” itakamilisha Mfumo wa Taifa wa kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora. Mfumo huo utahusisha uboreshaji wa uzalishaji wa mbegu mama katika vituo vya utafiti; kuimarisha na kuboresha miundombinu ya mashamba yaASA yanayozalisha mbegu zilizothibitishwa; kujenga uwezo wa Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI); na kuboresha mfumo wa menejimenti ya upatikanaji, usambazaji na matumizi ya mbegu bora nchini.
31.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 kiuatilifu aina ya Sulphur pamoja na Vifungashio vya korosho (magunia) havitatolewa kwa njia ya ruzuku kama ilivyokuwa msimu wa Kilimo 2017/18. Wakulima watauziwa kwa bei ambayo itatangazwa na Bodi ya Korosho ili wakulima na wadau wa Korosho waweze kufahamu utaratibu wa kupata pembejeo hiyo pamoja na magunia kwa wakati na kwa bei itakayopitishwa. Aidha, Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na Vyama Vikuu vya Ushirika wa Korosho na Benki ya NMB imekamilisha mchakato wa uagizaji wa pembejeo za korosho ikiwemo kuingia mikataba na wazabuni ambao kwa ujumla wao wataleta salfa ya unga tani 35,000 na viuatilifu vya maji lita 520,000. Hadi leo tarehe 15.05.2018 kiasi cha tani 7,627 za salfa ya unga zimepokelewa nchini.  Kati ya hizi tani 1,328 tayari zimesambazwa kwa wakulima kupitia vyama vikuu vya ushirika na tani 6,299 zinasubiriwa kusambazwa. Na kiasi cha tani 37,873 zimeagizwa ambapo tani 17,500zinatarajiwa kufika nchini mwezi huu wa Mei.  Tani 20,373 zitawasili nchini kati ya mwezi Juni na Julai, na Serikali inasimamia upatikanaji wa magunia ya kuhifadhia Korosho kupitia makubaliano kati ya Vyama vya Ushirika, Benki na wazalishaji wa magunia.

2.2.3   Udhibiti wa Visumbufu vya Mimea na Mazao

Udhibiti wa visumbufu vya milipuko
32.  Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi April 2018, ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea walidhibitiwa  katika Wilaya 11 nchini ambapo jumla ya lita 2,425 kati ya 6,000 za kiuatilifu aina ya Fenthion 60% ULVzilitumika kuangamizandege milioni 61.7. Hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kufanya tathminiili kubaini kiwavijeshi vamizi (Fall armyworm) iliyofanyika katika Mikoa 6 sanjari na tathmini ya kubaini uwepo wa nzige wekundu katika mbuga za mazalio, hususan maeneo ya Ziwa Rukwa, Iku/Katavi, Malagarasi, Wembere na Bahi.
33.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara itaendelea kudhibiti visumbufu vya mazao na mimea kwa kufanya tathmini ili kudhibiti milipuko ya nzige, kweleakwelea, panya, viwavijeshi na magonjwa ya mimea. Hatua pia zitachukuliwa kuimarisha vituo vya ukaguzi vya mipakani na kituo cha kudhibiti milipuko cha Kilimo Anga. Vilevile, kupitia ASDP II Wizara itavijengea uwezo na kukarabati vituo 36 vya Afya ya Mimea na Vituo 8 vya Ukaguzi wa mazao mipakani.

