Thursday, June 28, 2018

DKT TIZEBA AZINDUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA WIZARA YA KILIMO JIJINI DODOMA


Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati akifungua mkutano na kuzindua Baraza la wafanyakazi wa wizara ya kilimo kwenye ukumbi Wa Wakala Wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) Mjini Dodoma, Leo 28 Juni 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, WK)
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba (Kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe (Katikati) na Katibu wa Baraza la wafanyakazi Wizara ya kilimo Bi Agnes Hugo wakiimba wimbo wa mshikamano wakati wa ufunguzi wa mkutano na uzinduzi wa Baraza la wafanyakazi wa wizara ya kilimo kwenye ukumbi Wa Wakala Wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) Mjini Dodoma, Leo 28 Juni 2018.
Katibu Mkuu wa wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano na kuzindua Baraza la wafanyakazi wa wizara ya kilimo kwenye ukumbi Wa Wakala Wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) Mjini Dodoma, Leo 28 Juni 2018.
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano na kuzindua Baraza la wafanyakazi wa wizara ya kilimo kwenye ukumbi Wa Wakala Wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) Mjini Dodoma, Leo 28 Juni 2018.
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano na kuzindua Baraza la wafanyakazi wa wizara ya kilimo kwenye ukumbi Wa Wakala Wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) Mjini Dodoma, Leo 28 Juni 2018.

Na Mathias Canal, WK-Dodoma

Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba leo 28 Juni 2018 amefungua mkutano na kuzindua Baraza la wafanyakazi wa wizara ya kilimo, mkutano utakaotuama kwa siku mbili kuanzia leo mpaka kesho 29 Juni 2018 katika ukumbi wa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma.

Akizungumza katika mkutano huo Dkt Tizeba aliwasisitiza wajumbe wa baraza hilo kwa umoja wao kujadili kwa muktadha wa kutatua changamoto na kuboresha sekta ya kilimo kupitia mada mbalimbali zitakazowasilishwa ikiwa ni pamoja na kuhusu elimu ya majukumu ya wajumbe wa Baraza la wafanyakazi, Elimu juu ya watumishi wa Umma na hoja kutoka vyama vya wafanyakazi sambamba na wajumbe kupitishwa katika bajeti ya wizara kwa mwaka 2018/2019.

Alisema kuwa Baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu ambacho kimepewa nguvu kisheria ili kuwapa watumishi nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusu utendaji na ufanisi wa Taasisi ili kuongeza tija mahali pa kazi hivyo wajumbe hao wanapaswa kujadili mada hizo kwa ufanisi na tija.

Alisisitiza kuwa Baraza hilo linapaswa kuzaa matokeo mazuri ikiwemo uboreshaji wa mazingira ya kazi huku akisema kuwa serikali imekuwa ikisisitiza kila taasisi ya umma kuunda mabaraza ya wafanyakazi ili kuongeza ufanisi na tija katika mchango wa mapinduzi ya uchumi wa viwanda.

Alisema, serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli inatambua ushirikiano wa pande hizo mbili katika maamuzi hivyo ni vigumu kutekeleza majukumu endapo pande moja haitashirikishwa kwani umuhimu huo umetiliwa mkazo na kupitia sera, sheria na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa taasisi za umma.

Katika hatua nyingine Mhe tizeba aliwakumbusha wajumbe hao kuwa miongoni mwa majukumu muhimu ya sekta ya kilimo ni pamoja na kutambua kuwa katika maendeleo ya nchi asilimi 66.5 ya watanzania wanategemea sekta ya kilimo pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula nchini hivyo ni vyema katika mkutano huo kujadili mada hizo na kuwa na mategemeo ya kuwanufaisha zaidi wakulima kote nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akizungumza kabla ya kumkaribisha waziri wa kalimo kufungua kikao hicho cha Baraza la wafanyakazi alisema kuwa Baraza hilo jipya limeundwa kufuatia Baraza la awali kufikia muda wa ukomo wake baada ya maridhiano baina ya Menejimenti ya wizara ya kilimo na vyama vya wafanyakazi vya TUGHE na RAAWU kufikiwa.

