Wednesday, April 10, 2019


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Nyasebwa Chimangu akitoa neon fupi la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Waziri WIzara ya Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa kwenye kwenye Mkutano wa Wadau wa Pembejeo Jijini Dodoma katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi


Mgeni Rasmi wa Mkutano huo wa Wadau wa Pembejeo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Innocent Bashungwa akiwahutubia Wadau wa Pembejeo kutoka Taasisi mbalimbali za Wizara ya Kilimo pamoja na Washiriki wengine kutoka Sekta Binafsi pamoja na Wasambaji na Wauzaji wa Pembejeo za Kilimo kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Bora (TOSCI) Bwana Patrick NgwediagiSehemu ya Washiriki Mkutano huo wa Wadau wa Pembejeo wakimsikiliza Mgeni Rasmi, Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Mhe. Innocent Bashungwa katika ukumbi wa Bwalo la Polisi Jijini Dodoma

Nyang’anyeni Leseni za Wauzaji wa Pembejeo ‘Feki’ – Naibu Waziri Bashungwa


Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa amewaelekeza Wadau wote kwenye mnyororo wa pembejeo kuwa sasa ni wakati wa kusimamia ipasavyo Sheria zote zinazohusu tasnia ya pembejeo kuanzia viutatilifu, mbegu pamoja na mbolea ili kumsaidia Mkulima mnyonge wa Tanzania.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo tarehe 9/4/2019 wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Pembejeo za kilimo ambapo Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Bora (TOSCI) imeandaa mkutano kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI) kwa lengo la kufanya tathmini ya maboresho ya mambo kadhaa yenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hizo kwa pamoja.

Naibu Waziri Bashungwa amesema Mkulima wa Tanzania amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi wakati wa kuendesha kilimo chake na kuongeza kuwa changamoto hizo ni pamoja na viuatilifu ‘feki’, mbegu hafifu na ‘feki’ pamoja na mbolea ‘feki’ sasa zinapaswa kuisha kwa kuwa Taasisi zote zimepewa mamlaka ya kumkamata na kumfungulia mashitaka muuzaji yeyote atakaye kutwa akiuza au kusambaza pembejeo ‘feki’ na kuongeza kuwa amekuwa akishangazwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa jambo hilo.

“Ndugu zangu Wataalam nimekuwa nikisikia na kuona idadi ndogo ya Wasambazaji na Wauzaji wa pembejeo feki wanaokamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, tofauti na idadi kubwa ya malalamiko ya Wakulima wetu, sasa iwe mwisho, Wasambazaji na Wauzaji wanafahamika, simamieni sheria, wakamatwe na wafikisheni kwenye vyombo vya sheria na wanapopatikana na hatia, wafungwe kwa mujibu wa sheria.” Amekaririwa Waziri Bashungwa.

“Si sawa Wasambazaji feki wa pembejeo kuendelea na mchezo huu, huu ni wakati wa kuwadhibiti na kuwafunga, kwa sababu sheria zipo na zinasema wazi wazi, adhabu ya Mtu anayefanya kosa hilo” Amekaririwa Mhe. Bashungwa.

Naibu Waziri Bashungwa ameagiza kuwa mbali na mambo mbalimbali watakayojadiliana katika mkutano huo msisitizo lazima uwekwe kwenye kutafu njia bora ya kuongeza ufanisi na kuondoa changamoto kwenye upatikanaji na utoaji wa huduma ya usambazaji wa pembejeo bora kwa Wakulima na kama kuna vikwazo vyovyote mkutano huo utoe mapendekezo kwa Wizara nini kifanyike.

Napenda mjikite katika kujadiliana  ili kuibua vikwazo vyote ambavyo mnaona kama vitaboreshwa basi vitasaidia usambazaji wa pembejeo zote kufika kwa Mkulima katika hali ya ubora ili Sekta ya Kilimo iwe na uzalishaji mkubwa na wenye tija kwenye mazao ya Kimkakati, mazao ya chakula na mazao yenye thamani kubwa.

“Naomba mtuambie kama kuna Sheria au Kanuni ambazo haziendi sambamba na mahitaji ya nyakati na zimekuwa kikwazo, ili huduma ya kufikishia Mkulima Viuatilifu sahihi, mbegu bora mtuambie na kutushauri, njia zipi zitakuwa sahihi katika kufikisha maarifa mapya kwa Wakulima kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji” Amekaririwa Mhe. Bashungwa.