2.2.4   Utafitina Utoaji wa Matokeo ya Utafiti kwa Wadau

34.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/18, Wizara kupitia Vituo vya Utafiti na kwa kushirikiana na Taasisi binafsi za kilimo imegundua na kuidhinisha mbegu bora mpya 25 (Kiambatisho Na.1.) Aidha, mbegu hizo zitaanza kuzalishwa na ASA na Makampuni binafsi nakusambazwa kwa wakulima.
35.  Mheshimiwa Spika, matokeo ya mbegu bora zilizogunduliwa na watafiti  na kusambazwa kwa wakulima wa korosho yameonesha kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 127,956 mwaka 2012/13 hadi tani 265,238 mwaka 2016/17 ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni bora za kilimo, udhibiti wa wadudu na magonjwa, pamoja na kuimarika kwa bei ya korosho.
36.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19, Wizara kupitia vituo vyake vya utafiti itaendelea kuwezesha kugundua, kutathmini na kusambaza teknolojia bora za kilimo. Aidha, mbegu bora mama na mbegu za awali tani 10 zikiwemo nafaka na mikunde zenye sifa mbalimbali zitazalishwa.
37.  Mheshimiwa Spika,Wizara kupitia Programu ya ASDP II itaboresha na kuimarisha miundombinu ya utafiti kwa kukarabati ofisi, maabara na nyumba katika vituo nane (8) vya utafiti, Kituo cha Taifa cha Utunzaji Nasaba za Mimea (National Plant Genetic Resource Centre) pamoja na ujenzi na uboreshaji wa Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI).
38.  Mheshimiwa Spika,Wizara itahakikisha kuwa matokeo ya utafiti yanawafikia wadau wa kilimo kwa njia ya mtandao, maonesho, mashamba ya mfano, taarifa na machapisho mbalimbali kama vile mabango, vipeperushi na vijarida. Aidha, itaratibu upatikanaji wa taarifa muhimu za utafiti kupitia majarida makubwa ya utafiti ulimwenguni kwa kushirikiana na Taasisi za Kimataifa ili kuongeza ubunifu wenye tija kwa maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.

2.2.5   Huduma za Ugani na Kusambaza Teknolojia za Kilimo

39.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Wizara imeendelea kupeleka teknolojia za kilimo kwa wakulima kwa kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya viuatilifu vya zao la pamba kwa wakulima viongozi na wengineo 15,230 katika Halmashauri 14 nchini.
40.  Mheshimiwa Spika, Wizaraya Kilimo kwa ushirikiano na TAMISEMI itaendelea kusimamia huduma za ugani na kuboresha usambazaji wa teknolojia za kilimo bora kwa wakulima kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo utoaji wa ushauri wa kitaalam na ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za ugani katika Halmashauri zote nchini. Aidha, kupitia ASDP II Wizara itaendelea kuviimarisha vituo saba (7) vya maonesho ya wakulima (NaneNane)na kujenga kituo kimoja kipya cha maonesho cha Kanda ya Ziwa Mashariki katika Mkoa wa Simiyu ili kupeleka teknolojia za kilimo kwa wakulima wengi zaidi.

2.2.6   Usimamizi wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani na upatikanaji wa masoko

41.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Wizara kwa kushirikiana na wadau kama vile FAO, ANSAF na HELVETAS imekamilisha Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa Mazao baada ya mavunounaolenga kupunguza upotevu wa mazao ya chakula,kuongeza upatikanaji wa masoko na kipato kwa mzalishaji.
42.  Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa andiko la Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (Tanzania Initiative for Preventing Aflatoxin Contamination – TANIPAC) ambao unalenga mazao ya mahindi na karanga na utatekelezwa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Tabora, Simiyu, Kigoma, Dodoma, Morogoro, Manyara, Ruvuma, Songwe na Mtwara.
43.  Mheshimiwa Spika, Wizara pia itatekeleza Mradi waTANIPAC ambapo itafanya usanifu wa ujenzi wa kituo cha mfano cha kusambaza teknolojia za usimamizi wa mazao baada ya kuvuna (Post-harvest Centre of Excellence), Maabara ya mfano (Central Agriculture Reference Laboratory for Aflatoxin and Fungal Testing) kwa ajili ya vipimo vya maambukizi ya sumukuvu na aina nyingine za ukungu mkoani Dodoma. Aidha, katika kuimarisha soko la ufuta, kuanzia msimu wa mavuno wa mwaka 2017/2018, zao laufuta litauzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala hususan katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Morogoro, Dodoma na Singida, na maandalizi yamekamilika.
44.  Mheshimiwa Spika, katikakudhibiti matumizi ya vipimo vya mazao visivyo rasmi, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji na wadau wengine, itasimamia na kuhamasisha matumizi ya mizani na vifungashio sahihi ili kumsaidia mkulima kupata mapato stahiki kutokana na mauzo ya mazao yake. Aidha, Serikali itasimamia utekelezaji wa Sheria ndogo ndogo ili kudhibiti matumizi ya vipimo visivyo rasmi na  inaelekeza kwa kadri inavyowezekana mazao yote yauzwe kwa uzito badala ya ujazo. Lumbesa ni tatizo la kujitakia, tukiuza kwa uzito tatizo hili litapungua sana au kuisha kabisa.