Mhandisi Mtigumwe aliongeza kuwa Mkutano wa Baraza la wafanyakazi ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya ajira na mahusiano kazini Na 6 ya mwaka 2004 na sheria ya majadiliano ya pamoja katika utumishi wa umma Na 19 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2005. Ambapo kwa mujibu wa sheria hizo lengo la kuanzishwa mabaraza ya wafanyakazi ni kuwa na chombo cha ushauri na majadiliano ya pamoja kati ya wafanyakazi na waajiri ili kuwa na ushirikishwaji mpana wa wafanyakazi mahala pa kazi.

Alisema, kufuatia mabadiliko ya muundo wa Wizara ya kilimo hususani baada ya idara ya utafiti kuwa Taasisi inayojitegemea imelazimu muundo wa Baraza hilo kufanyiwa mabadiliko na kupelekea kupungua kwa idadi ya wajumbe kutoka 98 hadi kufikia 57, Aidha, mkataba mpya wa kuunda Baraza la wafanyakazi umezingatia mabadiliko hayo.

MWISHO.
Reply, Reply All or Forward

Tuesday, June 26, 2018

WIZARA YA KILIMO YANG'ARA TUZO ZA UTEKELEZAJI WA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI 2017/2018


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba Tuzo ya Uwezeshaji Kiuchumi, baada ya Wizara ya kilimo kuibuka mshindi wa pili katika kundi la Wizara, Wakala na Idara za Serikali kwenye  Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofunguliwa na Waziri Mkuu katika ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma Juni 18, 2018. (Picha Na Mathias Canal Wizara ya Kilimo)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha Taarifa ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mei 2017 Mpaka Mei 2018  baada ya kuizindua katika Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika kwenye ukumbi wa LAPF jijini Dodoma Juni 18, 2018. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Dkt. John Jingu.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua Kongamano hilo kwenye ukumbi wa LAPF jijini Dodoma Juni 18, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadhi ya viongozi walioshiriki katika Ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi wakipiga makofi baada ya Waziri Mkuu kufungua Kongamano hilo kwenye ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma Juni 18, 2018. kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu  Profesa, Faustine Kamuzora, Meya wa jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Anthony Mtaka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi  Dkt. John Jingu, Mkuu wa mkoa wa Dodoma,  Dkt. Binilith Mahenge na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng'i Issa.

Na Mathias Canal-WK, Dodoma 

Wizara ya kilimo imeipuka Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa wizara iliyoshika nafasi ya pili kama wizara iliyofanya vizuri dhidi ya taasisi nyingine za serikali zikiwemo wizara katika utekelezaji wa shughuli na programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuongeza ujuzi na kuimarisha uratibu wa shughuli za uwezeshaji katika kipindi cha mwaka 2017/2018.

Kwa niaba ya wizara ya kilimo tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba ambaye amesema kuwa wizara yake ilistahili kushika nafasi ya kwanza kwani imefanya majukumu makubwa kupitia nafasi yake ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Tuzo hiyo dhidi ya Wizara zilizofanya vizuri, Taasisi za serikali, na wajasiriamali zimetolewa leo (Jumatatu, Juni 18, 2018) na waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa  wakati akifungua Kongamano la Tatu la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa LAPF, Jijini Dodoma.
Katika hafla hiyo WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema taarifa ya Kongamano la Uchumi la Dunia la mwaka 2018 inaonesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na uchumi jumuishi miongoni mwa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Amesema hali hiyo, imetokana na Tanzania kufungua fursa za ujasiriamali ambapo kuna zaidi ya biashara milioni tatu zinazokuwepo kila mwaka, lengo la nchi ni kuhakikisha kuwa uchumi unakua na unamgusa kila Mtanzania hususan mwananchi wa kawaida. 
Waziri Mkuu ameongeza kwamba Serikali inaamini kuwa uchumi wa viwanda ukiimarika uchumi utakuwa kwa kasi kubwa na matokeo yake yataonekana wazi kwa kupanua wigo wa ajira, soko la huduma na shughuli nyingine za kiuchumi. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema suala la uchumi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ni moja ya ajenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo amezitaka sekta zote zihakikishe zinatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa viwanda.

Wakala wa barabara nchini ndio umeongoza kwa kushika nafasi ya kwanza iliyofanya vizuri dhidi ya taasisi nyingine za serikali huku vigezi vilivyotumika kuwapata washindi ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira wezeshi kwa watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa mabadiliko ya sera, sheria, kutengeneza kanuni, mikataba, kujenga uwezo n.k

Kongamano hilo lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba, Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Bw. Suleiman Jafo.