Mkutano huo wa siku mbili unaowakutanisha Wadau mbalimbali pamoja na Taasisi kubwa tatu, ambazo zinahusika moja kwa moja udhibiti wa pembejeo za kilimo kuanza udhibiti wa viuatilifu (Madawa), mbegu na mbolea. Taasisi hizo ni pamoja na Taasisi inayojishughulisha na masuala ya Udhibiti wa Mbegu Bora (TOSCI). Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) pamoja na Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI).
Thursday, February 7, 2019

Wataalam Wakutana Kujadili Namna ya Kupata Takwimu Sahihi za Kilimo


Wadau wa CAADP  kutoka  Wizara ya Kilimo,   Viwanda na Biashara, Wizara ya  Mifugo na Uvuvi,  TADB, NBS, SAGCOT, ANSAF wamekutana kujadili namna ya kupata takwimu halisi za kilimo nchi nzima.

Akizungumza na wataalam  hao katika Kikao kilichofanyika  tarehe 24-25/01/2019  katika ukumbi  wa   Senate, Jengo  la Utawala  Chuo  Kikuu  Dodoma Bi. Jackline Mbuya ambaye ni Afisa Kilimo Mkuu  amesema kwamba upatikanaji wa takwimu za uhakika utasaidia kuimarisha Sekta ya Kilimo

Aidha, Bi. Jackline amesema kwamba mpango wa kuwa na takwimu za uhakika ni muendelezo wa malengo waliyojiwekea  ikiwa  ni pamoja na kufufua na kuendeleza  Kilimo  barani Afrika  kwa kutumia rasilimali zilizopo kwa njia endelevu ili kukifanya kilimo kikue kwa asilimia 6 kwa mwaka .

Bi. Jackline amesisitiza kwamba matokeo ya kikao kazi hicho yatasidia taifa katika upatikanaji wa chakula, kuleta maendeleo vijijini na kuondoa umaskini kwa   kujikita katika Nyanja za Uchumi, Siasa na Jamii.

Awali Bi. Jackline alibainisha kwamba Mpango  wa  Kuendeleza   Kilimo  barani Afrika  (Comprehensive Africa Agriculture Development  Programme  CAADP) uliandaliwa na kuridhiwa na baraza la Mawaziri wa Kilimo.

Katika mkutano huo wa wakuu wa nchi uliofanyika   Julai 2003  Maputo Msumbiji  waliazimia kutekeleza  yatokanayo na maamuzi husika na walipitisha Azimio  la  kutenga asilimia 10 ya bajeti za Serikali zao kwa ajili ya kuendeleza Kilimo.

 Kutokana na kikao hicho wataalam wametakiwa kuwa na takwimu halisi za ukuaji wa  Kilimo ili ziweze kujazwa  na  kuwasilishwa  kwa matumizi  zikiwa ni takwimu za Kilimo za  nchi nzima.
Na. Beatrice Kimwaga                                       


Friday, January 18, 2019

FEDHA ZA UTEKELEZAJI WA ASDP 11


 Aliyekaa kulia ni Mratibu wa ASDP II Bwana Zakaria Muyengi akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalam kutoka Wizara za Sekta ya Kilimo waliohudhuria warsha hiyo.


Wataalam  kutoka  Wizara  za Sekta ya Kilimo, Taasisi zaSerikali na Sekta binafsi wamekutana kwa pamoja kwa lengo la kujadili namna ya upatikanaji wa fedha kwaajili ya Utekelezaji wa Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Mkutano huo umefanyika tarehe 14 na 15/01/2019 katika Ukumbi wa Economic Social Research Foundation uliopo maeneo ya Victoria jijini Dar es Salaam.Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na OR- TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kilimo,Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi, Wizara ya Maji, MIVARF,SAGCOT, TARI,MVIWATA,TADB,NBS,TAHA,DALBEG, BOT pamoja na TASAF


Akiongea na wataalam waliohudhuria mkutano huo,Mratibu wa ASDP II Bwana. Zakharia Muyengi kutoka Wizara ya Kilimo amesema kwamba ni jukumu la wadau wakuu watatu ambao ni Serikali, Wabia wa Maendeleo na Sekta binafsi kuhakikiksha kwamba fedha zinapatikana kwa ajili ya Utekelezaji wa Progam hii ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea kwa wakati.Hata hivyo ameendelea kusema kwamba Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ASDP 11 na tayari shughuli za kilimo zimekwisha anza kutekelezwa. Katika ASDP 1 kulikuwa na mfuko wa busket fund ambapo kama tungeutumia kwa sasa fedha hizo za wafadhili tungezikuta lakini Serikali kupitia bajeti zake imeendelea kutenga fedha na billion 236 tayari zimeshaingizwa kwenye akaunti. 