2.2.7   Kusimamia Uzalishaji Kupitia Bodi za Mazao

45.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Wizara imeendelea kusimamia uzalishaji wa mazao kupitia bodi zake. Uzalishaji kwa baadhi ya mazao makuu ya asili ya biashara umeongezeka  kwa viwango tofauti kama inavyoonekana katika Jedwali namba 1. Ongezeko hilo limechangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo matumizi ya teknolojia na mbinu bora za uzalishaji pamoja na ongezeko la bei ya mazao ya pamba, pareto, korosho, chai na tumbaku katika msimu uliopita,hali kadhalika Salfa iliyotolewa bure na Serikali kupitia fedha za export levy, ilisaidia kuongezeka kwa mavuno ya zao la korosho.

2.2.8   Uzalishaji wa mazao ya bustani na mbegu za mafuta

46.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, uzalishaji wa mazao ya bustani na viungo umeongezeka kwa viwango tofauti kama inavyoonekana katika Jedwali namba 2. Ongezeko hilo linatokana na wakulima kuhamasika kuzalisha mazao ya parachichi, matikiti na nyanya. Wizara imeendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali ili kuhamasisha kilimo cha mazao ya bustani na viungo pamoja na ulaji wake.

2.2.9   Mikakati ya uzalishaji wa mazao

47.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara itahakikisha kuwa Mpango wa bajeti unatekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele na miongozo ya Kitaifa ili kilimo kichangie kutoa malighafi za viwanda na kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Lengo letu ni kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati mwaka 2025. Mimi binafsi naamini kwa dhati kwamba endapo programu za kilimo zitatekelezwa kama tulivyojipanga, Tanzania itakuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo au kabla ya mwaka 2022. Inawezekana.
Wizara kupitia ASDP II itatekeleza mkakati wa maendeleo ya mazao ambao unaweka mfumo (framework) wa kuendeleza mazao ya kilimo kwa kushirikisha wadau mbalimbali na Wizara ikiwa na jukumu la uratibu wa utekelezaji.

2.2.10                Taasisi za Wizara

48.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Wizara kupitia Taasisi zake imeendelea kusimamia hifadhi ya chakula,kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu, uzalishaji wa mbegu bora na udhibiti wa ubora wa pembejeo za kilimo.
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula - NFRA
49.  Mheshimiwa Spika,katika kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula nchini, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulifanikiwa kununua tani 26,038.643 sawa na asilimia 143.2 ya lengo la tani 18,182.00 za mahindi.
50.  Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia NFRA inatekeleza Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafakakwa kujenga Maghala na Vihenge vya kisasa katika maeneo nane (8) ambayo ni Dodoma, Songea, Makambako, Mbozi, Sumbawanga, Mpanda, Shinyanga na Babati.Jiwe la msingi liliwekwa Dodoma tarehe 21 Aprili 2018 na ujenzi umekwisha anza, ambapo vihenge na maghala hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 250,000.Katika mwaka 2018/19, Wakala umepanga kununua jumla ya tani 28,200 za nafaka nakuendelea kutekeleza Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka unaolenga kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.
Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo - AGITF
51.  Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Februari, 2018 Wizara kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Trust Fund -AGITF) imetumia Shilingi 2,391,246,400kukopesha zana mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi kama inavyooneshwa katika Kiambatisho Na 2.
52.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara kupitia Mfuko huo imepanga kutoa mikopo ya zana mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi kama inavyooneshwa katika Kiambatisho Na 3.