Wengine ni Wakuu wa Mikoa mbalimbali, Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Wilaya ya Mkoa wa Dodoma, Makatibu Tawala wa Mikoa, Mwenyekiti na Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,Wakurugenzi wa Halmashauri za Mamlaka za Serikali za Mitaa,

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bibi Beng’ Issa, wadhamini wa Kongamano hilo na Wawakilishi kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na Sekta binafsi.

MWISHO.

Wednesday, June 20, 2018

DKT TIZEBA AZINDUA AINA MPYA 9 ZA MBEGU BORA ZA MAHARAGE


 

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba (Mb) akitembelea shamba la maonyesho na uzalishaji mbegu kabla ya kuzindua aina mpya Tisa za mbegu bora za maharage katika hafla iliyofanyika kwenye eneo la Taasisi ya utafiti wa Kilimo na Maendeleo Kanda ya Kaskazini (Selian) Mkoani Arusha, Leo 20 Juni 2018.


Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba akikata utepe ishara ya uzinduzi wa aina mpya Tisa za mbegu bora za maharage katika hafla iliyofanyika kwenye eneo la Taasisi ya utafiti wa Kilimo na Maendeleo Kanda ya Kaskazini (Selian) Mkoani Arusha, Leo 20 Juni 2018. Sherehe hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya kilimo, Mifugo na Maji Mhe Mahmoud Mgimwa (Mb)

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba leo 20 Juni 2018 amezindua aina mpya Tisa za mbegu bora za maharage katika hafla iliyofanyika kwenye eneo la Taasisi ya utafiti wa Kilimo na Maendeleo Kanda ya Kaskazini (Selian) Mkoani Arusha.

Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe Tizeba ameitaja Wizara ya Kilimo kupitia taasisi za utafiti wa Kilimo Selian, Uyole na Maruku zikishirikiana na taasisi ya kimataifa PABRA/CIAT ndizo zimegundua mbegu bora hizo tisa za maharage zenye kuongeza uzalishaji na pato la mkulima.

Alisema kuwa kati ya hizo aina tisa za  mbegu za maharage, aina mbili zina viwango vya juu vya Madini muhimu ya Zinki na chuma yatakayosaidia kuongeza damu mwilini hasa kwa watoto, mama wajawazito na wazee, ambapo aina nne ni maharage ya muda mfupi yenye kustahimili ukame hivyo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi huku akizitaja aina zingine tatu kuwa ni kwa ajili ya usindikaji.

Alisema kuwa aina hizi Tatu za usindikaji zitawasaidia walaji kuokoa muda wa maandalizi pia itafungua fursa ya uanzishwaji wa viwanda vya usindikaji hivyo kuongeza ajira na kipato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Mbegu hizi zitakuwa mkombozi mkubwa katika kuboresha lishe kwenye jamii, kwani tatizo la upungufu wa damu ni tishio kwa watoto na kina mama wajawazito, Aidha ugunduzi juu utachangia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani kati ya aina zilizogunduliwa kuna zinazokomaa kwa muda mfupi wa kuanzia siku 72" Alikaririwa Dkt Tizeba

Mhe. Dkt Tizeba alisisitiza kuwa maharage ni zao muhimu kwa chakula nchini Tanzania na ni zao la pili kwa umuhimu baada ya mahindi hivyo linapaswa kulimwa kwa muktadha wa kibiashara sio kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia pekee ambapo pia, alisema kuwa inapaswa kuwekwa juhudi mahususi katika kusambaza aina hizo mpya za mbegu.

Katika hatua nyingine, Mhe Dkt. Tizeba amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa Kilimo na Maendeleo Kanda ya kaskazini Ndg Ramadhan Ngatoluwa kukaa upya na watafiti hao ili kuwa na majina mapya yatakayotambua kazi kubwa iliyofanywa na watafiti hao.

Monday, June 11, 2018

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakulima wa pamba katika kijiji cha Msai wilaya ya Iramba  akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Singida kutembelea vituo na kujionea ununuzi wa pamba, 
Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wakulima wa pamba katika kijiji cha Msai wilaya ya Iramba  akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Singida kutembelea vituo na kujionea ununuzi wa pamba, Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe Emmanuely Lwehahula.
Kituo cha ukusanyaji na ununuzi wa pamba katika kijiji na Kata ya Msai, Wilayani Iramba

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe Emmanuely Lwehahula akitoa salamu za shukrani kwa Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba kwa kufanya ziara ya kuwatembelea  wakulima wa pamba katika kijiji cha Msai wilaya ya Iramba akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Singida kutembelea vituo na kujionea ununuzi wa pamba, 


Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba amemuagiza Mrakibu wa polisi Wilaya ya Iramba ASP Magoma Mtani kumkamata aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha ushirika (AMKOS) Msai.