Aidha  Bwana. Muyengi amesema kwamba 59% ya fedha za kuendesha mradi huu zinatoka kwenye Sekta binafsi na ili tuweze kupata hizi fedha ni vizuri tukajua nani anaweza kuchangia. Katika maelezo yake amewakumbusha pia wataalam hao maagizo ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwamba bado kuna matumizi duni ya zana za kilimo, matumizi ya pembejeo za kilimo ni madogo ikiwa ni pamoja na mbolea,viuatilifu na kukosa masoko ya mazao ya kilimo.


Tuwe na Vikao vya kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais aliyoyatoa wakati wa Uzinduzi” Alisema Bwana. Muyengi


Naye Mratibu wa SAGCOT Bwana Gofrey Kirenga amesema kwamba  SAGCOT ilitokana na Utekelezaji wa ASDP 1, Hata hivyo imeonekana kwamba maeneo mengi tunayozalisha chakula cha kutosha hakuna Uwajibikaji na Usimamizi mzuri katika  Kilimo. Pia nchi zote zilizoendelea kwenye Kilimo shughuli za kilimo zinafanywa na Sekta binafsi na kazi ya Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri ya wafadhili kujiamini
Wednesday, January 9, 2019

Wizara ya Kilimo Kuja na Mkakati Kabambe wa Kuinua Zao la Chai NchiniHayo yamesemwa na Naibu waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa alipokuwa akiongea na Wananchi na wanachama wa Chama cha Ushirika cha wakulima wa Chai katika kijiji cha Mkonge wakati wa ziara yake ya kutembelea wakulima wadogo na wakubwa wa Chai Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.


Akiwa katika Kijiji cha Mkonge Kata ya Luhunga Tarafa ya Ifwagi Mhe. Naibu Waziri Bashungwa alieleza namna Wizara ilivyojiwekea mkakati wa kuinua zao la Chai nchini, ikiwa na  lengo la kumnufaisha Mkulima ili kulifikisha Taifa katika Uchumi wa kati kwani zaidi ya asilimia 65.5% nchini ni wakulima hivyo ni lazima kufunganisha Kilimo na Viwanda ili kufikia lengo hilo.


“Ni wakati sasa wa kuona zao la Chai linamnufaisha mkulima, nimeshawaelekeza bodi ya Chai Tanzania haraka iwezekanavyo tuleteeni ule mkakati wa kitaifa wa kufufua zao la Chai nchini na tutoke kwenye uzalishaji wa tani 34,000 za sasa na angalau kufikia tani elfu arobaini 40,000 kuwafikia wenzetu wakenya” alisema


Mhe. Bashungwa alisistiza kwamba ni lazima mkulima aone kwamba zao hili ni zao la kimkakati na linamuondoa kwenye umaskini kama Rais Dkt John Pombe Magufuli anavyotaka wasaidizi wake kuwasaidia wakulima ili kuwezesha taifa kufikia katika kipato cha kati kwa kuangalia fursa zilizopo.


“Uzalishaji wa chai kwenye upande wa masoko tayari tumeshaagiza bodi ya Chai kufikia mwezi wa Mei mwaka huu 2019 mkakati wa kuanzisha Soko la Chai Tanzania pale Jijini Dar es salaam unakamilika na kuhakikisha Chai inauzwa hapa nchini ili mwaka wa fedha wa 2020 unapoanza Julai tayari tunakuwa na mnada ili gharama za usafirishaji Chai nje zinapopungua basi faida ile ije kumsaidia mkulima” Alisema


Aidha ameitaka Bodi ya Chai Tanzania kueleza ni kwa nini wanapanga bei ndogo za ununuzi wa Chai kwa wakulima wakati wanunuzi wananunua zaidi ya ile bei ndogo iliyopangwa na wao, bodi ya Chai kupitia kwa Mjumbe wake Dkt. Emmanuel Simbua alieleza namna mchakato unavyofanyika wa upangaji bei na kuahidi kubadilisha viwango vya bei elekezi ya ununuzi wa chai kutoka kwa wakulima mwaka huu 2019 kwa kuwashirikisha wadau wote.