Wakala wa Mbegu za Kilimo - ASA
53.  Mheshimiwa Spika, Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) umezalisha tani 784.155 za mbegu bora zikiwemo mbegu bora za nafaka, mikunde na mbegu za mafuta ambapo kati ya hizo tani 650.045 wameuziwa wakulima. Aidha, miche bora ya Kahawa 1,163,758 imezalishwa ambapo kati ya miche hiyo, 207,358 imezalishwa Lyamungo (Kilimanjaro), 132,900 Ugano (Ruvuma), 646,800 Maruku (Kagera), 71,000 Mwayaya (Kigoma), 100,000 Mbimba (Songwe) na 5,700 Tarime (Mara).
54.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2018/2019 Wizara kupitia ASA imepanga kuzalisha mbegu bora za nafaka na mikunde tani 1,800; kwa kushirikiana na Sekta binafsi itazalisha tani 1,500 za mbegu bora katika shamba la Mbozi;  vipando bora vya Muhogo pingili 7,000,000 katika mashamba ya Mwele na Msimba na miche bora ya matunda 50,000 katika mashamba ya Bugaga na Arusha.
Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania- TFRA
55.  Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TFRA imeendelea kudhibiti ubora wa mbolea nchini ambapo hadi mwezi Februari 2018, imesajili wafanyabiashara wa mbolea 430 na kufikia idadi ya wafanyabiashara wa mbolea 2,045 kwa nchi nzima; imetoa vibali 286 vya kuingiza mbolea nchini ambapo tani 310,673.703 zimeingizwa; imefanya ukaguzi wa maghala na maduka ya wafanyabiashara wa mbolea kwenye Mikoa 19 nchini.
56.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2018/2019, Wizara kupitiaTFRA itaimarisha Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa pamoja kwa kuhamasisha makampuni ya mbolea kuagiza mbolea kwa kiasi kikubwa katika kipindi ambacho bei ya mbolea kwa soko la dunia iko chini ili kuepuka ongezeko la bei katika soko la dunia. Aidha, TFRA itatoa elimu juu ya mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja kwa wasambazaji (agro – dealers) wa mbolea katika Mikoa na Halmashauri; kusajili wafanyabiashara wa mbolea; kukagua na kutoa vibali vya kuingiza mbolea nchini.
Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu - TOSCI
57.  Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TOSCI imekagua mashamba ya mbegu hekta 8,103.08 ambapo hekta 24.3 sawa na asilimia 0.3 hazikukidhi viwango vya ubora;imehakiki uhalisia, ubora na sifa za aina mpya 126 za mbegu kwa ajili ya usajili; imetoa vibali 860 vya kuingiza mbegu na vibali 11 vya kutoa mbegu nje ya nchi ambapo jumla ya tani 13,393 za mbegu zimeingizwa nchini.
58.  Mheshimiwa Spika, TOSCI imefungua kituo kipya cha udhibiti wa ubora wa mbegu katika Kanda ya Kusini chenye makao makuu yake Mtwara ili kurahisisha utoaji huduma katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Aidha, TOSCI itahakiki upya, uhalisia na sifa kwa aina 107 za mbegu mpya na kutoa lebo 15,000,000 kwa ajili ya kuweka kwenye mifuko ya kuuzia mbegu ili kukabiliana na tatizo la mbegu zisizo na ubora.

2.2.11                Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo

59.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Wizara imetoa ufadhili kwa wanafunzi 1,956 kwenye mafunzo ya kilimo ngazi ya Astashahada na Stashahada katika Vyuo 14 vya mafunzo ya kilimo. Vilevile, Wizara imedahili wanafunzi 246 wanaojilipia wenyewe ngazi ya Astashahada na Stashahada.
60.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2018/2019, Wizara itadahili wanafunzi 2,300 ngazi ya Astashahada na Stashahada  kwa ufadhili wa Serikali; itandaa mtaala wa Stashahada ya Matumizi Bora ya Ardhi katika mfumo wa moduli; itahuisha mtaala wa Stashahada ya mboga, maua na matunda; itakarabati miundombinu ya vyuo saba vya mafunzo ya kilimo na vituo vitano  vya mafunzo kwa wakulima.