Waziri Tizeba ametoa agizo hilo jana 9 June 2018 Mara baada ya kutembelea kitongoji cha Kati, Msai na Mtoa akiwa katika ziara ya kikazi ya Siku mbili kwa ajili ya kutembelea vituo vya ununuzi wa pamba na kujionea msimu wa ununuzi wa zao hilo katika vijiji hivyo.

Dkt Tizeba amelaani vikali ufujaji huo wa fedha za wakulima huku akimtaja Paul Ramadhan Kurwa kuhusika na ufujaji huo wa shilingi milioni 23 huku akiendelea kuonekana mtaani pasina kuchukuliwa hatua za kisheria.

"Wakati muelekeo wa serikali yetu inayoongozwa na Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli ukijipambanua kutaka kuboresha maisha ya watanzania kupitia Kilimo lakini kuna watu wanataka kurudisha nyuma juhudi hizo, hakika tutawapa kibano kweli kweli hakuna utani kwenye fedha za wananchi" Alikaririwa Dkt Tizeba

Mhe Tizeba ametoa siku moja kukamatwa kwa mwizi huyo na kufikishwa mahakamani ili awe mfano kwa wezi wengine wasio kuwa na haya wala soni.

Aidha, amewataka wananchi katika msimu huu wa uuzaji na ununuzi wa Pamba kutouza Pamba zenye uchafu wakidhani wataongeza idadi ya kilo kwani kufanya hivyo ni kufifihisha juhudi zao wenyewe jambo ambalo halina tija.

Sambamba na hayo pia amewaondoa hofu wakulima kote nchini kuwa serikali ya awamu ya tano inatekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi yenye mkataba na wananchi katika kipindi cha miaka mitano 2015-2020.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe Emmanuely Lwehahula amempongeza Waziri Tizeba kwa kutembelea maeneo mbalimbali ili kujionea ununuzi wa Pamba huku akiwasihi wananchi wilayani humo kulima kiasi kikubwa cha Pamba msimu ujao kwani mbegu na madawa ya kuulia wadudu vitatolewa bure kuanzia msimu ujao wa mwaka 2018/2019.

MWISHO.
br />
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akizungumza kwenye kikao kazi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida. 
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu (Kushoto) na Mkuu wa Wilya ya Singida Mhe Elias Tarimo wakifatilia kikao cha kazi kilichoongozwa na waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba, Juzi 8 Juni 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza jambo mbele ya waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba alipotembelea ofisi ya Mkoa akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Juzi 8 Juni 2018.
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akizungumza kwenye kikao kazi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida. Juzi 9 Juni 2018.
Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Singida na tayari amewasili mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ya siku moja hapo kesho 10 Juni 2018.

Akiwa Mkoani Singida Mhe Dkt. Tizeba ametembelea vituo mbalimbali vya ukusanyaji wa pamba na kujionea msimu wa ununuzi wa pamba katika Wilaya ya Ikungi na Iramba.

Miongoni mwa mambo ya msisitizo katika maeneo yote hayo ni pamoja na kuwashauri wakulima kutouza pamba chafu kwa kudhani kuwa watapata kilo nyingi kwani jambo hilo linafifihisha soko la zao hilo kwa wanunuzi.

Katika hatua nyingine ametoa onyo kwa viongozi wa vyama vya ushirika AMKOS kutojihusisha na ubadhilifu wa fedha za wakulima huku akielekeza kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa wale wote waliobainika kuiba fedha za wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, ametangaza neema kwa wakulima wa pamba kote nchini kuwa msimu ujao wa kilimo wa mwaka 2018/2019 wakulima watapatiwa mbegu na dawa bure pasina malipo.

Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Tizeba amewasisitiza watendaji wote mkoani humo kutoa ushirikiano mahususi kwa wakulima ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la pamba na mazao mengine yakiwemo mahindi, mtama, alizeti N.k

Zao la pamba ni miongoni mwa mazao ya biashara yanayolimwa katika mkoa wa Singida, Katika msimu huu wa mwaka 2017/2018, mkoa ulipokea mbegu bora za pamba aina ya UKM 08 tani 381.48 na kusambazwa kwa wakulima ambapo jumla ya ekari 35,889 zilipandwa. Aidha, sumu chupa 137,970 zimesambazwa kwa wakulima na mabomba ya kunyunyizia sumu 365 yamesambazwa pia.