Kutokana na changamoto mbalimbali za wakulima kabla ya mwezi Februari kitafanyika kikao cha wadau wa Chai nchini hapa Mufindi kwa sababu ndipo asilimia takribani 70% ya uzalishaji wa Chai  nchini unafanywa katika Wilaya ya Mufindi na Njombe na hapo changamoto nyingi za wakulima wa zao hilo zitapatiwa ufumbuzi na hatimae kuwainua wakulima wa Chai nchini Tanzania.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William alisema Serikali imejitahidi kutafuta wafadhili na wadau mbalimbali ambapo leo hii Mhe. Mbunge alikuja na Wataalamu kutoka wakala wa barabara vijijini na mjini TARULA kutoka makao makuu Dodoma kwa ajili ya kushughulikia suala la barabara hii Km 40 kutoka Sawala hadi Lulanda ikiwa ni moja ya kupunguza changamoto ya miundombinu ya barabara ndani ya mashamba ya Chai ili kuzisafirisha kwa urahisi.


Akisoma risala Katibu wa Chama cha Ushirika wa wakulima wa Chai Mkonge Bwana Venusto Chang’a alieleza kwamba Changamoto nyingine ni mkulima kutoshiriki katika mnyororo wa thamani katika zao la chai kwa kuishia kuuza majani mabichi pekee na bei kubwa ya pembejeo inayopatikana bila ruzuku ya serikali.


Akijibu changamoto ya bei Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru alikiri changamoto hiyo na kusema kwamba tatizo hilo linatokana na mnada wa soko kuwa Mombasa Kenya hivyo wao kujipendelea lakini pia ubora wa chai hivyo Serikali tayari mkakati wake wa kuanzisha mnada wake Jijini Dar es salaam ili kusaidia bei kupanda unakamilika mwaka huu mwezi mei.


Mwaka 2017 chama hiki kilipata tuzo ya kuwa chama bora cha ushirika ngazi ya Mkoa na mwaka jana 2018 chama kilipata tuzo ya mshindi ngazi ya Taifa katika tasnia ya chai katika vyama vya msingi Tanzania sanjari na kufanikiwa kutoa Wakulima bora wa zao la chai kikanda na kitaifa kwa miaka mitano (5) mfululizo kuanzia mwaka 2008-2012.


Kilimo cha chai katika kijiji cha Mkonge kilianzishwa mwaka 1971 chini ya mamlaka ya chai Tanzania (MACHATA) au TTA wakulima waanzilishi walikuwa 174 ambao walimiliki hekta 118. Chama kilianzishwa mwaka 1989 kama kikundi cha wakulima baada ya Mamlaka ya chai Tanzania (TTA) Kusitishwa.


Lengo la kuanzishwa kwa chama hiki lilikuwa ni kuwaunganisha wakulima wa chai Mkonge katika kilimo cha zao la chai na kuwa na sauti moja katika kudai haki kutatua changamoto pamoja na kutafuta fursa.


KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO MHANDISI MTIGUMWE AIAGIZA NFRA KUNUNUA MAHINDI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, leo tarehe 07 Januari 2019, ameuagiza uongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuendelea kununua mahindi ya wakulima kwa bei ya sh. 450 kwa kilo. 

Mhandisi Mtigumwe ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Maafisa Kilimo wa Wilaya za Mkoa Wa Katavi, Wadau mbalimbali wa Kilimo wakiwemo mawakala wa pembejeo, wasindikaji, wawakilishi wa vyama vya msingi vya ushirika na wakulima, kilichofanyika katika ukumbi wa Polisi Wilayani Mpanda mkoa wa Katavi.

Katibu Mkuu huyo ameitaka NFRA kununua mahindi kwa wakulima kwani kufanya hivyo kutaimarisha soko la wakulima Wa mahindi nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Wizara ya Kilimo sambamba na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli la kutafuta masoko ya Mazao ya wakulima.