2.2.12                Kuunda na kupitia Sera na Sheriaza Sekta ndogo ya

Mazao

61.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilifuta ada na tozo za mazao 78 kati ya 139 zilizokuwa hazina tija kwa wakulima. Kufuatia hatua hiyo, Wizara ilifanya marekebisho ya kanuni na sheria zilizoanzisha tozo na ada husika ili kuwezesha utekelezaji wa marekebisho hayo.
Serikali inasisitiza kuwa utekelezaji wa sheria na kanuni hizo uzingatiwe na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa wale wote watakaokiuka.
62.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara imechambua na kubaini ada na tozo 21ambazo bado ni kero kwa wakulima nchini na kuzifuta.Lengo ni kubakizaada na tozo ambazo zina mahusiano ya moja kwa moja na uendelezaji wa mazao husika kama vile uendelezaji wa utafiti wa mazao. Ada na tozo zilizofutwa ni 3 katika tasnia ya chai, 3 tasnia ya kahawa, 2 tasnia ya tumbaku na tozo mojamoja kwa tasnia za sukari na pamba. Aidha, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, Serikali imefuta tozo 5 kwenye uzalishaji wa mbegu. Vile vile, kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya ushirika nchini, tozo 6 katika ngazi mbali mbali za ushirika zimefutwa.
63.  Mheshimiwa Spika, Wizarapia imewasilisha Wizara ya Fedha na Mipango mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kodi na tozo kwa lengo la kuwekamazingira wezeshi ya uwekezaji na uendeshaji biashara katika shughuli za kilimo. Mapendekezo hayoyanalenga kutoa unafuu wa kodi katika vifungashio vya mazao na mbegu za mazao ya kilimo, mabomba ya kunyunyuzia madawa (Knapsack Sprayers), mashine na mitambo ya usindikaji wa mazao, miundombinu ya uzalishaji na hifadhi ya mazao ya bustani na kulinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani usio sawa wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Mpango wa Wizara ni kuhakikisha kero zote zinazokwamisha maendeleo ya tasnia ya mazao ya kilimo zinashughulikiwa.

2.2.13                Kuimarisha Uratibu, Ufuatiliaji na Tathmini ya Sekta

64.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Wizara imeandaa taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Kilimo (Annual Performance Report) kwa mwaka wa fedha 2016/2017;imeboresha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za Kilimo (Agriculture Routine Data System - ARDS); imeandaa mfumo wa kupima matokeo ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II Result Framework) pamoja na viashiria vyake.

2.2.14                Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini

mwaTanzania - SAGCOT

65.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Wizara imeendelea kuratibu uwekezaji kwenye ukanda wa SAGCOT. Hadi sasa jumla ya Dola milioni 500kati ya Dola bilioni 3.5 zilizopangwa kuwekezwa ifikapo mwaka 2030 zimewekezwa katika Kilimo kwenye ukanda huo. Kati ya uwekezaji huo, Dola bilioni 2.4 zitatokana na Sekta Binafsi. Aidha, wawekezaji wakubwa wameweza kuunganishwa na wakulima ili kuongeza tija, kipato, chakula na lishe kwenye kaya za wakulima wa soya, chai, viazi vitamu na mviringo, mpunga, mboga na matunda.
66.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2018/2019, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa kilimo itapanua uzoefu uliopatikana kutoka SAGCOT kuendeleza kilimo kwenye maeneo mengine nchini. Hivyo, Wizara inao mpango madhubuti wa kuendeleza kilimo kwenye Ukanda wa Ziwa hususan kujenga mabwawa yatakayotumika kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na Wabia wa Maendeleo na Wadau wengine wa Sekta ya Kilimo ili kufikia malengo ya Sekta.

2.2.15                Kuimarisha Masuala Mtambuka

Ushiriki waVijana katika Kilimo
67.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Wizara kwa kushirikiana na Farm Africa imetekeleza Mkakati wa Kuongeza Ushiriki wa Vijana Katika kilimo kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na uzalishaji wa mazao ya ufuta, mahindi, maharage, mpunga, uyoga na asali kwa vijana 96,365 kutoka mikoa mitano ambapo kati ya hao 56,805 ni wa kiume na 39,560 ni wa kike.
68.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Vijana Kushiriki katika Kilimo na Kuongeza ajira kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta, Wabia wa Maendeleo na Wadau Sekta ya kilimo.