Pia amesisitiza kuwa uongozi wa mkoa huo unapaswa kujipanga kikamilifu kusimamia ununuzi wa pamba kupitia utaratibu uliowekwa wa kuvitumia Vyama vya Ushirika vya Kilimo na Masoko (AMCOS) pamoja Vyama vya Awali vya Ushirika  (Pre Cooperative Societies).

Katika mkoa huo jumla ya AMCOS 36 na “Pre Cooperatives” 20 zitahusika katika ununuzi wa zao la pamba katika msimu huu wa kilimo wa mwaka 2017/2018.

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt Rehema Nchimbi alisema kuwa mkoa huo ulikuwa na matarajio ya awali ya mavuno kwa tani 21,533.4 ambapo matarajio haya yameshuka mpaka kufikia tani 14,015.2 zinazotarajiwa kuvunwa kutokana na athari za wadudu waharibifu.

Alisema jumla ya vituo vitakavyotumika kukusanya na kununua pamba ni 117 ambavyo vimesambaa katika maeneo yote yanayolima pamba yaliyopo katika Halmashauri saba za Mkoa huo.

Aliongeza kuwa maghala yatakayotumika kununulia pamba katika vituo hivyo  yamesafishwa na kufukiziwa sumu ya kuuwa wadudu. Kampuni iliyoruhusiwa kununua pamba katika Mkoa huo ni BioSustain (T) LTD ambayo ni mdau mkubwa wa kilimo cha zao la pamba katika mkoa wa Singida kwani imewekeza kiwanda cha kuchambua pamba kilichopo Manispaa ya Singida.

MWISHO.
Reply, Reply All or Forward Wazo Huru wazohuru14@gmail.com

Saturday, June 9, 2018

Rais Mhe Dkt. John Pombe Magufuli azindua rasmi program ya ASDP II

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli leo emezindua rasmi programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) hafla ambayo imefanyika katika jengo la Mikutano la kimataifa la Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam, na kuhudhuriwa na makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dara es salaam Mhe Paul Makonda, Mawaziri wa sekta za kilimo pamoja viongozi wa dini na wadau wote wa sekta ya hiyo. Akhutubia katika mkutano huo Rais amezitaka sekta za kilimo ,Sekta binafsi na Asasi za kiraia kujumuika pamoja katika kutelekeza mpango huu wa ASDP II ili kuongeza tija katika sekta za Kilimo,Mifugo,Uvuvi na Viwanda. Hata hivyo Mhe.Rais ameiagiza wizara ya kilimo pamoja na wadau wengine wa kilimo kushughulikia kikamilifu changamoto zote zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa programu hiyo ya awamu ya Kwanza. Aidha ameongeza kuwa sekta ya kilimo inanafasi kubwa ya kubadilisha hali ya uchumi wa nchi kuliko sekta za madini na gesi hivyo kilimo kiboreshwe ili kiweze kuleta mapinduzi katika sekta nyingine. alisistiza Mhe.Rais Katika hatua nyingine Mhe. Rais ameitaka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) kusimamia malengo ya kuanzishwa kwake ili iweze kutoa msaada kwa wakulima ikiwemo kuwakopesha badala ya kufanya biashara baina ya benki na kuwakopesha wafanyakazi wake jambo ambalo ni kinyume na utaratibu. Awali waziri wa kilimo Mhe. Dkt.Charles Tizeba amesema kwamba Makadirio ya mahitaji ya rasilimali (Bajeti) kwa ajili ya utekelezaji wa program hiyo ni shilingi Trilioni 13 ambazo zitahitajika kutekeleza mpango huo kwa kipindi cha miaka 5 ya mwanzo. “tayari kwa mwaka ujao wa fedha wa 2018/19, Serikali unayoiongoza inatarajia kuchangia kiasi cha Shilingi Bilioni 943 kupitia Wizara za Sekta ya Kilimo ambazo ni Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji. Aidha Halmashauri zote za Wilaya kupitia makusanyo yake ya ndani (own sources) zinatarajia kuchangia kiasi cha Shilingi bilioni 36”. Alisisitiza Dkt Tizeba