Alisema kuwa Wizara ya Kilimo imeanza mkakati rasmi wa kutafuta masoko ya Mazao mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha kikosi maalumu kitakachoshughulikia dhamira hiyo.

Akiwa katika ziara hiyo mkoani Katavi, Katibu Mkuu ametembelea maduka ya mawakala wa pembejeo za kilimo na kujionea hali ya upatikanaji wa pembejeo za mbegu na mbolea mkoani Katavi.

Alisema kuwa pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea ni nyenzo muhimu kwa mkulima katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo.

Pia, ametembelea maghala ya wafanyabiashara wa mbolea, kiwanda cha kusindika mahindi, mpunga na alizeti.

Katika hatua nyingine katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe amesema kuwa Wizara ya Kilimo ipo katika mapitio ya sifa za Viongozi wa vyama vya ushirika nchini ili kupata viongozi watakao ongoza kwa weledi sekta ya Ushirika nchini.

Alieleza kuwa zipo nafasi za uongozi katika vyama vya ushirika ambazo zinahitaji utaalamu na si tu kuchagua kiongozi anayejua kusoma na kuandika, mfano Mhasibu.

Alisema, dhana ya kuchagua viongozi wa Ushirika wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika imeanza kupitwa na wakati hivyo yanahitajika mabadiliko jadidu katika sekta hiyo.


WIZARA YA KILIMO IPO KATIKA MAPITIO YA SIFA ZA VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA – MHANDISI MTIGUMWE


Wizara ya Kilimo ipo katika mapitio ya sifa za viongozi wa Vyama vya Ushirika nchini ili kupata viongozi watakao ongoza kwa weledi sekta ya Ushirika.Dhana ya kuchagua viongozi wa ushirika wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika imepitwa na wakati hivyo kuna kila sababu ya kuchagua viongozi wenye weledi na utashi katika utendaji.


Hayo yameelezwa jana tarehe 8 Januari 2019 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe wakati akizungumza kwenye kikao kazi na maafisa wa Kilimo wa Wilaya za Mkoa wa Rukwa, Wadau mbalimbali wa Kilimo wakiwemo mawakala wa pembejeo, wasindikaji, wawakilishi wa vyama vya msingi vya ushirika na wakulima, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.


Alisema kuwa mfumo wa ushirika  ni nyenzo muhimu ambayo ukitumika vizuri itasaidia kuondoa  umaskini wa wakulima hapa nchini na utaimarisha uanzishwaji wa viwanda kuleta tija katika kilimo hivyo ni lazima kuwa na juhudi za makusudi kuwa na viongozi wenye weledi.


Katibu Mkuu huyo katika ziara yake mkoani Rukwa alitembelea maduka na maghala ya mbolea yanayomilikiwa na kampuni za ETG, YARA na PREMIER na kujionea hali halisi ya upatikanaji wa mbolea ambapo amepongeza utoshelevu wa mbolea uliopo mkoani humo.Akizungumzia swala la masoko ya mazao ya wakulima Mhandisi Mtigumwe alisisitiza kuwa ubora wa mazao ya wakulima ni suala la msingi kulizingatia ili kuweza kusaidia wakulima kupata masoko ya uhakika na kujiongezea kipato, kwani mazao bora yana ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.Kuhusu Milipuko ya visumbufu vya mimea, Mhandisi Mtigumwe alisisitiza kuwa ili kunusuru mazao ya wakulima nchini, hatua madhubuti zinaendelea kuchukuliwa ili kuweza kudhibiti wadudu wanaothiri mazao akiwemo Kiwavijeshi Vamizi (FAW).Hivyo, alitoa rai kwa Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa na Makatibu Tawala wote nchini, kuwaagiza Maafisa Kilimo kufanya tathmini ya awali na kubaini maeneo ambayo kiwavijeshi vamizi ameanza kuonekana ili Wizara kwa kushirikiana na halmashauri ziweze kuchukua hatua za kudhibiti milipuko ya kiwavijeshi vamizi kabla hajasambaa zaidi na kuleta athari kubwa.