Hifadhi ya Mazingirana Mabadiliko ya Tabianchi
69.  Mheshimiwa Spika,Katika kutekeleza Mpango wa Kilimo kinachohimili mabadiliko ya Tabianchi (Agriculture Climate Resilient Plan) wa mwaka 2014, Wizara kwa kushirikiana na Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA) inatekeleza mradi wa kujenga uwezo wa kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi kwa usalama wa chakula ambapo mashamba darasa mawili yameanzishwa katika wilaya za Kongwa na Uyui.

70.  Mheshimiwa Spika,Wizara kwa kushirikiana na wakulima kupitia Mradi wa Kuongeza Uzalishaji na Tija kwa zao la Mpunga (Expanded Rice Production Project – ERPP) imeandaa Mipango ya Usimamizi wa Mazingira na Jamii (Environmental and Social Management Plans - ESMPs) wa kutunza mazingira ya skimu za umwagiliaji za Kigugu, Mbogo-komtonga, Mvumi, Msolwa Ujamaa na Njage.


71.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2018/2019,Wizara itazijengea uwezo Halmashauri za Wilaya katika Mikoa ya Kagera, Mbeya, Iringa, Morogoro na Kilimanjaro wa kutambua umuhimu wa kujumuisha njia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika bajeti na mipango ya maendeleo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.

2.2.16                Kuendelea kutekeleza Mpango wa Serikali kuhamia

Dodoma

72.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2017/2018, Wizara imeendelea kutekeleza agizo la Serikali la kuhamia Dodoma katika awamu tatu, ambapo katika awamu hizo watumishi 316 waliokuwa Makao Makuu ya Wizara Dar es salaam wamehamia Makao Makuu Dodoma.
73.  Mheshimiwa Spika,katika mwaka 2018/2019, Wizara itaendelea kuhamisha watumishi wake kuja Makao Makuu Dodoma.

3.0      Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara Fungu 24 – Vyama vya Ushirika kwa Mwaka 2017/18 na Mpango kwa Mwaka 2018/19


3.1              Mapato na Matumizi ya Fedha katika Kipindi cha

mwaka 2017/18

74.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2017/18, Fungu 24 – Vyama vya Ushirika, lilitengewa jumla ya Shilingi 6,293,857,760 zikijumuisha Shilingi 2,413,888,760 za Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO). Kati ya fedha hizo, Shilingi 1,456,634,072ni kwa ajili ya matumizi mengineyo zikiwa ni Shilingi 942,577,072 za Tume na Shilingi 514,057,000 za COASCO. Jumla ya Shilingi 4,837,223,688 zilitengwa kwa ajili ya mishahara ambapo Shilingi 2,937,391,928 zilikuwa ni mishahara ya watumishi wa Tume na Shilingi 1,899,831,760 ni kwa ajili ya watumishi wa COASCO.

3.2              Fedha zilizotolewa katika Bajeti ya Kawaida

75.     Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi 2018, fedha za matumizi ya kawaida zilizopokelewa kutoka Hazina zilikuwa ni Shilingi 3,854,197,441.41 sawa na asilimia 61.24 ya kiasi kilichoidhinishwa.

3.3              Matumizi

76.        Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2018 jumla ya Shilingi 3,854,197,441.41,sawa na asilimia 100ya fedha zilizopokelewa kwa Fungu 24 zilikuwa zimetumika.