Tuesday, January 8, 2019

SERIKALI KUSAINI MIKATABA YA UBANGUAJI WA KOROSHO JANUARI 10


Serikali imesema kuwa tarehe 10 Januari 2019 itasaini mikataba na wamiliki wa viwanda vya ubanguaji wa korosho waliojitokeza kwa ajili ya kubangua korosho za serikali za msimu wa mwaka 2018/2019 zilizonunuliwa na serikali kwa bei ya Shilingi 3300 kwa kilo.Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 8 Januari 2019 wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara.


Alisema kuwa hivi karibuni serikali ilitangaza kuwa korosho ghafi zote zitabanguliwa nchini hivyo utekelezaji wa jambo hilo umeanza, ambapo Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko itaingia mikataba ya ubanguaji.


Pamoja na wamiliki wa viwanda kupewa kazi ya kubangua korosho lakini pia serikali imewakaribisha wananchi kujitokeza kubangua korosho za serikali kupitia vikundi au mtu mmoja mmoja. “Wananchi wenye uwezo wa kubangua tunawaomba waende Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo-SIDO) kwa ajili ya kujiandikisha ambapo mpaka sasa watu 126 kwa ajili ya ubanguaji na Tani 29 zimechukuliwa kwa ajili ya kuanza kubanguliwa” Alisisitiza Mhe Hasunga


Katika mkutano huo Waziri huyo wa kilimo Mhe Japhet Hasunga amempongeza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kushuhudia utiaji wa saini mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) wa Bilioni 21 zitakazoiwezesha NFRA kunua mahindi kwa wakulima hivyo kuimarisha soko la nafaka nchini.


Mhe Hasunga alisema kuwa pamoja na kuanza ubanguaji kupitia SIDO lakini serikali imeanza mchakato wa kukufua viwanda vya ubanguaji vya serikali na watu binafsi nchini ili kuongeza ajira kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya wabanguaji wadogo wadogo.


Akizungumzia kuhusu swala la malipo ya korosho na uhakiki wa wakulima alisema kuwa tayari kiasi cha korosho ambayo imekusanywa kwenye maghala makuu ni Tani 203,938.3 wakati korosho iliyopo kwenye Vyama vikuu vya ushirika ni Tani 29,803.53 inayofanya jumla ya korosho yote iliyopokelewa kwenye vyama vya ushirika na maghala makuu kuwa Tani 233,741.83 sawa na asilimia 84.7 ya lengo lililowekwa la ukusanyaji katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani.


Kuhusu malipo ya wakulima alisema kuwa miamala ya malipo ambayo imefanyika ni 261,458 yenye jumla ya watu 203,569. Aidha, vyama 490 vilimelipwa kati ya vyama 617, Alisema Mkoa wa Mtwara jumla ya vyama 39 bado havijalipwa, Mkoa wa Lindi vyama vitano na Ruvuma viwili hivyo serikali imejipanga ndani ya wiki mbili vyama hivyo kuwa vimelipwa.


Waziri Hasunga amesema kuwa mpaka kufikia jana tarehe 7 Januari 2019 fedha ambazo zimeingizwa kwenye Account za wakulima ni zaidi ya Bilioni 257 huku ambazo tayari zimeingia kwenye Account za wakulima ni Bilioni 226.2 ambapo Zaidi ya Bilioni 30.7 zilizohakikiwa bado hazijaingizwa kwenye Account za wakulima kutokana na taarifa za baadhi ya wakulima hao kutofautiana majina ama vinginevyo. “Tunawaomba sana wananchi kwenda Benki kujiridhisha kama Account zao zinafanya kazi kwani serikali ina fedha za kuwalipa wakulima wote wa korosho” Alisema


“Tena nisisitize kwa wale wanaofanya biashara ya korosho kinyume na utaratibu maarufu kama (Kangomba) wajisalimishe na kuomba radhi wenyewe kuliko kusubiri serikali iwabaini” Alisema


Vilevile, Mhe Hasunga alisema kuwa wizara yake imeweka mikakati mbalimbali ambapo hadi kufikia Januari 31 mwaka huu zoezi la uhakiki wa wakulima wanaostahili kulipwa liwe limekamilika ambapo zaidi ya asilimia 80 ya wakulima wawe wamelipwa.


Pia amewataka wananchi kupuuza taarifa mbalimbali zizotolewa na baadhi ya wananchi wasiolitakia mema Taifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa serikali hailipi wakulima badala yake amesisitiza kuwa serikali ina fedha za kutosha kulipa wakulima wa korosho isipokuwa kangomba wao hawatalipwa


IFIKAPO JUNI 2019 WAKULIMA WOTE WATAKUWA WAMESAJILIWA NA KUWA NA VITAMBULISHO – MHE HASUNGAWizara ya Kilimo imeanza kuandikisha wakulima nchini kwa lengo la kuwatambua ili kuwarahisishia huduma mbalimbali zikiwemo uhitaji wa pembejeo za kilimo.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo wakati akizungumza na Wenyeviti na makatibu wa Vyama vya Msingi kwenye kikao kazi  kilichofanyika leo tarehe 6 Januari 2019 katika Ukumbi wa Claster Mjini Tunduru katika Mkoa wa Ruvuma.


Akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani Tunduma Waziri huyo amesema kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa taarifa zinazohusu uandikishwaji wa wakulima kuwa una lengo baya, hivyo amewataka wakulima hao kutosikiliza propaganda hizo zisizo na tija kwani utambuzi wa wakulima ni jambo la kawaida kufanya utambuzi.


Alisema kuwa kuandikisha kwa wakulima ni njia pekee ya kuwa na takwimu sahihi kwa kutambua idadi ya wakulima, vijiji na Kata wanazolima ikiwa ni pamoja na kutambua ukubwa wa mashamba yao kwani kufanya hivyo serikali itakuwa na urahisi wa kuwahudumia wakulima hao.


Katika hatua nyingine Mhe Hasunga amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe Juma Homera kwa kusimamia vyema sakata la korosho kwa kusikiliza kesi 11 huku zikifikishwa mahakamani kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.


“Nakupongeza sana Mhe Homera kwa usimamizi madhubuti katika kudhibiti kangomba nilipata taarifa kuwa Kg 17,679 za korosho mmezikamata pamoja na zingine Kg 2,779.2 jambo hilo ni zuri endeleeni kusimamia vyema majukumu ya serikali ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020” Alikaririwa Mhe HasungaKwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe Juma Homera aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuanza kuwalipa wasafirishaji wa korosho kutoka maghala ya vyama vya msingi, kuwalipa gharama za uendeshaji kwa vyama vya masingi, kuwalipa watunza maghala na magunia sambamba na kuondoa mzigo kwa wakati kutokana na ghala kuezuliwa na upepo lililokuwa na jumla ya Tani 536.Pamoja na pongezi hizo pia Homera amezitaja changamoto mbalimbali katika Oparesheni korosho kuwa ni pamoja na kuchelewa kwa malipo ya wananchi waliofanyiwa uhakiki, utaratibu wa upatikanaji wa miche ya korosho kwa msimu wa mwaka 2018/2019, na mkanganyiko wa upatikanaji wa mapato ya Halmashauri 3% ya bei ya korosho.


Thursday, January 3, 2019

WAZIRI MKUU AFUNGUA SOKO LA MAZAO SONGEA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amefungua mradi wa maghala ya kuhifadhi nafaka na soko la mazao la OTC-Lilambo katika Halmashauri ya Songea uliogharimu sh. bilioni 1.5.

Amesema Rais Dkt. John Magufuli ameazimia kuwawezesha wakulima kuwa na mahala pa uhakika pa kuhifadhia mazao yao na sehemu ya kufanyia biashara ili kuwaongezea tija.

Amefungua soko hilo leo (Alhamisi,  Januari 3, 2019) akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku nne ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Ruvuma.

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ujenzi wa soko hilo pamoja na maghala kwani umezingatia viwango. Maghala hayo mawili yana uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 za nafaka.

“Licha ya soko hili kuwapa wakulima wetu fursa ya kupata masoko ya kuuzia mazao yao, pia  watapata mafunzo ya namna ya kuhifadhi bidhaa zao pamoja na taarifa za masoko.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza bodi ya soko hilo kuhakikisha inatoa matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari ili wakulima waweze kupeleka mazao yao sokoni hapo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka wananchi kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha nchini kuandaa mashamba, kupanda mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

“Nawaagiza viongozi wa kata na vijiji hakikisheni wananchi katika maeneo yenu wanaandaa mashamba na kupanda kwa wakati, tunataka tuwe na chakula  cha kutosha na ziada tuuze.”