3.4               Utekelezaji Halisi wa Majukumu kwa Mwaka

2017/18 na Mwelekeo kwa Mwaka 2018/17

77.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara chini ya Fungu 24 imeendelea kutekeleza majukumu yaliyopangwa.Kwa muhtasari majukumu yaliyotekelezwa na mpango kwa mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:-

3.5              Ukaguzi na Uchunguzi

78.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Wizara kupitia Tume imekagua   vyama vya ushirika 2,896 sawa na asilimia 55.7 ya lengo la kukagua vyama 5,200. Aidha, Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limekagua vyama vya ushirika 1,520 sawa na asilimia 18.91 ya lengo la kukagua vyama 8,040.
79.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara itaendelea kuiwezesha COASCO kufanya ukaguzi katika Vyama vya Ushirika 8,040. Aidha, Wizara kupitia Tume itakagua Vyama Vikuu vya Ushirika 47, Miradi ya Pamoja na 34, Vyama vya Ushirika vya Msingi 10,909 nchini.

3.6              Usimamizi wa Chaguzi za Viongozi wa Bodi za

Vyama

80.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Wizara kupitia Tume imesimamia chaguzi za viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Miradi ya Pamoja 12 sawa na asilimia 26.7 ya lengo la kusimamia vyama 45. Aidha, Wizara kwa kushirikana na Mamlaka za Serikali za Mitaa imeratibu na kusimamia chaguzi za vyama vya msingi 5,599 sawa na asilimia 93.3 ya lengo la kusimamia chaguzi za vyama 6,000.
81.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa itaratibu na kusimamia chaguzi za Vyama Vikuu na Miradi ya Pamoja 36 na vyama vya ushirika vya msingi 5,000 nchini.

3.7              Uhamasishaji kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa

na Wadau wengine

82.        Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2017/2018, Wizara imeendelea kuhamasisha umma hususan vijana, wanawake na vikundi kujiunga au kuanzisha Vyama vya Ushirika. Kufuatia uhamasishaji huo, vyama vya Ushirika vipya 394 vilianzishwa na kusajiliwa.Wizara pia kwa kushirikiana na Wadau wa ushirika nchini imeratibu na kuwezesha kufanyika kwa majukwaa ya ushirika kwa mikoa 23 nchini na lengo ni kuongeza idadi ya wanachama wa vyama vya ushirika kufikia 7,000,000 ifikapo Juni 2019.
83.        Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imehamasisha wanachama 9,188 wa Vyama Vikuu vya Mikoa ya Lindi na Mtwara kujiunga na fao la Bima ya Afya lijulikanalo kama Ushirika Afya.

3.8       Kujenga uwezo wa Tume katika kutoa Huduma kwa

     Wadau

84.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Wizara imekamilisha uteuzi wa Mwenyekiti na Makamishna 10 wa Tume; imeendelea kuboresha ofisi zake mikoani na taratibu za maandalizi ya ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu zipo katika hatua ya kukamilisha malipo ya ununuzi wa kiwanja.

4.0            HITIMISHO NA SHUKRANI

4.1            Hitimisho

85.     Mheshimiwa Spika, licha ya ukweli kwamba sekta ya kilimo ni muhimu kwa maisha na ustawi wa uchumi kwa watu wengi hapa nchini; bado mchango wa sekta hii katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii hausadifu fursa kubwa tuliyonayo kama nchi. Kwa kiasi kikubwa hali hii inachangiwa na mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu, hususan kuwa na mawazo mgando kuhusu uendeshaji wa kilimo na mapokeo ya maumbile asili ya dunia.
86.     Mheshimiwa Spika, tumedhamiria kuondokana na mgando huu kwa kufanya mageuzi makubwa katika uendeshaji wa shughuli za kilimo kupitiaASDP-II na Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.Wizara imebaini maeneo manne ya kuongoza mageuzi hayoambayo ni pamoja na:


(i)   Kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo;
(ii)  Kusimamia kikamilifu hifadhi na matumizi jadidifu ya maji, ardhi na mazingira, sambamba na kuongeza miundombinu ya umwagiliaji;
(iii)  Kuweka msukumo katika mabadiliko ya fikra na mazingira ya kibiashara kwa sekta ya kilimo; na
(iv)  Kuweka mfumo mpya wa usimamizi wa kilimo kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa uendeshaji kilimo.
87.  Mheshimiwa Spika,dhamira hii ya Serikali ni endelevu na ya kweli na ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuanza utekelezaji wa hatua hii ya mageuzi kwa kuelekeza kuondoa kero na vikwazo walivyowekewa wakulima kwa miaka mingi. Nawaomba waheshimiwa Wabunge waniunge mkono katika mageuzi haya. Natambua ugumu uliopo hasa pale tunapogusa maslahi ya waliokuwa wananufaika na mifumo ya zamani. Mwanzo ni mgumu na wajibu wetu kama viongozi ni kutotetereka na kubaki tumejielekeza katika malengo ya tunayojiwekea.