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Songea, Martin Mtani ameiomba Serikali iwapatie mashine itakayowawezesha kupanga madaraja ya mazao ya nafaka mbalimbali.

Mkurugenzi huyo ameomba soko hilo liwekwe kwenye mpango wa kujengewa vihenge vyenye uwezo wa kukausha mazao kwa viwango vya kimataifa ili kutatua tatizo la unyaufu.

Pia Mkurugenzi huyo ameiomba Serikali iwasaidie katika kuliunganisha soko hilo na TMX ili waweze kuuza mazao ya nafaka ndani na nje ya nchi .

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme na maafisa wengine wa Serikali.


Wednesday, January 2, 2019

Waziri Hasunga aziagiza Bodi za Mazao nchini kuwasajili Wakulima wote

Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga (Mb)  amewaagiza Wakurugenzi wa Bodi za Mazao kuanza mara moja zoezi la kuwatambua na kuwasajili wakulima wa mazao yote nchini lengo likiwa kuwatambua ili kupanga mipango sahihi yenye kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yote.

Ametoa agizo hilo jana tarehe 29 Disemba 2018 wakati akizungumza na Wenyeviti wa Bodi za Mazao pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hizo za Mazao, kwenye ukumbi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma.

Mhe. Hasunga amesema ili kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta ya kilimo na kuandaa mipango madhubuti ya kuendeleza mazao yote ni vyema kuwatambua Wakulima wote nchini na kuongeza kuwa Wakulima wa zao la korosho wametoa funzo kubwa kwa  Wizara yake kufanya jambo kama hili katika mazao mengine hapa nchini.

Itakumbukwa kuwa wiki tatu zilizopita, Waziri Hasunga alitoa agizo kwa Bodi ya Korosho agizo kuandaa daftali maalumu la kuwatambua Wakulima wa korosho kote nchi ambapo moja ya taarifa ambazo zitajumuishwa katika daftali hilo ni pamoja na Jina Kamili la Mkulima,  Mkoa, Wilaya, Kata na Tarafa anayotoka.


Mambo mengine ni pamoja na Kitongoji, Mtaa au Jina la Kijijini anapotoka, mahali lilipo shamba pamoja na ukubwa wa shamba lake.

Waziri Hasunga ameongeza kuwa mipango sahihi ya kuwaendeleza Wakulima kuanzia kwenye kilimo chenyewe hadi kufikia katika hatua ya kuvuna, kuhifadhi na kulifikia soko ni vyema kuwa na mfumo maalumu wa kanzi data (Database) ya kuwafahamu ili kushughulikia mahitaji yao kisasa na kwa haraka zaidi.

Waziri Hasunga alienda mbali na kushauri matumizi ya TEHAMA na ya Mfumo wa GPS ili kuboresha daftari hilo kwa lengo la kuboresha uwekaji wa taarifa za Wakulima na maeneo wanayotoka Wakulima kwa usahihi zaidi.

“Tumepata changamoto kadhaa wakati wa kuwahakiki Wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma na kama Bodi ya Korosho ingekuwa makini kuandaa daftari la Wakulima zoezi la uhakiki lingekuwa rahisi, kwa ajili hiyo niliwaagiza Bodi ya Korosho kukamilisha zoezi hili mpaka Mwezi Machi, 2019 na Bodi za Mazao zilizobaki ukiacha Bodi ya Tumbaku ambao wao tayari walishafanya hivyo, kukamilisha Mwezi June, 2019”. Amekaririwa Mhe. Hasunga.

Waziri ameitisha kikao maalumu na Viongozi wa Bodi za Mazao, Wakala na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuboresha mikakati na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Wizara pamoja na kujitathmini kabla ya kufikia nusu mwaka wa utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya Wizara ya mwaka 2018/2019 ili kujipanga kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya kilimo ya mwaka ujao wa 2019/2020.

Bodi za Mazao zilizoshiriki mkutano huo ni pamoja na Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba, Bodi ya Mkonge, Bodi ya Pareto, Bodi ya Chai, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Bodi ya Sukari.

Wakala zilizoshiriki ni pamoja na  Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA) Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTDA).

Taasisi nyengine za Wizara ya Kilimo zilizoshiriki ni pamoja na Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI), Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Ukanda wa Kitropiki (TPRI), Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) na Bodi ya Leseni za Maghala.

MWISHO