4.2            Shukrani

88.  Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuzishukuru Nchi na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa ambayo yamesaidia sana Wizara katika juhudi za kuendeleza kilimo. Kwanza napenda kuzishukuru nchi za Japan, Marekani, Uingereza, Ireland, Malaysia, China, Indonesia, Korea ya Kusini, India, Misri, Israel, Ubelgiji, Ujerumani, Finland, Norway, Brazil, Uholanzi, Vietnam na Poland. Nayashukuru pia Mashirika na Taasisi za Kimataifazifuatazo:-
 Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, AU, IFAD, DFID, UNDP, FAO, JICA, EU, UNICEF, WFP, CIMMYT, ICRISAT, ASARECA, USAID, KOICA, ICRAF, IITA, IRRI, ILRI, CABI, CFC, AVRDC, AGRA, CIP, UNEP, WARDA, Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (DLCO-EA), HELVETAS,  Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu (IRLCO-CSA), Bill and Melinda Gates Foundation, Gatsby Trust, Rockfeller Foundation, Aga Khan Foundation, Unileverna Asasi zisizo za kiserikali nyingi ambazo hatuwezi kuzitaja zote hapa. Ushirikiano na misaada ya nchi na mashirika hayo bado tunauhitaji ili tuweze kubadili kilimo nchini.
89.  Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za pekee, kwa wakulima wa nchi hii kwa kazi kubwa wanayofanya katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb); Katibu Mkuu Mhandisi Mathew John Mtigumwe; Naibu Katibu Mkuu Dkt. Thomas Didimu Kashilila; Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa Vitengo; Taasisi na Asasi zilizo chini ya Wizara; watumishi wote wa Wizara; na wadau mbalimbali wa Sekta ya Kilimo kwa juhudi, ushirikiano na ushauri uliowezesha kutekelezwa kwa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2017/2018 kama nilivyofafanua katika hotuba hii. Ni matarajio yangu kwamba, nitaendelea kupata ushirikiano wao katika mwaka 2018/2019. Mwisho natoa shukrani kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha kitabu cha hotuba ya bajeti ya mwaka 2018/2019.

5.0 MAOMBI YA FEDHA MWAKA 2018/2019

90.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/19 Wizara inaomba idhini ya kukusanya maduhuli ya jumla ya shilingi 2,315,010,000. Maduhuli hayo yanatokana na faini mbalimbali na ada ya cheti cha afya ya mimea katika uingizaji wa mazao ya kilimo nchini na usafirishaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi.
91.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2018/2019, Wizara ya Kilimo inaomba jumla ya Shilingi 170,273,058,000 kupitia fungu 43 na fungu 24 kama ifuatavyo;


FUNGU 43
92.  Mheshimiwa Spika,jumla ya Shilingi162,224,814,000 zinaombwa kupitia Fungu 43. Kati ya fedha hizo, Shilingi98,119,516,000 ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo na Shilingi64,105,298,000ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapoShilingi28,560,428,000ni kwa ajili ya Mishahara ya Wizara, Shilingi14,346,253,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Bodi na Taasisi, Shilingi 12,727,150,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara na Shilingi8,471,467,000nikwa ajili ya Matumizi ya Kawaida kwa Bodi na Taasisi.

FUNGU 24
93.  Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi8,048,244,000zinaombwakwa ajili ya matumizi ya kawaidakupitia Fungu 24. Kati ya fedha hizo, Shilingi 2,199,700,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC), Shilingi 4,013,370,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Tume na Shilingi 1,835,174,000 ni kwa ajili ya Mishahara ya Taasisi
94.  Mheshimiwa Spika,NAOMBA KUTOA HOJA